Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia siku ya leo kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza nimshukuru Waziri na Naibu wake wamekuwa wasikivu unapowaambia jambo, tunamshukuru kwa sababu ni sifa pia ya kiongozi kuwaheshimu wenziwe na kusikiliza mawazo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitajikita kwenye Fungu 64 - Uvuvi. Amezungumza kaka yangu Mbunge wa Kigoma hapa, tunasimama leo hapa tension iliyopo kwenye Mkoa wa Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa tunatamani tusikie kauli ya Mheshimiwa Waziri leo, masikio na macho ya wavuvi wa mikoa mitatu toka jana wanasubiri neno kwa Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Rukwa na Katavi tunategemea Ziwa Tanganyika, Ziwa Tanganyika tuna – share zaidi ya Nchi nne kwa maana ya Tanzania yenyewe, Kongo, Zambia pamoja na Burundi. Kongo inatumia kwa asilimia 45 ya Ziwa Tanganyika. Tanzania asilimia 41, hizo nchi nyingine hizo mbili asilimia inayobaki ndiyo wanatumia wao. Unapoingia makubaliano ya kufunga ziwa na hizo nchi ambazo zina asilimia ndogo lengo ni nini, tunakwenda kumnufaisha nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wengine wanaweza wakazungumza korosho ndiyo uchumi wao, madini ndiyo uchumi wao. Uchumi wetu ni Ziwa Tanganyika, ndiyo duka letu. Wavuvi hawa kwa sababu shughuli wanayoifanya ni halali ndiyo maana wanakata leseni kwa Serikali. Leo wamekata leseni ya mwaka mzima, Serikali inasema inakwenda kufunga Ziwa kwa miezi mitatu, watuambie, waliwashirikisha hawa wavuvi kwamba wanakwenda kufunga Ziwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atakapokuja atuambie tafiti zake zinasema ni samaki wa aina gani wamepungua? Kwa sababu hawezi kusema anakwenda kufunga ziwa wakati pale kuna dagaa, kuna aina nyingi za Samaki. Kama tafiti zake ni sahihi lazima waje watuambie wamegundua ni samaki gani? Hawa ndiyo wafungiwe, huwezi kufunga ziwa kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujiulize kwa nini tumefika hapa, lazima Wizara yako ijue kwa nini tumefika hapa? Kama ni kwa sababu nyepesi mnazotupa kwamba ni kupungua kwa samaki, kwa nini samaki wamepungua? Je, miezi mitatu ndiyo mmeona ni suluhisho la kurudisha samaki kwenye Ziwa Tanganyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupungua kwa samaki hakujapungua Ziwa Tanganyika peke yake na Maziwa mengine yote kuna upungufu wa samaki. Sasa kama sababu ni kupungua kwa samaki Serikali isije na majibu mepesi kwenye mambo magumu, lazima tuje na mkakati wa kudumu wa kuhakikisha tunazuia uvuvi haramu ndiyo changamoto ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza lazima uanze na kanuni zenu. Kanuni za uvuvi ni kanuni za ajabu sana, ambazo leo kuna kanuni zinakwenda kuwakandamiza wavuvi na kuwapa umasikini. Leo unaposema unakwenda kufunga Ziwa hujamshirikisha huyo mvuvi ambae unakwenda kufunga Ziwa, na ukiamini ndiye mwenye duka na leseni amekata. Mheshimiwa Waziri tukuite jina gani? Kwa sababu kama umechukua fedha za leseni ya mwaka mzima halafu unamfungia shughuli ambayo amekatia leseni, tuseme ni nini, uporaji? Tutumie lugha gani ambayo itafaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama Serikali ina nia njema kuongeza Samaki, kufunga ziwa miezi mitatu siyo suluhisho. Tuchukue hizo fedha ambazo mmetenga kwa ajili ya kufanyia patrol, kuwapiga wananchi ambao wanafanya kazi halali, shughuli halali, tukajenge vizimba ambao itakuwa mbadala wakati ambao tunasema tunasimamisha kwa muda ili Ziwa lipate Samaki, wananchi wawe na sehemu mbadala ya kupata kitoweo lakini kuweza kuendesha familia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwneyekiti, pamoja na ujengaji wa vizimba napenda nishauri Mheshimiwa Waziri, mkiwa na ushirikishwaji mtaleta uelewa wa pamoja, tukiwa na uelewa wa pamoja tutafanya uwajibikaji wa pamoja. Tukitoka kwenye uwajibikaji wa pamoja tutakwenda kufanikisha kwa pamoja malengo chanya tuliyojipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hatuwezi kufikia huko kwa sababu hatujawashirikisha hawa wananchi. Nchi hii ni ya kwetu sote na kama ni ya kwetu tusiwaone hawa watu, kwa sababu kama kwa mujibu wa Katiba inatambua kazi hii kwamba ni kazi halali. Tukienda kuamua bila kuwashirikisha ni suala ambalo halikubaliki nasi Wawakilishi kwa sababu hamjatuambia au hamjatushirikisha, hatutakubaliana na hilo jambo kwa sababu halina nia njema kwa wananchi wetu, halina nia njema kwa wavuvi wetu na kwa sababu tunajua Wilaya kama ya Nkasi inategemea uchumi kutoka Ziwa Tanganyika, kwa hiyo ukienda kufunga unategemea na ile Halmashauri itaishije? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka Waziri aje atueleze hapa, utafiti walioufanya na je, wamewashirikisha wananchi? Kama hawajawashirikisha wazo letu kwa pamoja Wabunge wa Mikoa Mitatu kwa sababu na sisi tunahitaji samaki wengi, turudi kwanza kuwashirikisha wananchi wetu ambao ni wavuvi. Tuwashirikishe wadau wote wa uvuvi na haya mambo hakuna sababu ya kugombana kama kweli nia ni njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena tunajua hili jambo Waziri ulisema lakini tunataka leo wavuvi wetu wapate kauli moja, lini utawashirikisha kabla ya kufanya hayo maamuzi mliyopanga Tarehe 15, ili na wao watoe mawazo yao kwa sababu lengo ni kujenga nchi yetu na kuchangia Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kufikia huko Mheshimiwa Waziri unaposikiliza yafanyie kazi mawazo ya wavuvi. Wavuvi wameshakuja mara kadhaa kulalamikia baadhi ya kanuni ambazo hazifai. Hizo kanuni ambazo tunazitoa leo ni lazima tuwe na lugha moja, hivi leo ukifunga Ziwa unasema tumekubaliana na Congo, ninyi mtapata nguvu wapi ya kwenda kuangalia Congo kama wamefunga hawatavua? Lakini kwa hali ya kawaida hivi huyu Zambia mwenye asilimia ndogo sana umekubaliana naye, unakubaliana naye kwa ajili ya nani? Sisi tunakubaliana kwa ajili ya wananchi.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Aida muda wako umeisha.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)