Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa fursa hii kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu. Nami nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa na Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ridhaa yako nisome kwenye randama ambayo imewasilishwa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kulikuwepo hoja nyingi sana ambazo zimejibiwa kwenye randama. Hoja namba sita ilikuwa inahusu ugawaji wa vitalu katika eneo la Ranch ya Mwisa II, na Wizara katika hiyo hoja imejibu. Naomba nisome. Serikali inasema, na ninaomba watu wangu wa Muleba wasikie. “Zoezi la ugawaji wa vitalu katika Ranch ya Mwisa II haliendelei.” Hiyo ni kauli ya Wizara ambayo naamini ni kauli ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendeleo kusoma. “NARCO inasubiri maelekezo ya Serikali baada ya Kamati ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kumaliza kazi yake iliyokuwa ikiifanya katika eneo la Mwisa II.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na ninaomba atakapokuja kuhitimisha hotuba yake, haya maneno ayaseme na ayawekee msisitizo na mkazo ili watu wangu wa Muleba ambao wameteseka sana, wananyanyaswa, wanaambiwa waondoke kwenye hili eneo ambalo ni eneo la makazi yao, kuna babu zao walizikwa pale, kuna makaburi yao, lakini leo unapokuja kuwaambia waondoke, Mheshimiwa Waziri haikubaliki hiyo, na hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru watu wa Kigoma kwa mshikamano wao kuhakikisha kwamba Ziwa Tanganyika halifungwi. Nawapongeza kwa mshikamano wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Mwisa ni eneo la wananchi wa Muleba. Nimesoma kwenye randama na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anasema, mmiliki wa Mwisa na Rutoro ni NARCO. Tangu lini? Kwa mamlaka ipi? Utakapokuja kuhitimisha hii hoja Mheshimiwa Waziri, naomba utuambie, kama eneo la Mwisa II na Rutoro ni mali ya NARCO, kwa nini tuna Hati za Vijiji ambavyo vimesajiliwa na tumepata hati za mwaka 2000? Inakuwaje Mheshimiwa Waziri? Mheshimiwa Waziri utakuwa mtu wa kwanza kuhamisha watu kutoka kwenye vijiji kuwapeleka mbugani na kuwaleta ng’ombe waishi kwenye vijiji, haikubaliki. Hii tutaiingiza kwenye vitabu vya Guinness sijui ya mwaka gani! Haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mwisa II limechukua muda wetu mwingi sana. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anaongelea migogoro ambayo imezaliwa mwaka 2022/2023 zaidi ya migogoro 55. Anasema wametatua migogoro 13 tu, ina maana NARCO kazi yake na Wizara ni kuingia na kutatua migogoro ambayo wanaisababisha wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 30 Juni, 2022 tulikaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alituita kwa ajili ya kujadili suala la Mwisa na suala la Rutoro. Kati ya maazimio tuliyofikia, tulisema suala la Mwisa lisimame mpaka hapo tutakapopata suluhu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Nakushukuru umelitamka hilo Mheshimiwa Waziri. Nakuomba hayo uliyoyasema yawe ni maneno ya kweli na hao watu ambao wanapita huko Muleba kwenye hayo maeneo yenye mgogoro, wanawaambia wananchi wahame, sijui wawapishe wawekezaji; Mheshimiwa Waziri nakuomba, utakapokuja kuhitimisha utoe kauli yenye uhakika hapa ili watu waendelee na maisha yao. Naomba Serikali itamke, kama tunasubiri taarifa ya Waziri Mkuu, wananchi ambao waliishi kwenye hivi vijiji, waendelee na kazi zao za kuzalisha mali, na waendelee kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea hapa nadhani wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu, nilisema lile eneo la Mwisa ni kubwa. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema ni hekta 66,000, lakini naweza kusema ni zaidi ya hapo. Ndiyo maana tunaomba hili eneo likapimwe upya, vile vitalu vikapimwe upya, tukafanye uhakiki wa lile eneo. Sisi wakazi wa eneo hilo, tunalijua, siyo hizi hekta 66,000 alizotuambia, hapana, ni zaidi ya hapo. Tukishalipima upya, tukapanga matumizi bora ya lile eneo, tunakubali ndio, kaleteni wafugaji, lakini lazima lile eneo tukishalipanga tuhakikishe kwamba, tunatunza na mazingira ya lile eneo. Tunataka tupate maeneo ya kulima, tupate maeneo ya ufugaji na tupate maeneo ya mifugo kwa kutunza ikolojia ya Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, lile eneo la Mwisa ndiyo eneo linalozalisha chakula kinacholisha Wilaya ya Muleba na Mkoa wa Kagera. Tunaposema tunakwenda kuweka wafugaji pale, tunautangazia njaa ambayo haitakuwa na ukomo Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili tuliangalie. Naomba nisisitize na nitaendelea kulisisitiza suala la Mwisa II na NARCO ni maeneo ya vijiji vya wananchi. Ni vijiji vilivyosajiliwa na Serikali hii ambayo inasema ni vitalu. Sasa kupanga ni kuchagua; kama tutasema ni vitalu, then tutangaze. Serikali itoe tangazo kwa wananchi wote kwamba vile siyo vijiji ni vitalu, then wananchi mkawapangie maeneo mengine ya kuishi, siyo kuwaachia wenyewe watafute mahali pa kwenda. Haiwezekani! Hii nchi yao, wamezaliwa kwenye vijiji vyao, lazima tuwaheshimu na tuwape heshima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uvuvi, Kata ya Mazinga wamenituma nimwombe Mheshimiwa Waziri ifuatavyo: Kata ya Mazinga tuna kikundi kimoja kinaitwa UWAMAKAMA, wanasema waliomba mkopo, kwenye mikopo iliyotolewa na Wizara, lakini bahati mbaya hawakupata mkopo, hawaku- qualify, lakini wametekeleza vigezo vyote. Wanaomba kwenye mgawo wa mkopo ujao wapatiwe mkopo kwa ajili ya kufuga samaki wa vizimba. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Ishengoma. Muda wako umeisha.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)