Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo. Kwanza nitangulize pongezi kwao Wizara nzima akiwemo Waziri mwenyewe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Makatibu wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ambalo ninapenda kusema ni kwamba kwa Tanzania tumekuwa na figures za mifugo kila mwaka tunaongeza. Lakini ukijaribu kuangalia takwimu zetu sijui kama tunazo takwimu ambazo ni sahihi. Tunasema leo tuna ng’ombe milioni 36.6, mbuzi milioni 26.6 na kondoo milioni 9.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukijaribu kuangalia kwa idadi ya mifugo tulionao na mchango kwenye Pato la Taifa kidogo inafikirisha. Ni lazima tujiulize kama Taifa kwamba tunajali mifugo kama kitega uchumi au tunaona mifugo kama tatizo kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo hii tukijaribu kuangalia Nchi kama Ethiopia ina mifugo zaidi ya milioni 70, lakini hatusikii Serikali yao ikisema kwamba mifugo wamekuwa ni tatizo. Lakini sisi Tanzania tumewatangulizia wafugaji tunawaona kama tatizo kwenye nchi hii. Ukishamtangulizia mtu ukamuona kama tatizo, huwezi ukamsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tu-change mentality kama Serikali ili wafugaji tuwaone kama ni watu ambao nao kwenye nchi hii tunaweza kuwasaidia wakaongeza uchumi wetu na maisha yao yakaimarika. Lakini tukiwaona kama tatizo tutaendelea kuwalaumu kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la hereni, kaka yangu, Mheshimiwa Musukuma pale, alizungumza, lakini binafsi pia wananchi wangu kila siku wamekuwa wakilalamika kuhusiana na suala la hereni. Binafsi sioni kwamba ni kitu ambacho kitatusaidia kujua idadi ya mifugo Tanzania. Kinachotakiwa, kama tunataka kujua idadi ya mifugo tulionao tuendeshe sensa kwa kila wilaya; tuna wakuu wa wilaya, tuna ma-DAS, tuna wakurugenzi, tuna watendaji wa vijiji, tuna watendaji wa kata, wafanye hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo tunakwenda tena kuwatoza Watanzania wenzetu, wafugaji, fedha kwa ajili ya kuhesabu mifugo yao. Sisi kama Serikali tuwekeze ili tupate kujua idadi ya mifugo na ili tuweze ku-accrue economic bases kutoka kwa wafugaji. Siyo tunawaona wafugaji kama tatizo. (Makofi)

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Edward Kisau.

TAARIFA

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa kwamba idadi ya mifugo tayari inajulikana. Tumeambiwa hapa ni milioni 30. Kwa hiyo sasa sijui wanakwenda kufanya nini tena.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa inapokelewa kwa mikono yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama wafugaji ambao tumekuwa kwenye ufugaji kuanzia utotoni mpaka sasa hivi tunajua mifugo ni mali, ni dawa na ni kitanda kwetu. Kwa sababu mfugaji nalalia ngozi, nakula nyama, nakunywa maziwa. Nikiugua nachinja mifugo kwa ajili ya kuleta afya yangu ijirudie katika hali ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wengine Tanzania tumewaona wafugaji kama ni watu ambao hawafai. Hata kwenye vyombo vya habari tunawaona wafugaji kama ni watu ambao ni wa kutoka hapa kwenda pale kila siku, kuzunguka. Kwa nini wafugaji wanazunguka Tanzania nzima; ni kwa sababu tumewanyang’anya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia kwa Wilaya yangu ya Ngorongoro kabla ya eneo lile la Pori Tengefu kutengwa hatujawahi kuhamahama lakini mwaka huu itakuwa mara ya kwanza kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuhama kwenda kutafuta malisho kwa sababu tumewanyang’anya ardhi yao. Na ili tuone ni tatizo baada ya lile eneo la pori tengefu kutengwa, mifugo zaidi, ng’ombe 5,780 wamekamatwa kwenye lile eneo, na Serikali kuwatoza zaidi ya shilingi milioni 578. Kwa sababu hawana malisho itabidi waende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima kama Wizara, sijui kama ndugu yangu, Mheshimiwa Ulega, wafugaji Tanzania hii – ukimuona Waziri wa Maliasili ana wivu na tembo wake, sasa sijui wewe utakuwa na wivu na mifugo? Kwa sababu Watanzania wafugaji wanaumia kwenye hii nchi. Hatujawahi kumsikia Waziri wa Mifugo akizungumza hadharani na kukemea tabia ya wafugaji kukamatwa na kutozwa shilingi 100,000; hatujawahi kumsikia. Kwa nini tusisikie, na wewe umepewa na Rais Wizara hii usimamia uweze kuwatendea haki wafugaji wa nchi hii. (Makofi)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Sasa sijui kama kuna Wizara…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kweli Waziri wa Mifugo anatakiwa awaonee wivu wafugaji wake; wanakamatwa, wanatozwa faini, na wengine, mfano Yohana Mahona aliuziwa ng’ombe wake 1,221 na alishinda kesi Waziri hajatoa tamko. Lakini kuna Shabani Roya wa Ngorongoro, ng’ombe 170, alishinda kesi lakini Waziri hajatoa tamko. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Emmanuel, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa inayopokelewa kwa mikono yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe taarifa kwamba Desemba mwaka jana familia 27 walitaifishiwa ng’ombe 1,922 Ngorongoro. Mpaka leo familia hizo zimekuwa maskini. Kwa hiyo, niombe pamoja na masuala mengine tuwatafutie wafugaji wetu maeneo ya malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hawezi kukunyima fedha ukiwa na big vision lakini ukiwa Waziri unayekaa kila siku, kama walivyosema wengine, ni lazima ufikirie namna ya kuwakamua hawa wafugaji wa nchi hii. Tumechoka kuonewa kwenye nchi hii. Tunahitaji na sisi tuthaminike na tuweze kuchangia uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la chanjo; nashukuru umetuletea dozi 1,200 za PPR. Lakini toka mwezi Septemba mwaka jana mpaka sasa hivi hawajachanja mifugo kwa
sababu kwenye wilaya zetu wewe unapeleka chanjo lakini huna fedha za operesheni kwa ajili ya kufanikisha. Sasa sijui chanjo zitakwenda kwa mifugo yenyewe? Tunahitaji gari na fedha kwa ajili ya wataalamu kwenda kuchanja mifugo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechukua muda wangu kwa taarifa, naomba uniongezee.

MWENYEKITI: Hapana Mheshimiwa, taarifa ni sehemu ya mjadala.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)