Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi pia na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kushuika nafasi hii. Naamini nyie ni vijana, Mheshimiwa Rais anaelewa kazi ya ufugaji iko vijijini na sio vijijini tu, maporini na ndiyo maana amewateua nyie vijana ili mweze kufika huko kuonana na wafugaji. Baada ya kuyasema haya; mimi ni Mjumbe wa Kamati kwa hiyo kuna mambo ambayo tuliyaona hasa kwenye ziara na nilikuwa natamani kuishauri Wizara na ikiwezekana Bunge tuweze kusaidia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea miradi, hasa ule mradi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo. Tulitembelea Bwawa la Matekwe Nachingwea. Mmpaka ufike Nachingwea kwanza ni safari ndefu sana ambayo kwa kweli unafika umechoka, lakini kutoka Nachingwea penyewe mjini kwenda huko Matekwe kwenye hilo bwawa ni kilometa 154. Kwa hiyo unaweza uka imagine ni kiasi gani Kamati iliingia ndani na iliingia ndani kweli kweli maporini. Kwa nini nayasema haya, jana wakati nawasilisha taarifa ya Kamati, nadhani mtakua mlisikia nyote, kwamba thamani ya bwawa tuliyoikuta kule ilikuwa haiendani na uwekezaji ambao tuliambiwa. Sababu kubwa ambayo tuliiona kama Kamati; engineers wapo wawili, sijui watatu nchi hii, wazunguke wao kushughulikia miradi yote hii ni, ngumu kufanya hicho kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni mashahidi, tunao ma- engineers kwenye majimbo yetu au Wilayani lakini bado hawajaweza kufika sehemu zote hizo, sasa Engineer mmoja kuweza ku manage miradi ambayo inapitishwa na Wizara hapa ni ngumu, na ndiyo maana tukaja na pendekezo kama Kamati jana. Kwamba, tunaomba iwekwe taasisi maalumu inayo-deal na mifugo, na pia iwekwe taasisi maalumu inayo-deal na uvuvi, sawa na ambavyo tumeanzisha Wakala wa Umeme Vijijini, tumeanzisha wakala wa barabara na vitu vingine kama hivyo; tuanzishe wakala atakay-deal na mifugo na atakaye-deal na uvuvi, itatusaidia miradi ile ambayo tunaipeleka huko vijijini tuweze kuwa na monitoring. Ni aibu kupeleka mradi wa milioni 405 mna uweka porini baada ya hapo mmeaga na salama ndio mmeondoka na mradi ukishazinduliwa umekabidhiwa kwa wananchi umepotea. Kesho hata kama kuna tatizo linalotokea hakuna mtaalam kule. Kwa hiyo mradi mnauweka baada ya muda value for money haionekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unajenga mradi wa maji hata wa milioni 20, milioni 30 kuna watu wanaufanyia monitoring na ma engineer wapo. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba taasisi maalumu ya ku-deal na mifugo na uvuvi iundwe ndani ya Bunge hili iweze kusaidia fedha hizi zinazopelekwa huko. Ni mabilioni ya shilingi yanapelekwa lakini hayaonekani thamani yake kwa sababu hakuna anayefatilia. Mwaka mwingine unaofuata Waziri anakuja na kitu kipya, tukishapitisha unaofuata anakuja na kitu kingine, hivyo hivyo. Kwa hiyo fedha hii inaenda lakini hakuna anayeonekana kuisemea. Nilikuwa nataka niliweka hilo.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra kuna taarifa naomba…

TAARIFA

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwamba maeneo haya sio yapo mbali tuna mjini kama alivyotolea mfano wa Jimbo la Nachingwea ambako mimi ni Mbunge bali hata monitoring yake kama halmashauri hatuelewi chochote kwa sababu Mkandarasi anatoka moja kwa moja Wizarani na kama halmashauri hatuna namna ya kwenda kumsimamia na kukagua huo mradi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra, taarifa hiyo unaipokea.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, ni nyama tosha kabisa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niachane na huko; cha kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Alhamisi alitoa hotuba hapa yenye mwelekeo mzuri; lakini kama Wabunge wengine walivyosema. Wizara ya Mifugo nimesema ninyi ni vijana tunaomba mtusaidie. Kuna kipindi tunagombana na watu wa maliasili hapa ninyi mkiwa mmekaa kimya; we want you to speak out. Kwa sababu Waziri wa Maliasili amekuwa na wivu mkubwa hapa. Unamuuliza kati ya tembo na binadamu anayeuawa mwenye thamani ni nani anawaambia wanamfuata tembo, unaweza ukaona; lakini nyie wafugaji wetu wananyanyasika kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nina ushahidi hapa kwenye simu ninaweza nikatoa. Juzi Alhamisi Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama, hapa ameelezea reconciliation ambayo inabidi ifanyike na akasema hata haya mambo sasa ya watu kukaa karibu na hifadhi wanachukua wananyama na wakati mwingine wanawaingiza ndani wanasema wamekamatwa, Jumamosi mwenyekiti wangu wa halmashauri, na message ninazo hapa, huyu si mtu mdogo ndiye anayesimamia halmashauri yetu, na haina hati chafu. Kwenye kata yake akanitumia ujumbe wafugaji wawili, mmoja katozwa milioni tano mwingine katozwa milioni 11 hawajapelekwa sehemu, pesa imetolewa cash hakuna risiti hakuna; wafugaji wananyanyasika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku mbili baada ya Waziri Mkuu kuhutubia Bunge mambo yanafanyika kule sisi tukiwa hapa. Kwa hiyo tunaomba Wizara ya Mifugo mchukue hatua vinginevyo sasa utakuja kuanza ugomvi kule wale wahifadhi na wakulima na sisi sasa tutaingilia kati. Lakini tumechoka, hatuwezi kuja hapa kila siku wafugaji wetu wananyanyaswa kila ng’ombe shilingi laki moja Wizara iko hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tunaomba mtusaidie, wafugaji ni Watanzania. Ni lazima, kama mnasema Pato la Tanzania linaingia kwa asilimia 7.8 hawa watu hii nchi ni yao, lazima ifikie hatua na wao waone thamani ya kuwa hapa, wasinyanyaswe tuna watu. Kwa hiyo tunaomba hilo mlione mje na strategy nzuri ya kutusaidia ili wafugaji ambao wanafuga ng’ombe kule na wao wajione kama Watanzania. Nimelisema mara nyingi hili suala sasa inafikia stage tunachoka, tunaomba hilo mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru pia na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, nadhani tumeona wote video na hotuba jana kipindi anapita kwenye mabanda. Ameelekeza suala la utambuzi wa wanyama lianze upya, hususan suala la herein, ameelezea jana pale. Kwa hiyo kama Waziri Mkuu tumepokea lakini tunachoomba tunaomba Wizara tuwashauri. Wafugaji hawa mlikuja na habari ya chapa ng’ombe wakachapishwa ng’ombe wakaumia ngozi matokeo yake hatukuona kilichoendelea, na baada ya miaka mitatu mnahamisha mnapeleka kwenye heleni sasa mimi nilikuwa na ushauri…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra kuna taarifa kutoka kwa Nusrat Shaaban Hanje.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mngeniacha nichangie, muda umeisha.

TAARIFA

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kuhusiana na suala la identification ya mifugo, kwamba si suala la utashi wa viongozi kwa sababu ni sheria ambayo ilitungwa na Bunge hili, Sheria ya Usajili, ufatiliaji na utambuzi wa mifugo mwaka 2010, ambapo kifungu cha saba, cha nane mpaka cha tisa vina elezea devices. Kwa hiyo ni jambo la kisheria si jambo la utashi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa unaipokea?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea ila sasa naomba unilindie muda wangu maana na mimi hapa nahesabu. Taarifa nazipokea jamani tungevumiliana tumalize maana muda unaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoomba, cha kwanza tuna ranchi zetu za taifa, kwenye zile ranch kuna watu wanapewa nafasi ambao si wafugaji. Kwa hiyo tunachoomba, kwa kuanzia, mifugo yote ambayo iko kwenye ranch za taifa, achana na hawa wafugaji ambao wanafuga wao kama wao. Wewe umekodisha mtu anakwambia ana mifugo kwenye eneo lako; mifugo ni mingapi hatujui anamifugo mingapi. Kwa hiyo tunachoomba process ya kuweka heleni ianze na ng’ombe wote walioko kwenye Ranchi ya Taifa, tuwajue. Tukishaanza na ng’ombe walioko kwenye Ranchi ya Taifa hapa ndipo tutakapoujua ukweli kwa sababu kuna watu wameshikiria maeneo kwenye ranch na hawana ng’ombe pale wanatukodisha sisi; hilo ni la kwanza ambalo watakuwa wametusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kwa wafugaji wale ambao dawa ni yake, malisho ni yake kila kitu ni chake hamjawatengea chochote wanapouza ng’ombe si wanatozwa kwenye minada, hawa watu wananunua madawa tunapata, hebu tufumbeni macho basi wafugaji hao muwasaidie kwa kwenda kuvalisha heleni. First process mfanye nyie the second one itakapotokea itakuwa sasa kila ng’ombe anayezaliwa anazaliwa mfugaji anaruhusiwa kulipia heleni; hiyo itaweza kutusaidia. Lakini leo ukimwambia mtu mwenye ng’ombe 200, 300 hadi 400 akalipe hereni kwa mkupuo itawaumiza sana wafugaji. Kwa hiyo tuombe, walio kwenye ranch kwa sababu ni wakodishaji wenu cha kwanza mtakijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, Wizara walituahidi habari ya malisho. Kwamba kuna majani maalum wanataka kuja kuotesha nchi nzima na yale majani yatatusaidia hasa upande wa kiangazi kuzuia ng’ombe wasitoke sehemu moja kwenda sehemu nyingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra ahsante sana.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie muda wangu umeliwa sana dakika moja, nimalizie.

MWENYEKITI: Mheshimiwa sekundee moja.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, sekunde haitatosha. Sasa Mheshimiwa Waziri tunakuomba fanya identification ya maeneo na hasa uanzie kwangu kwa sababu kuna mifugo mingi ili tutengewe maeneo na yale majani yaoteshwe, wananchi wa Biharamulo waweze kupata majani wakati wa kiangazi wasihangaike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaunga mkono hoja.