Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza mchana huu. Kwanza kabisa niipongeze na kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wetu na Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri, wananchi hasa wa Jimbo langu la Mwanga wanafurahia kazi za maendeleo zinazoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu kwa dhamana kubwa hii waliyopewa, hotuba ya Mheshimiwa Waziri toka jana asubuhi ilileta hamasa kubwa sana na hatuna sababu kwa nini tusipitishe bajeti yake. Naunga mkono hoja kwa sababu nataka kuona hiyo hamasa aliyotupa ikiingia kwenye vitendo.

Mheshimiwa Spika, niliangalia kwa haraka tu jukumu la Wizara hii. Pamoja na mambo mengine, lakini kuna statement pale kwamba ni kusimamia na kuendeleza Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa ujumla, kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuyafikia malengo ya millennium. Katika upana huo ni kwamba Wizara hii inagusa maisha ya kila mtu ya kila siku. Naamini kabisa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania aidha wanakula nyama au samaki, mayai au maziwa na ikibidi sana basi hata wanatumia mbolea kulima mchicha na kula mazao ambayo yanatokana na mbolea za mifugo hii. Kwa hiyo ni sekta ambayo imegusa maisha ya kila siku ya watu. Kwa hiyo usimamizi wake ni jambo ambalo ni la muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Mwanga tuna ufugaji wa aina mbili ukizungumzia habari ya ng’ombe na mbuzi. Maeneo ya milimani wanafugia ndani zero grazing, tunazalisha zaidi maziwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri alipokuwa Naibu niliwahi kumvuta koti siku moja, nikamwambia kwamba kule kwetu tunahitaji sana masuala ya kukusanya maziwa pamoja na uhamilishaji. Sasa amekuwa full Waziri tunaomba atukumbuke hasa kwenye Miradi yake ya Heifer ili tuendelee kuzalisha maziwa kule milimani.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ya tambarare karibu kata kumi, zote zina ufugaji huu wa huria wa kuchunga. Ni jamii za Wamasai pamoja na makabila mengine, lakini kwa kweli tumesahaulika sana kwenye upande wa miundombinu ya ufugaji kama majosho, malambo na hata madawa ya mifugo. Kama sio Shirika la WWF kutukumbuka mara kwa mara nadhani wale wafugaji wangu Mwanga wangekuwa wameshakimbia. Kwa hiyo, tunaomba Wizara itukumbuke katika huduma hizo.

Mheshimiwa Spika, pia tuna mnada wa kimataifa pale wa mifugo kwenye Kata ya Mgagao. Katika mnada ule wanakuja watu kutoka Mombasa na Comoro kuja kuchukua mifugo pale, lakini miundombinu ya mnada ule bado sio rafiki. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iwekeze katika mnada ule wa Kimataifa wa Mgagao. Pia eneo hili la Mgagao linafaa sana kwa Kiwanda cha Kusindika Nyama, kwa sababu tuko katikati tunapokea mifugo kutoka Mwanga yenyewe, Simanjiro na hata kutoka maeneo ya Mkoa wa Tanga na airport ya KIA haiko mbali, Bandari ya Tanga iko karibu pia, pamoja na mpaka wa Kenya pale kwa ajili ya biashara. Kwa hiyo, ni eneo la kimkakati, tunaomba pia tukumbukwe.

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye Sekta ya Uvuvi, Jimbo la Mwanga lina rasilimali kubwa mbili za uvuvi. Kwanza ni Ziwa Jipe ambalo liko mpaka mwa Kenya. Ziwa hili kwa muda mrefu sana uvuvi sasa unakaribia kufa kwa sababu ya suala la magugu maji. Serikali karibu miaka 20 sasa imekuwa ikitoa ahadi ya kuondoa magugu maji pale. Mara ya mwisho mwaka 2021 alikuja Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira akatuahidi pale kwamba fedha zipo na kwamba magugu maji yataondolewa, lakini mpaka leo hakuna kitu na nimeendelea kufuatilia kila siku lakini inaonekana ahadi hii haitimii wakati ilitolewa mbele ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri ni upande wa mifugo lakini ukiangalia jukumu la Wizara yake ni pamoja na kusimamia hivi vyanzo. Kwa hiyo, tunaomba kauli ya Serikali kwamba wanaliachaachaje Ziwa lile la Jipe life wakati ambapo lina uvuvi mzuri wa samaki aina ya tilapia na liko mpakani mwa Kenya? Tunaomba Ziwa lile liangaliwe kwa umakini sana.

Mheshimiwa Spika, ukija chanzo kingine ni Bwawa la Nyumba ya Mungu. Bwawa hili asilimia 61 iko upande wa Mwanga na asilimia zinazobakia ni Simanjiro na Moshi Vijijini. Watu wa pale wanategemea uvuvi peke yake kama njia yao ya Maisha, kwa sababu lile eneo halina hata mvua ya kutosha, hivyo, hakuna kilimo pale. Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa uvuvi wa pale hauendi vizuri, samaki wale hawakui na kwa sababu samaki hawakui kila Mvuvi sasa anaonekana ni mvuvi haramu. Serikali imepambana sana na uvuvi haramu lakini bado mambo pale ni magumu.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna taarifa kwamba Wakuu wetu wa Wilaya hizi tatu wameandika barua Wizarani kuomba kufunga lile bwawa. Sasa kufunga bwawa tafsiri yake ni kwamba uvuvi haramu ndio pekee unaosababisha kutokukua kwa wale samaki. Sasa nilizungumza na mtaalam mmoja ambaye hata Wizara inamtambua kwa umahiri wake akaniambia wale samaki aina ya tilapia wameumbiwa namna ya kujilinda wasipotee.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, panapokuwa na tishio fulani hivi la kimazingira kama ni mabomu ya uvuvi haramu au ni maji kupungua au ni maji kuchafuka huwa wana mature ghafla ili wasipotee wanaishia hapo hapo walipo. Kwa hiyo, ndio maana wote wanakuwa wadogo. Nilipokwenda jimboni mara ya mwisho kwenye weekend hii ya Mei Mosi, watu wananinonesha wanasema Mheshimiwa angalia hawa samaki ni wadogo lakini wana mayai, tena wana watoto na wajukuu tayari lakini ndio wamefikia hapo. Ndio maana kila mvuvi pale anaonekana kuwa ni mvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, sasa nasema kwa vile hatujaona kama wenzetu wa Lake Tanganyika, hatujapata taarifa kwamba kwa nini Serikali inaona ni uvuvi haramu tu na sio sababu zingine za kimazingira zinazofanya wale samaki wengine wasikue? Basi kama ni hivyo ina maana huu ufungaji ni ufungaji wa majaribio (experimental closure). Sasa kama ni experimental closure, tunaomba basi wale wananchi wapatiwe mbadala.

Mheshimiwa Spika, tumesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna fedha nyingi kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Naomba wakati tunafikiria kufunga Bwawa la Nyumba ya Mungu, basi wale wananchi wapatiwe hii miradi ya ufugaji wa samaki. Halmashauri ya Mwanga imewekeza ikajenga Soko la Samaki lenye mpaka jengo la chakula barafu. Sasa hatuwezi kuacha ile facility ikakaa hivi hivi, tufuge samaki ili tuendelee kutumia.

Mheshimiwa Spika, lengo letu kujenga lile Soko la Samaki na jengo la chakula barafu ni kwamba samaki wauziwe mahali pamoja ili tuweze ku-control vizuri masuala ya afya, masuala ya ushuru wa Serikali na yule mtu atakayekuja sokoni na samaki wake wasiuzike aweze kuwaweka kwenye chakula barafu wawe fresh kesho asubuhi. Pia yule anayetaka kusafirisha basi tunamtengenezea wanakaa kwenye temperature inayofaa ili aweze kusafirisha. Kwa hiyo hatutarajii kabisa na wala hatutamani tuone kabisa lile bwawa linafungwa na wale watu wakose chakula, wakose ajira halafu na hii facility kubwa ambayo tumeweka isipate matumizi.

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya Bajeti hii twende akaangalie eneo lile la Lang’ata jinsi ambavyo halmashauri imewekeza kujenga hizi facility na jinsi ambavyo watu wote wanategemea maisha yao pale kwenye bwawa, halafu ndio atuambie kwamba tunalifunga kwa utaratibu gani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)