Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa ya kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa hotuba yao hii ambayo moja kwa moja imeenda kutafsiri maono pamoja na mawazo ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan namna ambavyo anataka Taifa letu liendelee kiuchumi, kimaendeleo na mambo mengine zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama samia Suluhu Hassan kwa kweli Mama anafanya kazi kubwa mno, anajitahidi sana kufanya kila means kutengeneza diplomasia ndani ya nchi ili kuhakikisha Taifa linasonga mbele kwa maendeleo zaidi. Pia kupitia Wizara hii nitakuwa nina dhambi kubwa nisipompongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hususan kwenye Wizara kama hii kwa kule Zanzibar tunaita Wizara ya Uchumi wa Bluu, kwa kweli Mheshimiwa Rais ameonesha wazi namna ya kutaka kuifumua Zanzibar kwenye uchumi, hususani ambao utaenda kwenye masuala ya uvuvi kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na nimtie moyo aendelee kuchapa kazi na Watanzania tunaona kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa iliyowasilishwa hapa takribani zaidi ya miaka Kenda tunaposimama hapa kwenye Bunge tunakuwa tunashauri, hususani Wabunge ambao tunatokea upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna ya kitoweo ambacho kinaitwa nyama. Nyama ya ng’ombe kwa upande wa Zanzibar ni very expensive ukilinganisha na huku Bara, ingawa nyama ya ng’ombe kwa asilimia 100 kwa upande wa Zanzibar tunategemea soko kubwa kutokea huku Bara, lakini kuna tozo lukuki ambazo bado Wizara haijataka kusema kwamba sasa kwa vile sisi ni nchi mbili, tunawaachia wenzetu kwenye suala la kodi hizi nyingine ndogondogo ambazo zinatuumiza kwa upande wa pili wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuamini sasa hivi bei ya nyama ukilinganisha Bara na Zanzibar ni tofauti sana. Upande wa Bara nyama inanunuliwa kwa kilo moja shilingi 6,000 hadi shilingi 7,000 lakini upande wa pili wa Zanzibar nyama kilo moja sasa hivi unanunua shilingi 13,000 na kuendelea, hii yote inasababishwa kwamba bado Wizara haijaamua kabisa kusamehe baadhi ya tozo.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nizitaje baadhi ta tozo ambazo zimekuwa kichefuchefu kwa uapande wa pili wa Zanzibar na inapekea bei ya nyama kuwa nzito kwa upande wa pili wa Zanzibar. Mfano mzuri bei ya nyama, ng’ombe anapotoka Bara kumpeleka Zanzibar kuna tozo ambazo zinachajiwa, ipo tozo ambayo Wizara ya Mifugo inatoza ng’ombe ambaye anaenda Zanzibar, ambayo hii tunaweza pia tukaisamehe kama Wizara ili Zanzibar aweze kununua kilo ya nyama kwa bei nafuu, hii nayo iangaliwe Mheshimiwa Waziri ikiwezekana ifutwe kabisa na isamehewe, sote ni nchi moja, sote tunafanya kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, ipo tozo ya Halmashauri nayo pia inachajiwa, yule ng’ombe ambaye anapelekwa Zanzibar lazima achajiwe tozo ile ambayo inatoka huku Bara, Halmashauri ya Tanzania Bara. Pia ipo tozo ya Kijiji ambayo inachajiwa kwa ng’ombe yuleyule ambaye anaenda Zanzibar. Pia ipo tozo ambayo inachajiwa na wenzetu wa TRA yule ng’ombe mmoja ambaye anaenda Zanzibar. Tozo ya TPA watu wa bandari nao pia wanamchaji ng’ombe yule anayeenda Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia ipo tozo ambayo inaitwa export levy ambayo hii hata mtu wa Kenya akija kununua ng’ombe Tanzania anampeleka Kenya hii anachajiwa ambayo inaitwa export levy, na Mzanzibar hivyo akinunua ng’ombe huku Bara kumpeleka Zanzibar na wao pia inachajiwa. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, ili kulinusuru soko la Zanzibar pia kuwanusuru Watanzania wa Zanzibar tuziangalie hizi tozo na ikiwezekana mkae Wizara zote mbili ili kuweza kuzifuta hizi tozo na bei ya nyama ikawa rafiki kama ya Zanzibar na bei ya Bara zote zikawa sawa. Tukifanya hivi tutakuwa tayari tumewapunguzia wenzetu kule wa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naliomba sana hili jambo kupitia Wizara yako Waziri Mheshimiwa Abdallah Ulega, naamini ni kijana una uwezo mkubwa wa kuweza kufanya lobbying ya kuzungumza na baadhi ya taasisi nyingine hizi ambazo zinashirikiana na wewe kwa ajili ya kufuta kabisa hizi tozo.

Mheshimiwa Spika, niende upande wa pili wa uvuvi. Imekuwa kila mwaka kipindi cha bajeti nalizungumzia suala la zao la mwani, mara hii kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri umelizungumza zaidi ya mara tatu suala la mwani, lakini kuna taarifa imewasilishwa na Kamati ya Viwanda Biashara na Mazingira ambayo inashughulika na suala hili pia imezungumzia zaidi ya mara nne. Suala la mwani bado hatujaona mpango mkakati, bado mmezungumzia suala la elimu, kutoa vifaa, sijui kuwezesha wakulima wa mwani, lakini ninachotaka kuwaambia mwani hasa changamoto yake ni soko siyo issue ya kuzalisha. Wakulima wetu bado hawajakatishwa tamaa, zao hili takribani zaidi ya miaka 20, 30 linalimwa na wakulima bado hawajakata tamaa, bado hali zao ni duni bado najua hawakopesheki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali bado hamjaandaa mpango mkakati wa kulisaidia hili zao la mwani. Leo wakulima wengi wa mwani wanalalamika suala la bei, bado Serikali haijawa wazi kabisa, haijawa na mpango wa kuwasaidia wakulima kuweza kupata soko rafiki na ikapatikana bei nzuri ya mwani ili mkulima aweze kufurahia zao lake la mwani. Mfano mzuri, Mheshimiwa Waziri tunalo zao la korosho, kuna parachichi, kuna mazao mbalimbali yote tumeona Serikali imeweka mpango mkakati na mazao haya yote yanauzika huko nje na wakulima wanafurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini zao la mwani bado hatujaona kabisa Serikali kulizungumzia hili, hasa kuwatafutia soko la mwani? Kwa hiyo, nawaombeni sana, Mheshimiwa Waziri unaufahamu mwani, unawafahamu wajasiliamali wa mwani sasa hivi wanavyopata shida, lakini suala la soko bado. Tuliangalieni, karibisheni wawekezaji wakubwa waje kuwekeza hapa nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naiomba sana Wizara kwa ushauri tengenezeni Bodi ambayo itakuwa inashughulika na masuala ya mwani tu kwenye suala la bei, kwenye suala la upandaji, kwenye suala la dawa na masuala mengine mbalimbali itasaidia sana na naamini kwa kipindi kifupi zao la mwani litapata value kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nakuona umeshabonyeza kengele yako, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)