Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora na Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba ni ukweli usiopingika hali za Halmashauri zetu nchini kwa ujumla wake ni mbaya sana. Halmashauri hizi zina hali mbaya kwa sababu nyingi zimekuwa tegemezi na kwa asilimia kubwa zinategemea fedha kutoka Serikali Kuu. Halmashauri zetu hizi pia vyanzo vile muhimu ambavyo vingewezesha mapato ya Halmashauri zetu kuongezeka, kwa kiwango kikubwa vimechukuliwa pia na Serikali Kuu. Kwa hiyo, tumeziacha Serikali zetu za Mitaa katika hali ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kuna uhaba mkubwa wa watumishi katika Serikali za Mitaa kwa maana ya rasilimali watu. Takwimu zinaonesha tuna uhaba wa watumishi 43,560 katika idara 470 za Halmashauri zetu nchini, huu ni upungufu mkubwa sana. Kama kuna upungufu huu mwisho wa siku hata ufanisi wa fedha zinazopelekwa unakuwa hauonekani au haupo kabisa au ufanisi unakuwa kwa kiwango kidogo sana.
Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikaangalia ni namna gani wanakwenda kupunguza uhaba wa watumishi walioko katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine unapoongelea suala la Serikali za Mitaa huwezi kuwaacha Madiwani pembeni. Ni kwa muda mrefu Serikali mmewatelekeza Madiwani si kwenye maslahi, si kwenye kujengewa uwezo, Madiwani maslahi yao yanaboreshwa kwa kiwango kidogo sana. Ukiangalia sisi Wabunge hatuna utofauti sana na Madiwani lakini tunawaacha Madiwani na sisi tukiwa Bungeni muda mrefu wanaotufanyia kazi kwa kiwango kikubwa na kutusaidia ni Madiwani. Ni muhimu sana Serikali ikaangalia namna gani maslahi ya Madiwani yanaboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si maslahi tu, wakati wa awamu iliyopita walifuta mafunzo (capacity building) kwa Madiwani. Hivi unampeleka Diwani akamsimamie Mkurugenzi na watendaji wake ambao wao ni wataalam wa mambo fulani fulani halafu Madiwani wetu wamechaguliwa tu kwa kigezo cha kusoma na kuandika, hana ujuzi wowote, baadhi lakini wako wengine ambao wana ujuzi lakini walio wengi hawana ujuzi huo, hivi kwa nini Serikali isiirudishe ile programu ya kuwajengea uwezo Madiwani kwa kuwapatia mafunzo. Mimi nilikuwa Diwani, nakumbuka kulikuwa kuna programu ya kuboresha Serikali za Mitaa, tulikuwa tunapelekwa mafunzo ya miezi sita lakini inakwenda kwa awamu, ilitusaidia kutujenga na kusimamia zile fedha zinazopelekwa. Kwa hiyo, ni muhimu pia mkalitazama hili muone namna gani Madiwani wanarudishiwa hizo programu za kujengewa uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuhusu TAMISEMI ni udhaifu mkubwa ulioko katika usimamiaji wa Bajeti na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Kuna udhaifu mkubwa sana, udhaifu huu unaendana na bajeti zilizoidhinishwa kutokufuatwa na hizi bajeti wakati mwingine hazifuatwi kwa sababu ya matamko ya viongozi mlioko ngazi za juu na mlioko katika Serikali Kuu. Mfano, Halmashauri 34 zimetumia kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Hakuna mtu anayepinga au anakataa umuhimu wa maabara, umuhimu wa maabara unajulikana lakini ujenzi huu na fedha hizi zimetokana na tamko lililotolewa na Rais bila kuangalia wakati huo anatoa tamko kwenye bajeti za Halmashauri za Wilaya fedha hizi zipo? Kwa hiyo, inaonesha kuna shilingi bilioni 33 zimetumika kinyume na bajeti eti kujenga maabara katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, kuna takriban upotevu wa shilingi bilioni nane kwa ajili ya malipo yaliyofanywa na Serikali za Mitaa bila kuwepo na nyaraka za malipo. Pia kuna Halmashauri 62 zimefanya malipo ya shilingi bilioni 1.4 kinyume na vifungu vilivyopitishwa katika bajeti. Sasa kama Serikali hizi za Mitaa hazifuati bajeti ambayo imejiwekea hakuna sababu ya kupitisha bajeti au kama kuna matamko yanayotolewa bila kuangalia uhalisia wa Serikali zetu za Mitaa hakuna sababu ya kuwa na Serikali za Mitaa kama hatutambui na kuthamini yale ambayo yanayopitishwa katika bajeti zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG anasema watekelezaji wa miradi 76 walifanya matumizi nje ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 4.6. Yote ni kukiuka bajeti waliyojiwekea, yote ni kukiuka Sheria ya Fedha ambayo ipo. Wanasema matumizi mengine yalifanywa nje ya bajeti na yameongezeka, CAG anasema matumizi nje ya bajeti yameongezeka kwa asilimia 224. Kwa hiyo, haya ni mambo ya kuyaangalia na kuyasimamia kuona yanaondoka katika Serikali zetu za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo lingine la elimu bure. Mmesema mnatoa elimu bure, lakini nilidhani mngepaswa kujiridhisha na kuangalia hivi ni kweli mnaweza kutoa elimu bure au mlikurupuka tu mkachukua Ilani yetu na yenyewe mkaweka kwenye Ilani yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, kuna watu wamefanya tafiti, wanasema ili uweze kutekeleza elimu bure unahitaji takriban shilingi bilioni 715 kwa mwaka mmoja wa fedha. Ili uweze kutekeleza elimu bure maana yake unahitaji mambo makuu manne; jambo la kwanza ni kutoa ile ruzuku ambayo ilikuwa inatolewa ya shilingi 10,000 kwa shule za msingi na shilingi 25,000 kwa shule za sekondari. Kama ile ruzuku mmeamua kuitoa kwa sababu mnasema ni elimu bure maana yake Serikali inahitaji karibia shilingi bilioni 130 kwa shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kama mnaondoa ada ya shilingi 20,000 kwa watoto wa sekondari, Serikali inahitaji kuwa na shilingi bilioni 31.5 ili kufidia ada hiyo. Hivi hizi fedha hizi mnazo? Si huwa mnasema kasungura kadogo? Safari hii kamenenepa? Nadhani mnapaswa kuangalia haya mliyoyasema ya elimu bure hivi mnakwenda kutekeleza? Halafu mmetoa Waraka mwingine Na. 5 wa elimu mnasema kama wanataka wapate kibali kwa Mkuu wa Mkoa, sasa kwa nini hizi contradiction, si mmesema elimu bure? Basi acheni bure mbebe huo mzigo, mtafute fedha hizi mwende kutekeleza elimu bure ambayo mnataka kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa haraka ni kuhusu Mfuko wa Vijana na Wanawake. Waheshimiwa Wabunge wengi tunachangia kwamba tuhakikishe Serikali za Mitaa zinatenga ile 10 percent kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake lakini lazima kidogo twende mbali ya hapa. Mifuko hii ukiangalia mwongozo wake na mwongozo huu ulipitishwa na Bunge hili mwaka 1991, ni mwongozo wa zamani ambao hauendani na uhalisia wa leo.
Katika Bunge la Kumi niliuliza Swali Na. 379 kuitaka Serikali i-review ule mwongozo wa kuanzisha Mifuko ya Vijana na Wanawake, ni mwongozo wa zamani sana kwa sababu unasema kikundi cha watu watano watapewa mkopo wa shilingi 500,000. Hivi unawapa mkopo wa shilingi 500,000 kwa watu watano, shilingi laki moja moja inasaidia nini, haisaidii kitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vizuri mkaangalia tena kwa upya namna gani ya kuu-review mfuko huu uendane na hali halisi iliyoko katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, kuna Mfuko wa TASAF. Mfuko wa TASAF ni mkopo kutoka World Bank ambao ni dola za Kimarekani milioni 200 lakini fedha hizi zinakwenda kupewa watu kwenye kaya, wanasema kaya maskini na kwenye kaya maskini wanaangalia vigezo mbalimbali kama kuna wategemezi na vitu kama hivyo na kwenye kila kaya range ya fedha hizi ni kati shilingi 20,000 mpaka shilingi 62,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuwakwamua watu wetu kutoka kwenye hali mbaya ya umaskini hivi ni kuwapa fedha mkononi? Kwa sababu ukimpa fedha mkononi itamsaidia nini? Kwa sababu hizo hizo Kaya maskini wakati mwingine hata mlo kwa siku ni taabu, ukimpa shilingi 20,000/= unamwendelezaje aondokane na huo umaskini? Kwa hiyo, ni muhimu mkaangalia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na mifuko mingi ambayo mwisho wa siku hatuoni manufaa yake.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.