Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, nadhani sasa tutulie tupate mambo mengine tofauti kabisa na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utazidi kusisitiza umuhimu wa ukujuaji wa uchumi wa Taifa hili. Baadaye mtaona nitasisitiza umuhimu wa Sekta ya Uvuvi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, nikianza na Jimbo langu la Musoma Vijijini, tuna kata 21, tuna vijiji 68, Kata 18 ziko pembezoni mwa Ziwa Victoria wanajishughulisha na uvuvi. Katika hizi kata, ni kata tatu. Kwa hiyo, hiki ni kithibitisho kwamba uvuvi lazima uchangie uchumi wetu kwa hali ya juu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uvuvi tunavyouchukulia sisi watu wa Musoma na nadhani ndiyo Taifa zima, kwanza unatoa chakula. Kwa hiyo, kwa mambo ya kiuchumi, uvuvi ni kwenye food security, uvuvi unatoa ajira na uvuvi unachangia uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa. Uchumi wa Tanzania kwa muda wa kama miaka mitatu, minne unakua kati ya asilimia tano na sita. Saa hizi nadhani upo kwenye 5.6.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwenye hili Bunge la Bajeti kuna maeneo ambayo ninawasihi tutoe ushauri kwa Serikali kusudi uchumi wetu kama tunataka uondoe umasikini kama nilivyowaeleza juzi, uchumi ni lazima ukue kuanzia asilimia nane kwenda asilimia 10. Ni sekta tano tu ndizo zinaweza kufanya uchumi uende kwa haraka (accelerated growth). Cha kwanza kabisa ni gesi asilia. Tutalijadili huko. Cha pili ni madini, cha tatu ni kilimo, inakuja mifugo na uvuvi na cha tano ni utalii. Hizi sekta tano, kila moja ningechangia asilimia mbili ya ukuaji wa uchumi, tungeweza kufika hizo nane mpaka kumi.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa nini nasema uchumi. Wataalamu wa lishe wanasema kwamba, kama unataka balanced diet (chakula bora) unapaswa kutumia grams 280 mara mbili kwa wiki. Yaani portion ya kwanza gramu 140, na siku nyingine gramu 140, 280. Sasa tunavyosema uvuvi ni uchumi muhimu, tuangalie soko letu kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, soko letu la kwanza, kama wananchi wote duniani wanataka kula namna hiyo, wako watu bilioni nane sasa hivi. Tanzania ikiuza huko Samaki, tutapata fedha nyingi. Kama soko letu ni ndani ya Bara la Afrika, sasa hivi Barani Afrika tuko watu bilioni 1.43. Kwa hiyo, hizo ni fedha nyingi sana ukipiga kwa grams 280. Kwa hiyo, Sekta ya Uvuvi tuichukulie kibiashara.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2022 samaki waliozalishwa duniani walikuwa ni tani milioni 184.6. Mzalishaji wa kwanza hapo alikuwa ni China aliyezalisha tani milioni 67.5, na katika hizo tani milioni 54.6 alizalisha kutumia vizimba, na huko baadaye ndiyo nitakuja kusisitiza suala la vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wa pili alikuwa ni India ambaye uzalishaji wake duniani ni asilimia 7.56. Sasa maoteo ya mwaka huu ya biashara ya samaki duniani, mapato yake yatafika bilioni 612. Hapo ndipo tunapaswa kushawishi na kuishauri Serikali iwekeze zaidi kwenye uvuvi. Samaki wa vizimba duniani wanaozalishwa ni tani milioni 180. Mzalishaji namba moja ni China, anazalisha theluthi moja; wa pili, ni India ambaye anachuana na Misri (Egypt). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Afrika Egypt ndiyo inaongoza, sasa Egypt yenyewe kwa mfano mwaka juzi ilizalisha samaki tani milioni 2.2 kati ya hizo, tani milioni 1.7 walizalishwa kupitia vizimba hii ni zaidi ya 77%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja yangu hapa na mchango wangu kwenye hii Wizara nitabaki kwenye uvuvi na ninazidi kusisitiza umuhimu wa samaki wengi wamesema samaki wamekosekana Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria. Suluhisho lake ni samaki uvuvi wa vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuiangalie Tanzania ilivyo na ndugu zangu wa Lake Tanganyika walikuwa wanalalamika, wana haki ya kulalamika. Utafiti ambao nina muomba Mheshimiwa Ulega na maprofesa wake wafanye siyo ule alioripoti jana kwamba walifanya utafiti wakafikia conclusion kwamba lazima zana zipatikane. Nadhani hiyo unaweza ukafikia hiyo hata bila utafiti.

Mheshimiwa Spika, utafiti unaohitajika Mheshimiwa Ulega ni kijana mzuri, msomi mzuri wa Bio-aquatic sciences. Tunachukua Lake Tanganyika, Lake Tanganyika umri wake ni miaka milioni 10, maji ya Ziwa Tanganyika yaliyomo Ziwa Tanganyika ujazo wake ni cubic meter 18,880. Aina ya samaki waliopo ni zaidi ya 350. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Wizara yetu tunataka wafanye utafiti hapa, Ziwa Tanganyika; nikiwa Kigoma nimekaa Kipiri, nimekaa sehemu nyingi huko nafanya utafiti lakini mbona samaki ni aina mbili tatu? Hizi 330 wengine wanaenda kwenye extinction wanapotea sisi bila kuwajua. Tunaenda Ziwa Nyasa, Ziwa Nyasa lina umri wa miaka milioni mbili. Ujazo wa maji kwenye Ziwa Nyasa ni cubic kilometer 8,400, Ziwa Nyasa hilo na lenyewe ndiyo lina samaki wa aina nyingi kuliko aina yoyote hapa duniani. Ni kati ya 800 na 1,000 species of fish. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ripoti zetu hizi species zote 1,000 za Ziwa Nyasa ziko wapi? Tunakuja Ziwa Victoria lenyewe ndilo changa kuzidi yote. Umri wake ni miaka 400,000 lakini ujazo wake wa maji ni cubic kilometer 2,424. Aina ya samaki waliomo Ziwa Victoria ni zaidi ya 500. Kwa hiyo, pendekezo langu la kwanza kwa Wizara yetu hii kwenye haya maziwa makuu matatu yana maji ya kutosha. Yana aina nyingi sana za samaki kama Ziwa Victoria 500. Je, hawa samaki wote wako wapi? Wanavuliwa na nani? Hao wengine.

SPIKA: Mheshimiwa Muhongo kengele ya pili imeshagonga, dakika mbili malizia.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, dakika mbili afadhali. Sasa kwa kumalizia niseme hivi; Ziwa Victoria nimechukua ukubwa wake, Kenya wana 6% ya Ziwa Victoria, Uganda wana 45% na Tanzania tuna 49%. Kenya yenye 6% ina viwanda 18 vya samaki. Uganda yenye 45% wana viwanda 11. Tanzania ambao tuna 49% na ripoti hapa Mheshimiwa Ulega Musoma hatuna kiwanda hata kimoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo pendekezo langu la mwisho ni kwamba tuwekeze kwenye uvuvi wa vizimba. Tutoe kama hii mikopo iliyokuja nashukuru Mheshimiwa Waziri ameniambia wiki ijayo watu watapewa ile mikopo yao tuvue kwa vizimba lakini vilevile kwa sababu samaki wa vizimba ni wengi tutoe mikopo kwa Watanzania waanzishe viwanda vya samaki kwa sababu samaki wa vizimba watakuwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)