Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi nzuri inayofanyika katika hii Wizara na kwa hotuba nzuri ya bajeti.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi kwa kuwaongezea bajeti, kuwawezesha vijana na uboreshaji wa huduma za ugani.
Mheshimiwa Spika, mifugo; katika Mkoa wa Kagera shughuli kuu za uzalishaji ni kilimo, ufugaji na uvuvi. Ng’ombe wengi zaidi wanafugwa na watu binafsi. Kwa kuwa asilimia 90 ya eneo la malisho tayari limetumika, hivyo napendekeza yafuatayo: -
Kwanza, wafugaji/wawekezaji waliopewa vitalu, watenge maeneo, walime majani malisho; pili, wapewe elimu ya namna ya kulima majani/malisho; wawezeshwe kupata mbegu bora na NARCO iwezeshwe kuwa na matrekta na mitambo ya kulimia mashamba, wapewe mitambo ya kuvuna na kufunga majani ya malisho, ili sasa NARCO iwe inawakodisha wawekezaji mitambo, walime na kuuza majani ya malisho kwa wafugaji wengine hasa katika kipindi cha ukame/kiangazi.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera una Ranchi za Serikali tano, ya sita ambayo ni Mwisa II bado mchakato wake haujakamilika. Mwisa II ina ukubwa wa hekta 66,215.76. Vitalu tayari vilikwishakatwa, lakini wawekezaji hawajamilikishwa. Eneo hili likianza kufanya kazi litawezesha uwepo wa kiwanda cha nyama na kiwanda cha maziwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha mchakato wa Mwisa II?
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na migogoro mingi kati ya wananchi na wawekezaji waliopewa vitalu vya NARCO, kwa sasa migogoro mingi ilikwisha na imebaki katika eneo moja la Ranchi ya Kagoma; kati ya wakulima na wafugaji hakuna amani, wameanza na kuuana. Serikali ina mpango gani wa kuwagawia wananchi/wakulima maeneo na wawekezaji wakapatiwa ili kurejesha amani katika eneo hili?
Mheshimiwa Spika, kuhusu uvuvi; mkoa una fursa nyingi za uvuvi na soko la samaki ni kubwa humu nchini na Congo, Zambia, Malawi na South Sudan. Pia kuna fursa za uwekezaji katika viwanda vya uchakataji samaki, viwanda vya chakula cha samaki, cold rooms na mitambo ya kukausha dagaa.
Mheshimiwa Spika, vilevile mkoa una maziwa madogo madogo yanayoweza kutumika, wakapandikizwa vifaranga vya sato au kambale na kuwakuza, kuwavuna na kuwauza katika soko kubwa la samaki lililopo nchini na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, tunampongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi wa ufugaji wa vizimba katika Ziwa Victoria. Kuna maeneo mengi yanayofaa kwa ufugaji wa vizimba ambayo ni Kashenye - Missenyi, Rubafu - Bukoba Vijijini, Bumble, Ikondo, Kabasharo Kimwani, Kabunyora ya Runazi na Ikuza yakiwa katika Wilaya ya Muleba.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuwezesha maeneo hayo kupimwa na kupatiwa vibali vyote vinavyotakiwa (Ardhi, NEMC, TAFIRI). Gharama zake ni kubwa, zingewashinda wananchi/vijana/wawekezaji wengi, lakini Serikali imezibeba.
Mheshimiwa Spika, napendekeza ugawaji wa maeneo ya kuweka vizimba uzingatie pia kuwapatia maeneo ya kufugia vijana wetu wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maeneo ya Rubafu (Bukoba Vijijini) tayari mwekezaji amepatikana. Je, ni lini mchakato utakamilishwa, watu wakapewa maeneo na wakaanza kufuga samaki kwenye vizimba ili kuinua kipato cha hao wananchi na Taifa?
Mheshimiwa Spika, mwisho naunga mkono hoja.