Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipatia fursa hii kuchangia Bungeni kwako Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia nianze kwa shukrani. Moja nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ametukabidhi kwa sasa. Vilevile nimshukuru sana Makamu wa Rais kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Mionongozo ambayo amekuwa akitupatia muda wote kuhakikisha kazi za Serikali zinakwenda kama ambavyo Mheshimiwa Rais anakusudia na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu nikushukuru wewe binafsi umekuwa ukituongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu. Umekuwa ni Spika wa mfano na tumekuwa tukijivunia wewe kwa kazi njema ambayo unaifanya katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho na kwa umuhimu wa kipekee nimshukuru Waziri Ulega ni mtu rahimu, mtu mwema, Waziri anayesikiliza. Nimefanya naye kazi kama wakati akiwa Naibu Waziri na katika kipindi kifupi nimefanya naye kama Waziri. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kama tuna Waziri ambaye anaweza kusikiliza, nikishirikiana na Mheshimiwa Ulega tunaamini Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi tutaibadilisha kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhamira yetu kupitia Wizara hii ni kuhakikisha tunamsaidia Mheshimiwa Rais, moja katika kuongeza wigo wa ajira nchini kupita Sekta ya Mifugo pamoja na Uvuvi. Hayo ndiyo moja ya lengo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaongezaje ajira kupitia Sekta ya Mifugo na Uvuvi? Mmeona katika Hotuba yetu tumeandika hapa na tumeanza utekelezaji katika Mwaka wa Fedha ambao huu tunaimalizia 2022/2023. Tumekuja na program za vituo atamizi vyenye lengo la kutoa ajira kwa vijana kwa kuwapa mafunzo ya ufugaji kwa vitendo na program hizo mmekuwa mkiona tukizizindua, mmekuwa mkiona viongozi wakubwa wakienda tukiwaonyesha dira ya wapi tunataka Sekta ya Mifugo ielekee.

Mheshimiwa Spika, katika awamu iliyopita tulianza na vituo vichache na katika Bunge lako Tukufu Wabunge wengi wakati wanajadili wamekuwa wakisema kwamba vituo ni vichache wanataka ongezeko la vituo ili mafunzo kwa vitendo kwenye Sekta ya Mifugo yaweze kuongezeka. Jambo hilo tumelipokea na Wizara ya Mifugo na Uvuvi sasa hivi tuko katika mazungumzo na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba tunakuwa na vituo atamizi kila Mkoa ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu tunawaongezea wigo lakini vilevile watu wapate maeneo ya karibu ya kwenda kujifunza na kupata elimu ya vitendo ya ufugaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ndiyo moja ya malengo yetu ambayo tunakwenda kuyatekeleza katika mwaka wa fedha unaokuja. Jambo jingine tutaongezaje wigo wa ajira? Ni kwa kuendelea kutoa mikopo ya masharti nafuu ambayo inatokana na mikopo ya Extended Credit Facility kwa maana ya ECF ambayo tunaipata kutoka IMF na mikopo hiyo tumeielekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya ununuzi wa boti ambazo tutakwenda kuzitoa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu tumeonyesha hapa na tumeyaelezea hapa tutatoa boti 158 ambazo zipo katika hatua ya mwisho ya ujenzi wake. Kwa hiyo, kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu Wizara ya Mifugo na Uvuvi itafanya zoezi hilo na litatangazwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunatoa boti hizo kwenye maeneo ya wavuvi? Moja ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliagiza zinunuliwe boti hizo kwa lengo la kuongeza ajira kwa wavuvi lakini vilevile kuongeza uzalishaji wa mazao ya samaki na viumbe maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ni sehemu ya malengo ambayo sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Waziri wangu Comrade Ulega tumedhamiria kwenda kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili tumesikia maoni mengi na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge wakati wanajadili hapa wakizungumzia mchango mdogo wa Sekta ya Uvuvi vilevile Sekta ya Mifugo katika uchumi katika Pato letu la Taifa. Moja ya nia yetu thabiti kabisa ni kutaka kuona mifugo ikichangia pato zaidi ya ambavyo inachangia sasa, vivyo hivyo katika Sekta ya Mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika moja ya malengo ambayo tumejiwekea ni pamoja na lengo hili na ndiyo maana hata mchango wa mwisho wa Mheshimiwa Professor Muhongo wakati anaelezea hapa anasema sasa hivi tuje na mpango wa vizimba. Ninyi wote ni mashuhuda mpango huo sasa umeanza kutekelezwa katika baadhi ya maziwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini tunaleta huo mpango? Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki lakini vile vile utasaidia maziwa yetu yaani kwa maana ya hizi water bodies ambazo zipo zitakuwa na fursa ya kupumua wakati ule ambapo yatakuwa yamefungwa. Kwa hiyo, hayo ndiyo malengo ambayo sisi tumekuwa tukijiwekea na tunaamini kwamba tutayatekeleza.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu Mheshimiwa Waziri wakati tunajadiliana amenielekeza niwaeleze Bunge lako Tukufu kwamba sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi; moja hatutachukulia ufugaji ama uvuvi kama kero kwa Taifa letu. Kwa hiyo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi haitakuwa treated kama Wizara ya Migogoro na ndiyo maana tunaruhusu Wabunge kuleta maoni wakati wowote siyo wakati wa Bunge peke yake ama wakati wa bajeti. Tunaruhusu maoni, tunaruhusu ushauri ili kuhakikisha kwamba tunajikwamua katika mawazo yale ambayo yalikuwepo hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ni sehemu ya malengo makubwa ambayo sisi tumejiwekea kuhakikisha kwamba baada ya mwaka mmoja tunaamini kuna jambo tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kuisaidia Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne tumekubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba moja ya jambo kubwa tutakalolitilia mkazo katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi ni pamoja na kufanya tafiti nyingi zaidi za kitaalamu na ambazo zinatekelezeka ili tuweze kubadilisha mtazamo mkubwa ambao ulikuwepo hapo nyuma kwenye Wizara hizi mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tuanaamini kwamba mifugo pamoja na uvuvi ni utajiri kinachohitajika ni nia thabiti ya kutekeleza na kubadilisha hii Wizara kutoka katika mitazamo ambayo ilikuwepo hapo awali. Sisi tunaamini hivyo na linawezekana. Hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi siyo Wizara ndogo kama watu wanavyokuwa wakiifikiria. Ni Wizara kubwa ina malengo makubwa na tuna uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwa Bunge lako tukufu kwamba tunawaomba mkubali kutupitishia Bajeti yetu siku hii ya leo halafu baada ya mwaka mmoja mje muone matokeo ya kazi nzuri ambayo sisi tunaamini tutaifanya kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ni sehemu tu ya mambo ambayo sisi tumekusudia kuyatekeleza katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema maneno hayo machache, nikushukuru sana ninaunga mkono hii hoja ipite kwa 100% ili tukafanye kazi kwa sababu kazi tumeaminiwa kuifanya na tunaiweza na tunaamini kabisa kwa ushirikiano wa Bunge lako Tukufu jambo hili liko ndani ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mwenyezi Mungu akubariki. (Makofi)