Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nichangie kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Nataka nitumie fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayofanya kwenye Wizara hii, tuna imani naye tunachomuomba aendelee kuweka umakini katika kusimamia sekta zilizoko chini ya Wizara hii. Nataka nimpongeze sana ndugu yangu Mnzava ambaye ameeleza vizuri jambo hili kwa maslahi ya watu wa Mkoa wa Tanga na uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa spika sisi watu wa Tanga ni wahanga wa uwekezaji, siye tumegongwa na nyoka kwa hiyo, tukiona unyasi lazima tushtuke. Mwaka 2017 alijitokeza muwekezaji akiitwa Hengia akionesha nia ya kuwekeza kenye sekta ya saruji katika nchi hii na kiwanda kile alikuwa aje akijenge Mkinga. Mwaka 2019 TIC ilimpa leseni aje awekeze, mwaka 2020 akaanza kutoa fidia kwa ardhi aliyoitwaa kule Mkinga wananchi wakaachia maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, tangu wakati huo fidia stahiki haijatolewa, hivi ninavyozungumza wako wananchi 143 wa Mkinga kutoka Kwale na Mtimbwani wanadai Zaidi ya milioni mia tano na sabini na kitu hivi hazijalipwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilituma timu ikaja kukaa na uaongozi wa Mkoa na uongozi wa Wilaya na mwekezaji, wakakubaliana ifanyike kazi ya tathmini isiyo na shaka ili watu hawa walipwe, kazi imekamilika. Mwekezaji huyu wamepelekewa amegoma kulipa viwango stahiki vya kisheria.
Mheshimiwa Spika, hawa ni wananchi wamepoteza ardhi zao, hawana ruhsa ya kuingia kwenye maeneo yale mpaka leo hawalipwi. Kwa nini mwekezaji halipi? Ni kwa sababu ana machungu nilisema hapa kwamba jamani uwekezaji huu wa Hengia ambao wakati ule kama ungefanyika mwekezaji alikuwa anakuja kujenga kiwanda chenye thamani ya trilioni 2.3 uzalishaji wa saruji alikuwa anaenda kuzalisha tani 7,000,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, nimesikia taarifa ya Wizara hapa inazungumzia kwamba leo viwanda 14 tunazalisha tani 10,000,000 tulikuwa na mwekezaji ambaye alikuwa tayari kuja kuwekeza mtaji wa trilioni 2 azalishe tani 7,000,000,000 tuka–frustrate, nilikuja kusema maneno haya hapa nikasema wapo watendaji wetu hawana nia njema wanam–frustrate mwekezaji, wapo watu ndani ya industry ya saruji hawataki mwekezaji huyo awepo kwa sababu ataleta ushindani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunapozungumza tumepoteza uwekezaji ule, watu wa Tanga tuna machungu, tumegongwa na nyoka tukiona unyasi tunashtuka. Naiomba Serikali tathmini hii ilifanywa na timu ya Serikali Mheshimiwa Waziri nakuomba simamia ndugu zetu wale wa Mkinga 143 walipwe stahiki zao.
Mheshimiwa Spika, Sasa kwa muktadha huo huo, linapokuja suala la uuzaji wa hisa za Tanga Cement sisi hatuna hatupingi, lakini tunasema taratibu zifuatwe, watu wa Tanga leo hii pale Tanga tuna viwanda nane, baada ya kubinafsishwa vimegeuka kuwa magodauni vimegeuka kuwa magofu havifanyi kazi. Hatutakuwa tayari kuona Tanga Cement inabinafsishwa inageuka kuwa godauni mtu anakuja kuchukua raw materials Tanga anakwenda kuzalisha Dar es Salaam hilo hatutaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Viwanda vile nane tumehangaika ndani ya Serikali ili wawekezaji wale waheshimu mikataba yao wakati wanauziwa viwanda vile Serikali mmeshindwa kulisukuma hili, hii ndio hofu yetu, watu wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali taratibu zifuatwe uwekezaji ufanyike tujenge confidence ya wawekezaji tunapata shida kwenye sekta ya madini kila mwekezaji anayetaka kuja akija anang’ang’aniza kwamba kukiwa na disputy twende tukaamuliwe mashauri hayo nje ya Tanzania, kwa nini? Kwa sababu wanasema mahakama zetu haziaminiki. Kama kuna jambo lililoamuliwa kisheria tusikiuke maamuzi yale yaliyoamuliwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, kila muwekezaji kwenye sekta kule akija anaenda kujificha kwenye maeneo ambayo tuna mikataba ya kimataifa kwa hiyo anaenda kujisajili kampuni kwenye maeneo hayo ili mashauri yake yasiamuliwe Tanzania yaende kule. Tukiendelea kukiuka maamuzi ya vyombo vyetu vya kisheria tunaenda kupeleka ujumbe kwamba tusitumie mahakama zetu za ndani mashauri yote yakaamuliwe nje, hii haiwezi kuwa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru ahsante sana.