Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Nipende kwanza kumshukuru Mheshimiwa Waziri, najua, nimefanya naye kazi katika Wizara hii ya Viwanda, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati yake. Ni Waziri mahiri sana, anajiweza katika vitu vingi. Namshukuru kwa kufanya kazi vizuri na Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mapambano yake haya ambayo anaendanayo katika viwanda. Nilikuwa naona katika shughuli hizi alizokuwa anazungumzia Mheshimiwa Mgaya hapa, juu ya Liganga na Mchuchuma. Sasa kutokana na hayo mimi nikaona nije na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nianzenayo kabisa, Ukurasa wa 58; inasema, kuendeleza na kujenga viwanda mama ikiwemo viwanda vya chuma, Miradi ya Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, wazo limekuwepo tangu uhuru, ilani imeandikwa zaidi ya miaka 40. Sasa mimi nataka kujiuliza, Liganga na Mchuchuma sasa ni wimbo au ni mradi? Maana sasa tujue, Liganga na Mchuchuma ni wimbo au ni mradi? Maana tumesema Liganga na Mchuchuma hadi tumezeeka na tunaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Liganga na Mchuchuma tunaenda kufa, Liganga na Mchuchuma tunaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe hakuna jambo lisilowezekana duniani. Hakuna jambo…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Katani.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naye ameanza mapema huyu. (Kicheko)

SPIKA: Aah, ngoja, samahani, sijamsikia. Umesemaje Mheshimiwa Getere?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ameanza mapema. (Kicheko)

SPIKA: Nadhani katika watoa taarifa humu ndani unaongoza kwa hiyo, uvumilie tu. (Makofi)

Mheshimiwa Katani Katani.

TAARIFA

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe taarifa Mheshimiwa Getere kwa alichokisema. Tangu mimi nakuwa Mbunge mwaka 2015 mpaka leo, habari ya Liganga na Mchuchuma imekuwa ni maandishi ya kwenye makaratasi. Kwa hiyo, naunga mkono hoja yake tuone jambo hili linakaaje.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakuunga mkono kamanda. Na ninapokea Taarifa yako…

SPIKA: Mheshimiwa Getere unasubiri uitwe kwanza.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa yake kwa sababu, ana uchungu na huo mradi. (Kicheko)

SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Getere, usiwe na haraka sana.

Mheshimiwa Getere, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Katani?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, nataka kuzungumza kwamba hakuna jambo ambalo haliwezekani duniani. Tumekuwa na wazo la kuja Dodoma toka mwaka 1972, lakini limewezekana. Nami nilikuwa kwenye Kamati, naona juhudi za mama katika huu mradi inawezekana. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Rais kwamba hii jitihada aliyonayo ya Liganga na Mchuchuma iwezekane kwenye hii miaka inayokuja. Kwa hiyo ikifika 2030 wakati Rais anaanza labda anataka kuacha au kama anataka kuendelea, basi mradi utakuwa umekamilika. Nimwombe sana kwa jitihada yake hii, ili Liganga na Mchuchuma sasa zisifutike kwenye mawazo ya Watanzania, uwe mradi ambao unatuletea faida.

Mheshimiwa Spika, nizungumze habari ya viwanda vilivyotaifishwa na viwanda vilivyobinafsishwa. Wamezungumza wengi hapa. Hii nataka nitoe mfano na Wabunge wengine msikilize humu ndani, maana yake kuna watu wengine wakizungumza kwenye mikoa mingine tunakuwa tunagunaguna, mikoa mingine mna-support.

Mheshimiwa Spika, wamezungumza jana hapa Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Rukwa habari ya Ziwa Tanganyika, Wabunge tumewa-support na Serikali imewasikia, imekwenda kuwasikiliza. Tulizungumza sisi wafugaji ambao tulikuwa watu wanaofuga ng’ombe kuhusu mambo ya hereni, tumezungumza sana, Serikali ikasikia ikasimamisha mradi. Hivyo, wanapozungumza watu wa Tanga kuhusu eneo la Kiwanda cha Tanga Cement tuwasikilize. Kwa nini tusiwasikilize? Kwa sababu mikoa yote tumewasikiliza. Tuwasikiliza tujue nia yao ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama haya maneno yaliyokuwa yanaendelea hapa, kilichokuwa kinazungumzwa. Ukiangalia kwenye mitandao yote hili jambo limeandikwa, ukiangalia kila mahali hili jambo limeandikwa na ukilitazama vizuri liko kisheria. Kuna mahakama, kuna taasisi zetu, Tume ya Biashara na kuna Tume ya Mahakama, wamezungumza vizuri, wametoa maamuzi yao yanafuatwa. Kwa nini Serikali haitaki kuchunguza haya maamuzi?

Mheshimiwa Spika, kingine, amezungumza Mheshimiwa Shabiby hapa, inawezekana kabisa na siyo kuwezekana, ndivyo ilivyo, Kiwanda cha Tanga ndicho kina deposits nyingi miaka milioni karibu 30 na Kiwanda cha Twiga kina mitambo mizuri sana hapa Tanzania. Sasa hapo upime uone; je, kitu gani kitahama, kama Twiga Cement itachukua kile kiwanda itachukua clinker na malighafi kutoka Tanga kuja Dar es Salaam au itapeleka mitambo mizuri ya Dar es Salaam kwenda Tanga? Waliangalie hili sana, waliangalie.

Mheshimiwa Spika, walipozungumza Wabunge wa Tanga maana yake tuna imani kwamba inawezekana wakaweka maboksi pale kikawa ni godown pale. Clinkers zote zikaja Dar es Salaam, cement ikazalishwa biashara ikaendelea, lakini itakuwaje kwa wafanyakazi?

Mheshimiwa Spika, katika viwanda, tuna aina mbili ya viwanda; kuna labour intensive na capital intensive. Kiwanda cha Tanga ni capital intensive, kiwanda chenye mtaji wa kati ambapo wafanyakazi wengi ni Watanzania, ndiyo wanaweza kutengeneza thamani ya mnyororo. Sasa leo tunaona kuuza ni sahihi, cement inaweza kutengenezwa hata katika maeneo yote ya Tanzania, lakini kwa sababu tumetawanya kwenye mikoa mbalimbali kila mkoa tunataka upate faida yake.

Mheshimiwa Spika, lazima Serikali iangalie watu wa Tanga, wananung’unika nini. naomba hili jambo Mheshimiwa Waziri asilichukulie kama kawaida. Maana yake nasikia mtu anasema ni kiwanda cha mtu binafsi, anauza, anafanyaje, hapana, viwanda vyote vilivyobinafsishwa vya Serikali ni lazima tukae na kuviangalia vinafanyaje kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba, Mheshimiwa Waziri namwamini sana, utawasikiliza Watanzania wanaonung’unika na utafanya maamuzi ili kiwanda kile kifanye kazi. Ni kweli mtu anayemiliki kile kiwanda hana uwezo, lakini ni kweli kama kuna wazawa wanataka kumiliki kile kiwanda tuwaruhusu wamiliki hicho kiwanda kama wana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa hiyo naomba tuendelee kuangalia hili jambo linafanyikaje.

Mheshimiwa Spika, wakati niko kwenye Kamati ya Viwanda, mara nyingi sana wamesema tunajenga industrial park Bunda. Wilaya ya Bunda na Mkoa wa Mara kwa ujumla viwanda vya samaki vimekufa, viwanda vya pamba vimekufa, viwanda vya maziwa vimekufa, yaani ule mkoa sasa umebaki ni hewa tu. Tunaomba sasa Serikali iangalie Mkoa wa Mara kwa maana ya viwanda vya samaki, maziwa na pamba. Vinginevyo ule mkoa umebaki hewa, hakuna namna. Kwa hiyo naomba Waziri ufikirie jambo hili la kutufufulia viwanda ili watu wapate fedha katika Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante sana.