Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kusimama hapa. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Leo nitakuwa na mada mbili tu kuhusu Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na nitaongelea masuala ya ajira pamoja na utawala bora.
Tatizo kubwa la watumishi wetu ni maslahi yao na siyo maslahi yao tu lakini pia ni kujengewa uwezo wa kazi zao. Wafanyakazi wanalipwa mshahara ambao haulingani na maisha ya sasa. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri alisema mwaka 2010 uliongezwa mshahara kwa asilimia 13.2 tatizo siyo kuongeza tu mshahara, je, mshahara unakidhi mahitaji ya lazima ya mfanyakazi, hilo ndilo swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mshahara wanaolipwa, kiwango cha chini ni kuanzia shilingi 300,000 au 400,000 kwa wafanyakazi mbalimbali haufiki hata wiki moja. Wafanyakazi ambao wanautumia muda wao kuanzia saa moja mpaka saa tisa na anafika nyumbani saa kumi na moja afanye nini, hizi wiki tatu atafute wapi fedha za kuweza kuendesha maisha ya lazima, mfanyakazi huyo atatafuta njia ya kuweza kujisaidia. Nasema kwamba mtatumbua majipu mpaka mtatumbuana wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia watumishi ambao wanaondoka nchini na kwenda nchi za nje, Mheshimiwa Waziri hakuligusia suala hili katika hotuba yake. Tuna wataalam ambao tunawasomesha kwa fedha za umma ambao wanahitajika katika nchi, lakini baada ya kufundishwa na kupewa utaalam wa kutosha wanaondoka kwenda kujenga Taifa lingine. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri uangalie upya suala hili ili uhakikishe watumishi hawa ambao ni wataalam wanajengewa vivutio ili kuwawezesha kuishi na kufanya kazi katika Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upungufu wa wafanyakazi. Kuna malalamiko kwamba zaidi ya wafanyakazi 16,443 na wale wa wakala 2,552 bado wanahitajika. Huwezi kutoa service kama hakuna wafanyakazi. Uchumi unajengwa kwa watu kufanya kazi. Leo nguvu kazi, rasilimali watu zaidi ya 16,000 ukiongeza na 2,500 almost 18,000 na zaidi wanahitajika, leo Waziri anasema anakwenda kufanya mchakato. Hapa hakuna haja ya kufanya mchakato, nenda kafanye mchakato katika Wizara yako utuambie ni lini utaajiri watu hawa waweze kufanya kazi katika Wizara na sehemu nyingine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika utawala bora. Ninavyofahamu mimi utawala bora ni msingi mkubwa wa kuendesha Taifa. Utawala bora kama utausimamia vizuri hakuna haja ya kuhangaika kutumia nguvu, utawala bora unagusa kila maeneo ya nchi, kila mwananchi, kila kiongozi na kila mfanyakazi. Utawala bora ni kuheshimu Katiba na sheria ya nchi na ni kuheshimu demokrasia. Utawala bora ni kuheshimu utawala wa sheria na utawala bora ni kusimamia misingi mikuu ya uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa. Utawala bora ni kusimamia haki na usawa na uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kwa nini tunapata kazi kubwa ya kupambana na watu kwa nini tusitumie nyenzo kuu ya utawala bora kujenga misingi mizuri ya kuendesha Taifa hili? Kwa vyovyote vile kama hatutadumisha utawala bora tutazorotesha uchumi na maendeleo ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ni vizuri tuige kwa wale viongozi waliopita ili tujifunze walifanya nini. Kwa mfano, ukiangalia Waraka wa Programu ya Pamoja (Joint Program Documents), Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa William Benjamin Mkapa alichukua suala la utawala bora kama mhimili mkuu wa utawala wake katika Urais wake. Mnamo mwaka 1999 alijenga mazingira ya nidhamu ili kuweza kurekebisha masuala ya uchumi na kuweza kuleta maendeleo ya Taifa. Sera na mabadiliko yalikuwa ndiyo nguzo kuu ya mwelekeo pamoja na kuhakikisha kwamba utawala bora ndiyo dira ya Taifa. Kwa kufanya hivyo, aliweza kubadili mfumo wa dola ya Afrika katika nchi zile za Jangwa la Sahara. Matokeo yake aliweza kualikwa na World Bank kuweza kutoa hotuba ni kwa vipi ameweza kubadili masuala ya uchumi na utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kutenda haki na kuleta uchumi wa nchi hii hakuna haja ya kutumbuana majipu kwa nguvu. Silaha yetu tuliyonayo ni utawala bora, kila mtu atawajibika kwa nafasi yake. Rais atawajibika kwa nafasi yake, Waziri atawajibika kwa nafasi yake na Wizara mbalimbali zitawajibika kwa nafasi zao. Tanzania leo kwa kukosa haya niliyosema ni nchi ya 51 ambayo inakosa sifa za utawala bora katika nchi 72 na itaendelea kuwa chini kwa sababu misingi ya utawala bora imekiukwa, wanawekwa Mashehe ndani bila kosa. Watu wa aina hii hawataweza kuleta maslahi yoyote nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kimenishangaza tena sana na nitaendelea kushangaa ni Waziri anayehusika na Utawala Bora anasimama mbele ya Bunge kupongeza utawala haramu uliovunja Katiba ya nchi hii, hili ni tatizo kubwa. Zanzibar wamenyang’anywa haki yao, Waziri anakuja hapa mbele ya Bunge kusifu uvunjaji wa Katiba ya nchi, kunyang’anya demokrasia ya Wazanzibari, hili halikubaliki. Nasema Zanzibar itendewe haki yake na kamwe haki haikai chini, itakaa juu na mapambano yanaendelea hatuko kimya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili limetoa sura mbaya kwa Taifa na sura mbaya kwa Mataifa. Kukandamiza demokrasia ya wananchi ambao wamemchagua Rais wao waliomtaka na kuvunja Katiba na hatimaye kusaidiwa kupelekwa majeshi na zana nzito katika Visiwa vya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanzazibar wameumia sana, lakini dhuluma haidumu, yana mwisho, kila kitu kitaonekana. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu haki itaonekana ilikiukwa wapi. Asilimia 51.8 hawaitambui Serikali ya Shein, Serikali haramu, Serikali batili kabisa, tunasema waziwazi na tuna ushahidi wa kutosha kabisa.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi Waheshimiwa Wabunge wasome Katiba, hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nenda Sura ya Nne ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaona kwa nini Zanzibar inazungumzwa. Hakuna hata mmoja aliyekuwa hajui, akiwa mtoto, mtu mzima na wanyama wanajua ukweli uko wapi na ukweli utaendelea kujulikana uko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niseme kwamba msaidieni Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba aspect 22 za utawala bora anazifuata vizuri. (Makofi)
Narudia, msaidieni Mheshimiwa Rais aangalie aspect 22 za utawala bora anazitekeleza. Hakuna haja ya kutumbua majipu, hakuna haja ya fujo, uongozi si mabavu, mabavu yamepitwa na wakati. Mabavu ya Rais ni kufuata Kanuni na utaratibu wa utawala bora, basi! Utawala bora umejengeka katika Wizara zote hata vijijini, nadhani tukifanya hivyo haki itatendeka. Hakuna amani bila ya haki. Kama mtu unamnyang’anya haki yake na ananyamaza kimya hana imani huyo na imani haipo. Ni kama ilivyo Zanzibar, Zanzibar hakuna amani. Amani siyo kupigana kwa mtutu wa bunduki, amani ni ndani ya roho yako. Ukiwa huna amani ndani ya roho yako ndiyo unaanza kufanya mashambulizi. Kwa hiyo, nasema Zanzibar hakuna amani, tunasema waziwazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nakushukuru sana.