Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyoitoa Bungeni leo. Nina imani tunampongeza pia kwa kuwa ni Waziri ambaye anafanya kazi kwenye mazingira mazuri sana ya utawala bora.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri afungue nafsi, tunamtegemea sana kukuza wafanyabiashara, hasa wazawa wa Tanzania, kwa kipindi hiki ambacho nadhani ana uhuru mkubwa sana wa kuwasikiliza watu na kuamua. Tatizo ni kwamba Wizara haimalizi matatizo ya wafanyabiashara, yaani imekuwa kama ni mahakama, nenda, rudi, njoo kesho au keshokutwa. Nimwombe Waziri asiyakimbie matatizo ya wafanyabiashara. Wafanyabiashara wana matatizo mengi sana, wanategemea busara ya Waziri na yeye ni daktari na madaktari huwa hatukimbii matatizo, unakabiliana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nizungumze kidogo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa aniambie. Tuna kampuni inaitwa SICPA, anaifahamu, inafanya kazi ya kuweka stika kwa ajili ya kukusanya kodi ya TRA; wafanyabiashara wamemlalamikia sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri afikirie mkataba waliouweka miaka mitatu iliyopita, kila kizibo kimoja cha juisi inayotengenezwa Tanzania anakusanya shilingi nane na Serikali inapata shilingi sita. Mtu wa kuja na briefcase anachukua shilingi nane. Waziri anatambua mkataba wao umeshaisha miaka mitatu. Bado wameongeza muda na wazawa ndio wanafanya hiyo kazi. Swali langu ni kama lilelile la jana, najiuliza hivi kweli wasomi wetu wa Tanzania waliosomea mambo ya IT wameshindwa ku-copy ule mfumo tukauendesha wenyewe? Kwa sababu na mkataba unasema ile mali imeshakuwa mali ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, najua wakati wanasaini mkataba walipunjwa kwa sababu labda kulikuwa na viwanda 19, leo tuna mia na kitu. Kiwanda kimoja tu nimefanya mfano wa Azam, anachukua karibu milioni 300 mpaka 400 kwa siku. Ukienda viwanda vilivyoongezeka mia mbili na kitu mwaka jana peke yake kaondoka na shilingi bilioni 100 na wazawa na makampuni mengine yako Tanzania yanakwambia tuko tayari kuendesha huu mfumo kwa shilingi moja, Waziri ameng’ang’ania nini kwenye shilingi nane? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu anayekuchaji wewe Tanzania shilingi nane…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kampuni hiyo inayofanya kazi hiyo ya kuweka stempu inapewa leseni na Kampuni ya Serikali inayofilisika ya Posta. Posta wangeweza kufanya kazi hii na pesa zote zikaenda Serikalini. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naipokea. Darasa la saba huwa tuko active sana; nampongeza Mheshimiwa Hamis. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii kampuni inayochukua kazi hiyohiyo shilingi nane Tanzania, inafanya kazi Kenya kwa shilingi moja, inafanya kazi Uganda kwa chini ya shilingi moja. Sasa mtu huyu bado anaongezewa mkataba. Mkataba umekwisha, ongeza tena mwaka mmoja.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Tuamini kwamba Watanzania hatuna uwezo wa kuuendesha huu mfumo.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mfumo ni mali yetu, halafu tunaweka wakala tu katikati, mtu briefcase, anakusanya hela anapeleka Ulaya, halafu huku tunang’ang’ana kukamata mabegi ya watu huko Kariakoo wamebeba vijora viwili, vitatu. Hili… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.

TAARIFA

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe msemaji taarifa kwamba kulingana na utafiti uliofanywa pamoja na kushirikisha Federation ya Wenye Viwanda Tanzania, kampuni hii Tanzania ndiyo nchi peke yake Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kutoza fedha nyingi zinaoumiza viwanda na Watanzania katika kugonga stempu za kielektroniki kwenye bidhaa. Federation ya Wafanyabiashara wameshapeleka concerns zao Serikalini, lakini ninachoshangaa kampuni hii bado imeendelea kukumbatiwa katika Taifa letu.

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri; kweli hatupendi aondoke au kuharibu huu mfumo, lakini sasa hivi margin ni kubwa. Viwanda 19 kwa viwanda 200, halafu hela zote zinakwenda nje, Wizara inachukua shilingi sita, mtu kati shilingi nane, inahitaji kwenda shule kweli? Si bora muwe Madokta kama mimi wa wa heshima tu tumalizane huko? Jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wamekuja kwa Mheshimiwa Waziri, wameshakaa vikao zaidi ya kumi; ugumu uko wapi kuchukua maamuzi? Watuambie nani yuko nyuma ya mchezo huu, kwa sababu ni suala ambalo kwa mtu wa kawaida ukielezwa unajiuliza tu mara mbili, hata nikikataa kupunguza, wafanyabiashara wanasema tupunguze turudishe hata shilingi tatu wamemwambia, barua tunazo hapa, lakini Kiswahili, come tomorrow, wafanyabiashara mwisho wake labda wanasema kuna mtu nyuma yake. Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe Waziri, asiyakimbie matatizo, yeye ni daktari wa akili, wa kisomo. Amalize matatizo ya Watanzania wafanyabiashara wafanye kazi kwa uhuru. Mheshimiwa Rais anafungua masoko, wafungue uwanja wa kusikiliza watu na wawe na tabia ya kumaliza matatizo. Hatuna sababu ya kuja kupigizana kelele humu ndani, wala hatuhitaji tutajane, Hapana. Kama kuna mtu yuko nyuma ya mchezo amekula ametosha, watu wameshanawa, matongotongo yameisha, tuanze upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani, maana hata Wabunge tu kwa hili somo la muda mchache la Dkt. Musukuma hapa, wameelewa mchezo unaendaje. Sasa unahitaji kutumia degrees mbili mpaka tatu kwenye hili? Haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, nazungumzia suala la wafanyabiashara kulalamika kuhusu TRA. Tunajua Mheshimiwa Rais akitamka watu wa viwanda na biashara wafanye kazi ya kukamilisha ndoto ya Mheshimiwa Rais. Alipokuwa Bukoba alisimama kwenye mic akawaambia TRA msisumbue watu madeni ya miaka mitatu au minne nyuma. Mpaka leo bado wanasumbuliwa, ukiwauliza TRA wanasema hatujapata maelekezo kutoka Serikalini. Sasa wanataka watu wakimwona Rais wetu anazungumza tuamini kwamba wao hamna uwezo wa kutekeleza? Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, afanyie kazi matatizo ya wafanyabiashara ili aweze kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nazungumza kwa uelewa wangu na sitaki taarifa kuhusiana na Tanga Cement. Unajua sheria mbovu ndiyo zinatufukuzia wawekezaji. Najua kila mtu ana wasiwasi, lakini lazima Wabunge tuwe na akili za kufikiria mara mbilimbili. Hili suala la Tanga Cement kuna mchezo tunachekechwa, ama humu ndani au huko nje, kuna mtu pia yuko nyuma.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia watu waliofungua kesi ya Tanga Cement kuna kampuni inaitwa Chalinze Cement Limited. Nataka waniambie hii kampuni iko wapi. Nataka waniambie Kiwanda cha Cement cha Chalinze kiko wapi. Tanzania hii mimi ni mwenyeji, hiki kiwanda kiko wapi? Watu wana kiwanda mfukoni halafu wanakwambia kiko Chalinze. Nimetoka Chalinze juzi, nimezunguka Lugoba yote sijaona, na Mheshimiwa Ridhiwani yumo humu, nimemuuliza kiwanda kiko wapi, Mbunge hajui. Aasa huyo Chalinze ni nani anayetufungulia kesi? Maana yake tunachekechwa hapa, tusioneone aibu, tusitembeze dili humu ndani Waheshimiwa Wabunge. Chalinze na Chama cha Kutetea Walaji kiko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani tunatengeneza hofu, wanatengeneza utawala bora halafu wanajenga tabia mbaya. Mtu anawaambia mimi nimefilisika, nauza mali yangu, kama sheria ni mbovu, haya, akifunga tutauza skrepa? Wanampeleka wapi? Akiamua kufunga sasa mmezuia nisiuze. Nashauri, inawezekana hawa wenzetu wakati mwingine ni wajanja, wanatukwepa tusipate kodi ile ya zuio. Serikali isimamie mchakato, lakini hawa wacheza dili Waziri akija hapa najua anashughulika na hili suala, naomba atutangazie humu Bungeni hicho kiwanda cha Chalinze kiko wapi.

Mheshimiwa Spika, Wabunge ni wafanyabiashara; mimi ni Chalinze ninayefungua kiwanda cha cement, lazima nijue mkubwa ambaye nitashindana naye ni fulani, halafu anafilisika mimi nasema hapana, usifilisike, wakati mimi ndio nataka kufungua kiwanda. Jamani, hizi dili zitatumaliza Tanzania, lazima tutumie akili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri akija hapa aje na majibu mazuri, tusije tukaharibu image ya nchi yetu kwa wahuni wanaotembea na briefcase kwenye kwapa, hatuwezi kuishi kwa madili. Mshindani wako unamwoneaje wivu kufilisika mpaka ukafungue kesi, ulishaona wapi hii? Kama sheria tulitunga mbovu tuacheni kutembea na madili kwapani jamani, tutetee Tanzania. Rais anataka wawekezaji tumwache aoneshe ndoto zake, tutaulizana baadaye, ahsante. (Makofi)