Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi niweze kusema yale yanayojiri kwenye Wizara hii. Kati ya Wizara ambayo tuliitegemea na Watanzania wameendelea kuitegemea kwa ajili ya kuongeza ajira; na pili, kwa ajili ya kuongeza uchumi wa Watanzania na uchumi wa Taifa letu ni Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda pamoja na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala zima la viwanda na ambalo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema. Mwaka 2022 Serikali ilihamasisha Watanzania wa Mikoa mitatu; Dodoma, Singida na Simiyu, kwenda kuwa Mikoa ya Kimkakati ya kulima zao la alizeti ili tuweze kuondokana na wimbi kubwa la uingizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walihamasika na wakaomba ili waweze kutekeleza mkakati huo wapatiwe mbegu na vitu vingine. Pamoja na changamoto zote zilizokuwepo kwenye upatikanaji wa mbegu na pembejeo, wananchi hawa walifanya. Vile vile wakati tunapitisha bajeti, tuliondoa kodi kwenye mafuta kutoka nje ya nchi. Wananchi wetu wakalima alizeti, watu wa viwanda vya kuchakata mafuta, wameamua kupunguza bei ya mazao ya kuchakata mafuta hususan zao la alizeti. Baada ya kupunguza bei, wananchi wanaona hakuna sababu yoyote ya kuendela kulima zao la alizeti ambapo wanatumia gharama kubwa kwenye uzalishaji, likija suala zima la mapato, hawapati kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kisingizio wanachokileta leo na Mheshimiwa Waziri amekisema eti kwamba watu hawa wamefunga viwanda kwa sababu ya ukosefu wa malighafi za viwanda vyao. Hivi leo nani anaeweza kwenda kulima atumie laki tano kwenye heka moja aje avune magunia 20 aende akauze kwa elfu Sitini? Ni nani huyo anaeweza kufanya kitu cha namna hii? Kwa hiyo, kosa ni la Serikali ambao ninyi wenyewe mnaleta hapa mnatushawishi Wabunge tupunguze kodi kwenye mafuta halafu mnaendelea kutoa vibali vya mafuta.

Mheshimiwa Spika, leo wafanyabiashara wote wa Sekta ya mafuta ya kula wameamua kuagiza mafuta nje kwa sababu kodi yake ni ndogo na faida yao ni kubwa, mazao ya alizeti yanateseka mtaani yako kule wananchi hawana mahali pa kupeleka. Sasa, kwa nini tunafikia kwenye hatua hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kuanagalia kwenye viwanda vyenyewe bado hatuna viwanda vya kutosha ndani ya taifa letu. Leo ninapozungumza hapa Serikali yetu ama nchi hii hatuna viwanda vya kutengenezea hata vifungashio. Leo vifungashio vya kila zao tunatoa Kenya, vifungashio hivyo zao la Parachichi leo box tunachukua Kenya na wananadika Product from Kenya wakati parachichi inatoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchele leo wa Kyela Kifungashio kinatoka Kenya unaandikwa ni mchele wa Kutoka Kenya wakati ni mchele wa kutoka Tanzania Kyela. Hivi hata vifungashio? Viwanda leo tuna mashamba ya miti yako pale Iringa ya kutengeneza makaratasi ndio tunaagiza vifungashio kutoka Kenya? Waziri, tunakuomba tafadhari kama kuna sehemu ambayo unatakiwa uwekee mkazo ni kukuza na kutangaza bidhaa zetu. Anza na viwanda vya vifungashio, tangaza nchi yako, tangaza bidhaa yetu ili tuweze kuondokana na huu urasimu ambao tunafanyiwa na nchi za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la leseni. Imekuwa ni muda sasa na ni changamoto kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wetu wadogo wadogo kule chini. Leseni unakata lakini unatakiwa kuihuisha kila mwaka kitu ambacho kinakuwa ni kero kwa wafanyabiashara wetu. Hata hivyo, kila ninapouliza naambiwa suala la kuhuisha leseni ili kuwatambua wafanyabiashara waliopo kwenye eneo husika ama tulionao nchini. Nikawa najiuliza hivi ni kwa nini Vitambulisho vya Taifa hatuhuishi kila mwaka ili tujue nani kafa, nani yupo, nani kahama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala ni kutambua na kujua kwa nini vya taifa hatuhuishi kila mwaka? Leseni ambayo watu hawa wanajenga uchumi wa Taifa lao, wanalipa kodi kwa Taifa lao, leseni wanalipia lakini leseni hiyo kila mwaka umsumbue mwananchi huyu Kwenda kupanga foleni Manispaa kutafuta leseni. Hata hivyo, kwenye suala la leseni hilo hilo, tulisema hapa mfanyabiashara anaeanza biashara asikadiliwe kodi mpaka kipindi cha miezi sita afanye kwanza biashara. Kinachofanyika kwa uhalisia ulioko huko chini sio kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili upate TIN ni lazima uwe na leseni ambayo umetoka nayo Manispaa. Ukiwa na leseni ukienda kupata TIN ni lazima ukadiliwe. Vilevile, wanakukadilia kwa miezi hiyo ya huko nyuma. Kwa hiyo, ukishakadiliwa ni lazima ulipe hakuna namna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mfanyabiashara akishindwa kulipa anaandikiwa deni. Hilo deni linakwenda mwisho wa siku mnakwenda kufunga biashara za wafanyabiashara na mara mnapeleka kesi Mahakamani, kuzimaliza hamzimalizi, watu wanaendelea kufirisika ndani ya Taifa hili, halafu tunasema tunataka kutengeneza mabilionea wa Tanzania. kwa mfumo tulio nao hakuna mabilionea ni masikini wa Tanzania watanendelea kutngenezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kwenye suala la Leseni Mheshimiwa Waziri, wasaidieni watanzania kupata leseni iwe ni mara moja. Kama kuna michnago, kwanza michango kwenye biashara ziko lukuki, msimsumbue tena kaleseni kila mwezi, kila mwaka anaenda kuhangaika nako. Wekeni mfumo ambao utamsababisha huyu mwananchi akate leseni hata ndani ya miaka mitano afanye biashara akiwa na uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiliaji wa mapato TRA. Suala la ukadiliaji wa mapato pia nalo ni changamoto. Mtaji wangu ni kidogo, ukifika TRA kwanza unaulizwa eneo lako la biashara ni la kwako binafsi ama umekodi? Kama umekodi unaulizwa kiasi gani? Mtaji wako unaoanza nao biashara ni kiasi fulani. Nimefanya biashara nikifika wakati wa makadilio ya biashara ninakadiliwa kuanzia mtaji wangu mpaka na faida. Hii sio haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unachukuaje? Mitaji yenyewe tumekopa benki. Wajasariamali wetu hawa, wafanyabiashara wetu wanaenda kukopa benki. Kwa hiyo, unapomkadilia mpaka mtaji wake humtendei haki. Tumekuwa tukisema hapa biashara siku zote ili niweze hata kulipa mkopo wangu benki na kufanya mambo mengine tunatumia faida sio mtaji. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na Wizara ya Fedha suala la kulipa kodi kwa wafanyabiashara tu-charge kutokana na faida sio kujumlisha na mtaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa Kituo Jumuishi (One stop Center). Tumekuwa tukisema pia hili jambo kila wakati, iwe ni wawekezaji wetu lakini hata wafanyabiashara wetu wadogo wadogo. kumekuwa na changamoto sana. Wizara ya Madini wameweza, Mheshimiwa Dada yangu Ashatu, wewe unashindwa nini mama? Tusaidieni, wasaidieni wafanyabiashara wekeni kuwe na eneo moja dirisha moja. Watu hawa wakifika lile eneo aingie dirisha la kwanza atoke, aingie la pili atoke, aingie la tatu atoke badala ya changamoto leo anazozitumia mfanyabiashara. Anatakiwa kwenda TRA, manispaa, benki, OSHA, aende sijui naniā€¦ vurugu anatumia siku tatu, wiki, miezi hajakamilisha hiyo michakato. Kwa hiyo, tunaomba pia wewe kama walivyofanya Wizara ya Madini, halikadhalika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara tusaidieni hilo jambo ili tuweze kuwasaidia hawa wafanyabiashara wa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji wa Vibali vya wawekezaji. Wawekezaji wetu wengi wamekuwa wakija nchini lakini kumekuwa na urasimu sana. Tuombe angalieni Kanuni zetu, Sheria zenu. Tunatambua mnataka kupata wawekezaji wenye uhakika ndani ya Taifa letu. Punguzeni huo mlolongo, punguzeni kuvuta vuta miguu. Twendeni tufanye kazi tukimbizane na speed ya Mheshimiwa Rais, anayoifanya ili tuweze kupata wawekezaji wa kutosha watakaoleta tija ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nizungumzie na mimi suala la Sakata la Twiga pamoja na Tanga. Mheshimiwa Waziri, utanisaidia tu, nilikuwa najiuliza hivi kama Tanga amefirisika na anaona hawezi tena kuendelea na hii biashara, kwa nini achague mtu wa kumuuzia hiyo biashara yake? Kwa nini? Pia ninataka nijue hivi anachagua yeye ama Serikali ninyi ndio mnamchagulia mtu wa kununua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Kunti nimefirisika kwenye biashara yangu sioni dalili huko mbele za kuendelea na hii biashara si natangaza? Kwamba biahara hii siwezi kuendela nayo natangaza nauza hii biashara ili nipate watu wengine mbadala tofauti, waje hapa kama ni mnada nipige mnada nipate kile ambacho ninakihitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini leo tunasimama na msimamo wa kwamba Twiga ndio aende akanunue Tanga? Ninapata shida ukija hapa uniambie. Kwa nini mnalazimisha Twiga amnunue Tanga Cement? Nataka hayo majibu yenye kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa wakati wako. Ahsante sana. (Makofi)