Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye mchango wangu nami naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mzuri, uongozi bora, uongozi unaonesha matumaini na dira dhabiti ambayo inaonekana kabisa kwamba nchi yetu inakwenda kuendelea na inaondoka kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji Waziri wa Wizara hii pamoja na Katibu wake Mkuu kwa kazi nzuri na uongozi mzuri walionao kwenye Wizara hii. Kwa kweli tunaona mambo yote ya uwekezaji, viwanda na biashara yako consolidated na yanachakatwa na kuratibiwa kwa pamoja katika namna ambayo kwa kweli tunaona kwamba Taifa letu linasogea mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu asubuhi Waheshimiwa Wabunge wa Tanga, Pemba na wengine kutoka Kanda ya Ziwa wametoa michango yao kwenye sakata la uuzwaji wa Kampuni ya Tanga ambayo inataka kutwaliwa na Kampuni ya Twiga Cement. Yamkini watu wengi wamevurgwa na michango mbalimbali inayotolewa na pande mbili tofauti zenye mawazo tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tangumwaka jana wamekuwa wakifatilia jambo hili. Kwamba, mtu mwenye hisa zake, Tanga Cement anataka kuuza hisa zake kwa mtu ambaye amemchagua yeye kwa sababu anazozifahamu yeye. Mnunuaji anataka kununua zile hisa. Fair Competition Commission (FCC) wamefanya uchuunguzi na kuja na mapendekezo ya namna bora hili jambo linavyotakiwa kufanyika. Wapo wadau wengine Chama cha Walaji na chenyewe kikaenda mahakamani kushitaki kwamba zoezi lile libatilishwe; na mahakama yetu ambayo inafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria ambazo tulizitunga sisi wenyewe hapa Bungeni na yenyewe imetoa hukumu kwamba zoezi lile lisiendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka huu mwezi wa pili tumeona FCC tena wametoa tangazo kwenye Gazeti la Daily News kwamba mchakato ule uendelee kama kawaida. Mimi sipingi kwamba mtu mwenye hisa asiziuze lakini tusi-ignore mawazo ya Wabunge, wananchi na walaji ambao tangu asubuhi wamesimama hapa wakapaza sauti na kuonesha wasiwasi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Ngara sisi cement tunanunua shilingi 24,000 inayotokea Dar es Salaam, cement inayotokea Tanga huko ambako wanataka kuuza share tunanunua shilingi 22,000. Cement kuizalisha kwa siku moja, kiwanda kinaweza kikazalisha hata mifuko 5,000 lakini sisi wakulima ili tuweze kupata fedha tunalima mahindi, kuvuna mahindi ni miezi mitatu na siku nyingine zinaongezeka pale kutegemeana na mbegu uliyoipanda. Debe moja la mahindi nikiliuza ilitakiwa niweze kununua mifuko mitatu hata minne ya cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi mwananchi wa nchini ili niweze kujenga nyumba nzuri na niweze kutumia saruji maana yake ni kwamba kilimo ninachokifanya, ninachokivuna hakitoshelezi kwa sababu bei ya bidhaa ziko juu ikiwemo saruji. Wasiwasi wetu tunaoupata ni kwamba kwenye mchakato huo wa mauziano inawezekana kabisa anayetaka kununua pengine ipo siku kwa kuwa yeye wameshatuambia FCC kwamba huyu akishanunua atakuwa ana share kubwa kwenye soko anaweza akafanya chochote. Akitaka kuua wadogo anaweza akashusha bei, akitaka kupata faida kubwa anaweza kupandisha bei, vile yeye anavyoona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo hatuwezi kuliona. Vilevile anaweza akapunguza uzalishaji ili kuwe na scarcity halafu bei iweze kuongezeka. Hayo yote tunayoyazungumza ni vitu ambavyo tunavifikiria. Yamkini Serikali yetu kupitia kwa Dkt. Ashatu wameshaingia kwa undani kwa upana wake kwenye hili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba kuishauri Serikali, hivi kuna shida gani hii wizara ikitupa semina Wabunge wakatukalisha pale Msekwa tukaelewa undani wa hili jambo, kuna shida gani? Kwanza sikumbuki kama amewahi kutupa semina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza ninaomba hii wizara watuletee taarifa ya kutosha, watueleweshe mchakato mzima ulivyo. Ninaogopa kwamba wananchi wangu wa Ngara na mimi nikiwemo tunanunua bidhaa kwa gharama kubwa sana. Nimeambiwa Tanga Cement wananunua shilingi 15,000 mfuko lakini sisi Ngara shilingi 24,000 wote ni watanzania ndani ya Taifa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba busara na hekima zitumike katika jambo hili ili kuhakikisha kwamba huko mbeleni, miaka minne, mitano inayokuja Watanzania wasianze kutuzodoa na kutukumbusha kwamba Waheshimiwa Wabunge walisema mle Bungeni kwamba hili jambo lingeweza kuleta athari kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana FCC ama taasisi yoyote ndani ya Serikali iweze kupewa mamlaka ya kufanya regulation ya bidhaa za ujenzi ikiwemo saruji na nondo. Kuna kipindi unashangaa nondo inauzwa shilingi 18,000, unakwenda dukani baada ya miezi miwili unashangaa nondo ya mita 12 inauzwa 22,000, bei zinakuwa zinabadilikabadilika. Sasa sijui regulator ni huyo huyo FCC ama sijui ni nani. Niombe Serikali itazame kwa upana wake namna ambavyo hizi bidhaa za ujenzi ikiwemo saruji na nondo ziweze kuwa regulated ili kuhakikisha kwamba Watanzania hawaumii kwenye kununua bidhaa ndani ya Taifa lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mchango wangu kwenye enelo la Liganga na Mchuchuma. Uvumbuzi wa makaa ya mawe Mchuchuma ulifanyika mwaka 1860, ninazungumza miaka 163 iliyopita. Wajerumani walikuja wakagundua makaa ya mawe. Vivyo hivyo uvumbuzi wa chuma ulifanyika mwaka 1898 miaka 125 iliyopita. Wazungu wakavumbua wakaondoka, nchi yetu kupitia NDC wakatafuta mwekezaji, wakatangaza na zikajitokeza kampuni 48 ku-bid. Kati ya kampuni 48 ni kampuni moja tu ya Kichina ilionesha uwezo mkubwa, ilishinda tenda kwa kuomba kufanya miradi yote miwili, ya chuma na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba ule ukiusoma unakuta una changamoto, kwanza kwenye ule mkataba unakuta kuna partner ambaye hajulikani ni ile kampuni ile ya Kichina, Watanzania and others ambao unknown yaani hawa hawajulikani wako kwenye question mark. Hata hivyo, nchi yetu ikapata 20% kwenye ule mkataba mbali na hilo huyu Mchina akatakiwa kuleta dola 600,000,000 ili fedha hiyo sehemu yake itumike kwenda kutoa fidia kwa Watanzania wa kule Ludewa. Kwa bahati mbaya mambo mengi hayajafanyika, nampongeza Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha ili fidia iende kutolewa kwa wale wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti ulifanyika kwenye lile eneo, leseni ikapatikana akapewa Mchina na leseni imepatikana baada ya mkataba kuwa umesainiwa. Sasa, hivi kweli hatuna uchungu mali ameigundua mzungu, mikataba tumewapa watu wa nje, hata leseni tumezichakata sisi wenyewe zote tumepeleka nje, Watanzania, hakuna Mtanzania hata mmoja amepewa leseni pale, mzigo wote leseni yote wanamiliki wale wachina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya ziko taarifa kwamba Kampuni ya kichina sasa imemilikiwa na Jimbo la Sichuan. Naomba kuishauri Serikali makaa ya mawe ni dili, ukiwa na mali huna sababu ya kuhangaika. Nimeambiwa Mchina amekuja sahivi wako hapa Tanzania lakini yule original mwenyewe hayupo, kuna wengine wamekuja pengine ni wale others, unaweza ukakuta na mimi nikikomaa kwenye wale others naweza nikawa ni mimi mwenyewe, maana wale hawajulikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali wakati wa kuvuna na kuuza makaa ya mawe ni sasa, tufanye negotiation, tufanye negotiation ikamilike wakidengua dengua tumeshalipa fidia, leseni zikatwe pale, Watanzania wapewe, makaa ya mawe sio kitu cha kubembeleza bembeleza kama ilivyokuwa zamani, unachimba hapo hapo, mteja yuko hapo hapo, Serikali inauza hapo hapo, tunaingiza pesa hapo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa unyeyekevu mkubwa, Serikali ichukue mawazo haya, tuanze kuchimba makaa ya mawe na chuma sasa, baada ya kumaliza negotiation na hata ikishindikana hiyo negotiation Serikali ichimbe, Watanzania wachimbe, tupate pesa ndani ya nchi yetu, Watanzania tutajirike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja Mwenyezi Mungu akubariki kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana.