Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu anayeneemesha neema nyingi nami akanineemesha neema ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kadri zilivyojielekeza kuhudumia na kutatua kero za wananchi. Nianze na eneo la elimu bure. Safari moja huanzisha nyingine, tumeanza, pamoja na changamoto, inapaswa sasa kama Serikali ione namna ambavyo itaongeza fedha hizi ili ziweze kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati suala hili la MEM linaanza 2002 capitation tulikuwa tunapeleka dola kumi kwa kila mwanafunzi. Wakati huo exchange rate ilikuwa ni shilingi1000 leo ni shilingi 2000. Maana yake kwamba ili zitosheleze lazima tupeleke mara mbili. Naishauri Serikali iweze kuliona hili ili iweze kuongeza kiwango hiki kinachotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure chekechea hadi kidato cha nne ni sahihi. Mimi najiuliza hivi mtoto wa maskini huyu anapofika kidato cha tano anatajirika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie kwa upana wake hata kama siyo bajeti hii, bajeti ijayo iweze kuwaangalia watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la maji, maji ni hitaji la kila mmoja wetu tulioko mahali hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji alitembelea Wilaya yangu ya Magu kwa kweli alinitendea haki na Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali ijielekeze kuhakikisha kwamba wale ambao tunazungukwa na Ziwa Victoria tunapata maji ya kutosha na wengine ambao wanazungukwa na Ziwa Tanganyika nao wapate maji ya kutosha. Haiwezekani watu tunasimama tunaliangalia ziwa lakini maji hatuna, hamtutendei haki.
Naishauri Serikali hii iangalie kwa sababu uchumi wa nchi hii wachangiaji wakubwa ni akina mama lakini inapofika saa tisa za usiku akina mama wanaondoka kwenda kutafuta maji. Ninapotembelea vijiji vyangu wanalalamika wanasema hata watoto asubuhi hawawaoni hawa akina mama. Naomba sana Serikali iangalie hata kama ni kukopa kwenye mifuko ya fedha tuwekeze kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati. Namshukuru sana Naibu Waziri wa Nishati na Madini alitembelea Jimbo langu, tukatembea naye siku moja vijiji kumi, alinitendea haki Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi ukue umeme unahitajika kila mahali. Tunapozungumzia viwanda vidogo wakati mahali ambapo vinahitajika viwanda hivi vijengwe umeme haupo. Niombe Serikali kwa jitihada ilizonazo kupitia REA Phase II na III tuweze kukamilisha vijiji vyote kwa kuvipatia umeme. (Makofi)
Naomba nizungumzie afya. Hotuba ya Waziri inasema vijiji 8,043 havina zahanati. Wewe ni shahidi kwenye vijiji vyako Jimbo la Bariadi ni vijiji vikubwa sana ukizingatia na Jimbo langu la Magu nalo lina vijiji vikubwa, kuondoka kijiji kimoja kufuata huduma ya afya kijiji kingine unachukua kilometa 15 na hakuna hata zahanati za private, hakuna hata maduka ya dawa. Niishauri Serikali kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Magu wameanzisha maboma ya kutosha ya zahanati tupewe fedha za kukamilisha zahanati hizo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la viongozi wa kisiasa kwa maana ya Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji na Waheshimiwa Madiwani. Katika uongozi mgumu duniani sijui dunia au Tanzania hii, hakuna uongozi mgumu kama Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Kijiji na Mheshimiwa Diwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa lazima tuelewane vizuri na naomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu kuna kipengele kwenye viapo vyenu kinasema utamshauri Mheshimiwa Rais kwa hekima, hapa ndipo mnatakiwa mumshauri kwa hekima. Mwenyekiti wa Kitongoji yeye ndiye anayefanikisha ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati na vitu vyote vilivyoko kule. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kitongoji leo mwananchi akikamatwa mahali popote yeye ndiye anayekwenda kuandika dhamana adhaminiwe, huyu ni mtu muhimu sana. Mimi leo nikitaka kufanya ziara yeye lazima aweko. Naomba Serikali tuelewane iweke siyo fedha nyingi, tuanze na za kuanzia ili hawa watu waweze kupata posho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mheshimiwa Diwani mimi nimetokea huko niseme tu kwamba hawa watu ndiyo walionileta hapa kwamba tumpeleke mwenzetu anayetufahamu. Diwani aliyefanikiwa kuwa na gari halali usiku kucha gari yake ndiyo ambulance kupeleka wagonjwa hospitali. Leo maslahi yake tunayaona kama yanatosha hayatoshi. Niombe sana wasaidieni watu hawa na ndiyo wanaojenga siasa kwenye maeneo yetu, ni Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Madiwani. Naomba tuelewane vizuri hapa katika bajeti hii au bajeti ijayo. (Makofi)
Niendelee kusema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ndiyo ambayo wananchi walikuwa wakiingoja, ni Serikali shupavu, Serikali ya kazi tu. Mwaka fulani Mheshimiwa Rais Nyerere alitangaza Kilimo cha Kufa na Kupona, Rais Magufuli ametangaza kazi ya kufa na kupona, huyo lazima tumpongeze. Wale wanaobeza ni mioyo ambayo haina shukurani. Maandiko Matakatifu yanasema mioyo ambayo haina shukurani hukausha mema mengi. Naiomba Serikali hii ya Awamu ya Tano, wale watu ambao hawashukuru ikaushe miradi ya maendeleo isipeleke kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu aombaye hupewa, huwezi kuwa unasimama unatukana Serikali inayokujali halafu unapewa miradi. Naomba Serikali hii isiwape miradi watu hawa ambao hawana shukurani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wakisema Serikali hii haina meno, Serikali imeanza kutumbua majipu wao wanakuwa mawakala wa wale waliotumbuliwa.
Haiwezekani, tuipe heshima Serikali iweze kufanya kazi. Naomba tunapopanga miradi hii isimamiwe…
Na Wizara ili tuweze kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.