Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunikaribisha. Wizara ya Kilimo kama ambavyo tumekuwa tunajadili hapa, ina jukumu kubwa sana la kufanya uchumi wetu ukue kwa haraka (accelerated growth) na huko nako mijadala yetu ni kutayarisha Wizara ya Kilimo iweze kutoa mchango wa ukuaji wa uchumi wetu Kitaifa utakaotufikisha asilimia nane mpaka kumi. Kwa hiyo, hii Wizara ina jukumu la kutuhakikishia chakula kipo, ajira inapatikana, ustawi wa jamii na kuongeza pato la Taifa. Wizara inakuja vizuri, kuna mabadiliko, kuna maboresho na ubunifu. Sasa mimi napenda kusisitiza, ameongea Waziri, lakini najaribu kuweka uzito wa mabadiliko na ubunifu anaoufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kilimo chetu kiweze kuwa na tija kubwa, lazima kwanza tuwekeze kwa nguvu zote kwenye kilimo cha umwagiliaji. Sasa kwenye mambo ya umwagiliaji, takwimu hata za kutoka FAO zinaonesha kwamba, mfano mahindi, ukitumia mvua tunayoitegemea kwa hekta moja utavuna karibu tani moja mpaka tani 2.7. Ukienda kwenye umwagiliaji, ni kati ya tani sita mpaka tani tisa. Kule Namibia wameweza kuvuna mpaka tani 11.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni ngano waliyoongea Wizara. Kwa mvua za kudra ya Mwenyezi Mungu, unapata karibu tani nne mpaka tani tano kwa hekta moja, lakini ukitumia kilimo cha umwagiliaji unaenda tani nane mpaka tani 10. Kwa hiyo, maboresho makubwa yaende kwenye umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili ni zana za kilimo (farm implements). Sasa hivi duniani kuna zana nyingi, nitachukua tu tractors. Duniani sasa hivi kuna tractors milioni 16, hatujui Tanzania ziko ngapi, nadhani Wizara itajibu yenyewe. Mfano mzuri wa Tanzania kuiga ni nchi ya India. Mwaka 1961 tukipata uhuru, hekta 1000 India ilikuwa ina tractor 0.19; kwa mwaka 2000 India hiyo hiyo kwa hekta 1000 walikuwa na tractors tisa. Sasa hivi wana tractors 14 kwa hekta 1000. Kwa hiyo, Wizara ya Kilimo ipige mahesabu na yenyewe kwa hekta zetu tunazolima, tuna tractors ngapi? India, ukichukua jimbo linalolima sana la Punjab, wao kwenye hekta 1000 wana tractor 82. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha tatu, ni matumizi ya mbolea ikiwemo samadi. Wataalam wa Kilimo na wakemia wamepiga hesabu, ukichukua tani moja ya mahindi ukalima, ukaivuna, unachotoa ndani ya ardhi, unachopoteza ni kilogramu 25 za Nitrogen, Kilogramu 20 za Potassium, Kilogramu tano za Phosphorus. Kwa hiyo, matumizi ya mbolea ni muhimu sana. Kwa hiyo, katika hekta moja unapaswa kutumia mbolea ili urudishe virutubisho hivyo, unahitaji kilogramu 100 uongeze Nitrogen, kilogramu 100 uongeze potassium oxide na kilogramu 280 uongeze phosphorus pentoxide. Haya ni mambo ya mbolea, yanajulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha nne ni mbegu bora. Nimemsikia Waziri anaongea vizuri, na hii ni biashara kubwa sana duniani. Sasa hivi biashara ya mbegu inagharimu karibu Dola za Marekani milioni 70. Kwa hiyo, tuwekeze huko. Kwa hiyo, sisi Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara kwa ujumla, tunaunga mkono hoja ya bajeti hii kwa sababu tuna mabonde sita Mkoa wa Mara yamewekwa kwenye bajeti, nami Musoma Vijijini nina mabonde mawili; Bonde la Bugwema, Bonde la Suguti Namanyere. Ninachoomba, wale consultants waende haraka tuanze kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusisitiza sasa umuhimu wa kilimo kama biashara kubwa duniani. Mfano ni kwamba, yaani mahitaji ya chakula (Global food demand projections), mwaka 2030 tutahitaji tani bilioni kumi za chakula; na mwaka 2050 tutahitaji tani bilioni 15. Kwa hiyo, kilimo ni biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua mifano ya mazao. Kwanza ni mahindi. Kwa mwaka 2021 wauzaji wakubwa namba moja ni Marekani amefanya biashara ya Shilingi bilioni 18.8 na watatu Ukraine, amefanya biashara ya Shilingi bilioni 5.8. Mwaka 2022, makisio ni kwamba mahindi yatahitajika tani bilioni 1.075. Je, Tanzania tutauza? Kwa sasa hivi, Afrika, wazalishaji na wauzaji wakubwa ni Nigeria, South Africa, Egypt na Ethiopia. Kwa hiyo, Wizara ijitahidi angalau ifukuzane na Nigeria kuzalisha tani karibu milioni 35. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine wa biashara kubwa ya chakula duniani ni mpunga (rice) au mchele ukishakobolewa. Asilimia 50 ya watu duniani ambao sasa hivi ni bilioni nane wanatumia mchele kama chakula kikuu kila siku. Mwaka 2022 biashara ya mchele sasa, umeshakobolewa, thamani yake ilikuwa karibu Shilingi bilioni 300 na wazalishaji wakubwa ni China. Mbali na kuzalisha, lakini bado inanunua kutoka nje. Kilimo chetu, Wizara itusaidie kwenye hekta moja kama hatukupata mavuno mazuri, tuvune tani tatu mpaka sita lakini tukilima kwa uzuri zaidi, tuzidi zaidi ya tani kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara nyingine kubwa duniani ya mazao ni ngano. Kwa sasa hivi tuko watu bilioni nane duniani na bilioni tatu kila siku wanatumia ngano kama chakula. Biashara ya ngano ni kubwa. Mwaka 2020 ilikuwa ya Dola bilioni 155 na inategemewa mwaka 2028 biashara ya ngano itafika Dola bilioni 211. Kwa hiyo, ni busara kubwa sana kwa Wizara kuamua kufufua na kuwekeza kwenye kilimo cha ngano.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wazalishaji wakubwa, lakini mimi nilitaka kuongelea wanunuaji wakubwa, na hapa ndiyo naomba sisi Watanzania tusikilize vizuri. Egypt ananunua karibu Dola bilioni tano kwa mwezi; Nigeria, Indonesia, China na Turkey, Turkey ni karibu Dola bilioni tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Egypt tumewapa miradi hapa, China tumewapa miradi, Uturuki tumewapa miradi, kumbe wananunua ngano. Kwa hiyo, nasi tuwauzie ngano angalau turudishe rudishe kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine ni mihogo. Biashara ya mihogo mwaka 2022 imefika karibu tani milioni 280 na asilimia 70 ya mihogo duniani inazalishwa na nchi tano tu; Nigeria, Brazil, Thailand, Indonesia na Congo. Nigeria inazalisha kwa mwaka tani milioni 60. Sisi tuliomba tupeleke mihogo China hata tani milioni moja hatukupata. Nigeria inazalishwa kwa hekta moja tani 16. Je, kilimo ambacho tunafanya mabadiliko, mihogo tutazalisha kiasi hicho na kuvuka?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanunuzi wakubwa wa hizi biashara za mihogo, China inatumia Dola bilioni 2.2; Marekani ni ya pili, Dola milioni 150; Japan ni ya tatu Dola milioni 62. Kwa hiyo, ndugu zangu Wizara, wekeni mkazo kwenye kilimo cha mihogo, hata kule Musoma Vijijini nawasubiri kwa sababu wanunuzi wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusia biashara ya maua duniani, yaani yale maua yaliyokatwa yale. Mwaka 2022 hiyo biashara ukubwa wake ulikuwa wa bilioni 36.5. Mwaka 2027 biashara hiyo itafika karibu bilioni 45.5. angalia wazalishaji wakubwa wa maua duniani; suppliers wa kwanza ni Netherlands; wa pili, Columbia; na wa tatu, Ecuador. Sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Profesa, ni kengele ya pili hiyo.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, tena rafiki yangu, nimalizie tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua Kenya ni ya nne. Inauza maua ya milioni 766; Ethiopia ni ya tano, inauza maua milioni 235. Kwa hiyo, nimalizie kwa kusema, hata sisi maua lazima tushindane na Kenya na Ethiopia ili maua yawe ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)