Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema ambayo ametujalia.

Pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kilimo, tumeona pesa nyingi zinaendelea kuongezeka kwenye kilimo. Nimpongeze pia kwa kuendelea kusukuma suala la Katiba Mpya. weekend hii tumeona vikao vinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa Serikali mlete zile Sheria ili tuweze kuweka miundombinu vizuri kwa ajili ya kujiandaa na zoezi hilo. Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Mawaziri hawa, timu nzuri sana hii, wanafanya vizuri sana na kwa sababu ya muda sitaendelea sana hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianzie hapo, kwanza, niwapongeze wakulima wa Tanzania. Wanafanya kazi kubwa sana na ndio maana leo tunakaa hapa tunazungumza habari ya sisi kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia zaidi ya 100. Hii ni kazi ya wakulima peke yao. Kwa hiyo, kwa kweli tuwapongeze wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishauri Wizara, bei ya mazao. Bei ya mazao na hii ni kwa Tanzania nzima. Mkulima, mfugaji, mvuvi,yule ambae ni mzalishaji kabisa, wa katikati hapa anapata pesa nyingi zaidi kuliko mkulima. Kwa hiyo, ni lazima sekta hii ya kilimo kama kweli mnataka kuwalinda wakulima ni lazima tuwe na bei nzuri kwa wale wanaolima ambao hawalali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mbegu na mbolea, ripoti ya Kamati wamezungumza hapa na kwa kweli wameweka vizuri. Tumekuwa tukikutana mwisho wa mwaka ndio simu zinakuwa nyingi sana kuhusu mbolea iko wapi na mbegu iko wapi. Sasa, kwa sababu tunategemea mvua kwa asilimia kubwa sana kwenye kilimo chetu, ni vema Mheshimiwa Waziri mkaweka mipango tupate mbolea na mbegu mapema kabisa, hata kabla ya mwezi wa kumi. Kama tunajua mvua zinaanza mwezi kumi na wa kumi na moja, mna mwaka mzima wa kuanza kuweka mipango ili mbolea na mbegu zifike kwa wakulima kwa wakati tusisubiri mvua. Kwa sababu tukisubiri mvua, miundombinu, barabara zetu, magari mabovu, halafu technicality nyingi zinaongezeka hlafu zitatusumbua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi wakulima wanavuna mwezi sita, mwezi wa saba wanapata pesa. Sasa, kwa nini msiwauzie mbolea na mbegu kipindi hicho ili wahifadhi lakini lazima tutoe elimu kwa sababu ni kweli wakulima wakati fulani fulani wanahitaji elimu ya mbolea hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umwagiliaji, tunakupongeza sana Wizara hii imetengeneza a very ambitious plan ambayo ni nzuri kwamba tunataka twende kwenye umwagiliaji na ninashukuru sana hapa kwenye hotuba yenu ukurasa wa 235 nimeona Kiteto hapa Ngipa. Pia, jana nimepata simu kwamba timu zenu ziko huko sasa zinafanya upembuzi yakinifu, safi sana na hongera sana. Pia wananchi wa kiteto kwa kweli wanawasubirini kwa hamu kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiteto, nilishazungumza hapa mara nyingi, ukichukua ripoti za kilimo Kiteto ni karibu tani 400,000 za mazao mbalimbali na tunalima mazao karibu 28 tofauti tofauti. Kwa hiyo, kwa kweli ni bread basket. Mheshimiwa Waziri, ninachotaka kusema tunahitaji Soko kubwa la mazao Kiteto. Hawa wakulima wanalima sana na kama ni ardhi unataka njoo tutakupa bure.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa mzungumzaji, kwa sababu alipoanza kuzungumza ameihimiza Serikali kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya na Sheria zile zinazohusiana na Demokrasia ya Vyama Vingi ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Tume ya Uchaguzi vinakwenda haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa tamko la Mheshimiwa Rais la tarehe 6 mpaka sasa Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tayari imeshajipanga kuitisha kikao cha wadau kupitia Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hizi ambazo zimezungumzwa na Mheshimiwa Mbunge naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba tunataka kabla ya mwaka huu 2023, sheria hizi pia zitakuwa zimekwishafanyiwa kazi kusudi kila jambo liweze kwenda kwa wakati.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Edward, Taarifa hiyo.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea na tuko tayari, tunasubiri kwa hamu kubwa sana.

NAIBU SPIKA: Tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa hatua hiyo ya kuleta demokrasia nchini. (Makofi)

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, pia namna bora ya kumpongeza ni kuleta hizo sheria tupitishe haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza habari ya masoko ya mazao. Kiteto ni bread basket. Mheshimiwa Waziri, specific kuhusu suala la alizeti, Kiteto tulihamasika sana kuhusu alizeti na tulihamasisha sana wananchi. Kwa sababu tumejifunza mambo mengi sana baada ya janga hili la UVIKO 19, kwamba tunaagiza mafuta kutoka nje. Kwa hivyo, ikitokea janga lingine maana yake tunaweza tukakosa mafuta. Pia, wakulima wa Kiteto waliahamasika sana na projection zetu za alizeti mwaka 2023, ni tani 171,000. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri, utakumbuka mwaka 2022, bei ya alizeti ilikuwa nzuri sana lakini sasa bei inaenda chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa ili wakulima hao wahamasike ni lazima Serikali ije na mpango wa kulinda bei hii. Kwa sababu ni zao la kimkakati na sisi tumejiwekea mpango tukasema kama tunataka kupunguza adha hii ya kutoa mafuta kutoka nje, ni lazima wakulima wetu wailme hasa. Sasa, lazima tunataka plan, unapokuja kuhitimisha bajeti yako please utwambie. Unawambie nini wakulima wa Kiteto ambao wameweka nguvu sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, in fact nilikuwa nasoma statistic zenu kwenye taarifa yako iliyopita ya mwaka 2022 na mlisema tani milioni moja. Sasa kati ya tani milioni moja, kama Kiteto peke yake inatoa tani 171,000 lazima ufahamu kwamba wanachi wa Kiteto wamehamasika sana. Kwa hiyo, kwa kweli tunakusubiri utwambie baadae na wananchi wengi wa Kiteto wanakusikiliza wanataka kujua baadae unapohitimisha bajeti yako, nini suluhu ya bei ya zao la alizeti na mazao mengine?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni suala la wanyamapori wanaoharibu mazao ya wakulima. Hii imekuwa ni adha kubwa sana, wakulima haa wanahangaika wanalima kila kukicha, wanakimbizana na mvua lakini wanyamapori wanaharibu mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetamani sana Wizara ya kilimo, itufanyie tathimini maalum kuhusu mazao hayo ambayo yanaharibiwa na wanyamapori. Tusipoweka ulinzi, wakulima hawa ambao wanahangaika usiku na mchana kulima halafu mazao yao yanaharibiwa na wanyamapori, lazima kama nchi tuwe na mkakati maalum ili kunusuru wakulima hawa ambao hawalali usiku na mchana wakilinda mazao yao. Tunataka kuona exactly cost ambayo inaletwa na wanyamapori kwa wakulima hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mitaji ya wakulima, tunajua wakulima wetu wengi sana wanahangaika na mitaji, wanakwenda wakati mwingine kwenye mabenki wanaomba kupata mitaji kwa ajili ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri, bajeti yako ya mwaka 2022 ukurasa wa 135 ulisema hivi, naomba ninukuu; “Wizara imeunda kamati maalumu inayohusisha viongozi mbalimbali katika Wizara ya Kilimo, taasisi na Mfuko wa Fedha na Maendeleo kwa ajili ya kupitia ushauri wa namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya Miradi ya maendeleo ya kilimo.”

Mheshimiwa Naibu Spika, tutapenda sana utuambie baadae hili mmefikia wapi? Wakulima wanahitaji hii mitaji kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tulizungumza na ilani yetu iko wazi kwamba tunataka kupunguza jembe la Mkono kutoka asilimia 53 mpka asilimia 10 mwaka 2025. kwa mfano; Mradi wa matrekta umefikia wapi? Wakulima wangu wa Kiteto, tuliomba Serikali iweze kuweka pesa nyingi ili wakulima waweze kupata matekta mazuri ya bei nafuu na ya muda mrefu ili wakulima hawa kuendelea kulima.

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)