Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi pia kuchangia bajeti ya Kilimo. Pia niungane na Wabunge waliotangulia kuunga mkono bajeti hii kwa sababu kwa kiasi kikubwa imetendea haki wananchi wa Mkoa wa Mororgoro lakini hususani Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa. Kuna mambo mengi ambayo yanaendelea lakini kubwa kuliko yote, adha kubwa ya wananchi wa Bonde la Ruhende kule katika Jimbo la Mikumi, ilikuwa ni suala la uhakika wa kuuza mazao yao ya miwa ambayo ndio uti wa mgongo wa lile bonde.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ilikuwa uwezo mdogo wa Kiwanda cha Ilovo kuhimili uzalishaji mkubwa wa miwa kutoka kwa wakulima. Hata hivyo Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, iliahidi kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwamba inaenda kusimamia kupanua kiwanda cha Ilovo ambacho Serikali ni mbia. Sasa hivi kuna uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi bilioni 571 unaendelea. Uzalishaji ambao unampa uhakika wa soko mkulima wa muwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo changamoto kubwa ilikuwa wakulima kuchomeana mashamba. Adha hii ilikuwa kubwa na ilikuwa inatishia usalama wa wakulima katika bonde lile. Serikali iliahidi kuja na mpango mkakati wa kudhibiti hali hiyo kwa kuanzisha mavuno kwa zone lakini pia ku–reform Vyama vya Ushirika. Ahadi ile ilitekelezwa kikamilifu, sasa hivi uvunaji unaendelea, haki inatendeka, wakulima hawachomeani miwa yao, uhakika wa kuongezeka kwa mavuno ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba upanuzi wa kiwanda hiki cha Ilovo unaenda kukifanya moja ya kuwa Viwanda vikubwa kabisa vya sukari katika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tafsiri yake ni nini? Maana yake inaenda kuhitaji mavuno makubwa zaidi ya miwa. Uwezo wa wakulima na idadi ya wakulima wetu hawawezi ku-feed kiwanda hiki. Hata hivyo, tuna maeneo ambayo tunapaswa sasa hivi kuyaangalia, hususani katika kuongeza tija katika kilimo cha muwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pale Mkulazi, miundombinu ya kisasa ambayo imewekwa pale lakini tunaona katika mashamba makubwa ambayo Serikali ilikuwa inamiliki baadae ikabinafsisha, miundombinu mikubwa. Ukienda katika Bonde la Ruhende, ukiona shamba ambalo limechoka ni la wananchi, sasa wakati umefika mashamba ya wananchi kupendeza na kutengenezewa miundombinu kama mashamba ya wawekezaji na Serikali ambayo ikiwa inamiliki mashamba yao inavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kile ambacho kinafanyika Mkulazi, kinapaswa kwenda kufanyika katika mashamba ya watu, wakabidhiwe na walipe kulingana na mavuno yao. Kama hatutawekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ni ngumu sana kupiga hatua ya maana, na katika hili ni ngumu sana kufika huko ambako tunakoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umwagiliaji, kama tunazungumzia kwamba tuna hekta zaidi ya milioni 44 lakini ambazo zinamwagiliwa na zinatumika ni pungufu ya zaidi ya asilimia mbili kati ya hizo, tunaona kabisa kwamba tuna safari ndefu. Bado malengo ambayo tunayaona kupitia hotuba ya Waziri, kwamba ifikapo 2025 watafikia uwezo wa Umwagiliaji hekta milioni moja, bado ni ndogo sana na hatuwezi kufika. Pia katika hili naomba kutoa rai, sekta binafsi zihusishwe, sekta binafsi ziwezeshwe katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji lakini pia mkulima atengenezewe mazingira rafiki ili tija ambayo inatokana na kilimo, mauzo ambayo yanatokana na kilimo na mazao aweze kulipia miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya chakula tunaona 2020/2021 kulikuwa na tani milioni 18, 2021/2022 kulikuwa na tani milioni 17 lakini mahitaji ya 2023/2024 ni milioni 15. Kwa hiyo, tunaona kabisa jinsi tunavyoshuka lakini tunaambiwa kwamba ziada ambayo inakwenda kupataikana ni asilimia 115. Sasa, kama 2021/2022, ziada ilikuwa asilimia 125 na bado bei ya mazao ilikuwa imependa sokoni. Sasa hivi tunapokwenda kuzungumza kwamba tunakwenda kupata ziada ya asilimia 114, napata walakini kwamba bei ya vyakula inakwenda kuwaje huko masokoni?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matarajio na makadirio kwamba ifikapo 2030, tunahitaji tani milioni 20, matarajio ya mwaka 2023 ni tani milioni 15. Kwa hiyo, tuna gap ya tani milioni tano ili kukidhi matarajio. Kwa hiyo, hapa unaweza kuona mahitaji ya lazima kuona nini ambacho tunaweza kufanya kuboresha hali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la uratibu, haya yote ambayo Mheshimiwa Waziri, amezungumza hayatafanikiwa kama hakutakuwa na uratibu makini katika kuangalia jinsi gani tunakwenda kumlinda mkulima wa Tanzania. Pia, katika hili, uhusiano wa Wizara na Wizara, uhusiano wa taasisi ndani ya Serikali ni muhimu. Lazima taasisi zizungumze ndani ya Serikali, lazima Wizara zizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano pale Kilosa, mwaka 2022 ndege (kweleakwelea) walikuwa wanakula mpunga wa wakulima wetu. Ilichukua wiki tatu kabla ya ndege kufika kwa sababu kulikuwa na urasimu katika kutoa kibali kwa watu wa Hifadhi. Mwaka 2023, tulitoa taarifa tarehe 17 Aprili, kwamba ndege kwelea kwelea wanakula mipunga ya watu katika Kata za Tindiga, Mabwelebwele, Kilangali, zombo na hata Ulaya. Nini ambacho kimetokea? Ndege ile imeenda jana, kwa nini imeenda jana? Kwa sababu kulikuwa na urasimu wa kibali kutoka katika vyombo vyetu vya ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vyombo vyetu vya ulinzi vinapaswa kufahamu, usalama wa raia na mali zake ni pamoja na mazao mashambani. Nani ambae anawajibika katika kulinda mazao ya wakulima mashambani kama sio Serikali?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ni lazima Wizara ya Kilimo ipewe ushirikiano na taasisi za Serikali lakini pia na Wizara ambazo zinawajibika moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)