Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipoa fursa ya kuchangia Wizara hii ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanzia na ukusanyaji wa maduhuli, kama ulivyoona, lipo tatizo la ukusanyaji wa maduhuli ambalo limeoneshwa katika Taarifa ya Wizara lakini Taarifa ya Kamati. Niungane na Taarifa ya Kamati kama walivyosema, unaona kabisa wao walikadiria kukusanya bilioni 126.1 lakini wamekusanya milioni 600 tu, asilimia 0.48. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, nawaona bado vijana, wana uwezo mkubwa kabisa. Hivi mmekwama wapi? Mtueleweshe mnakwama wapi kukusanya kiasi hicho, kiasi kwamba sisi hapa leo tuwapitishie bajeti nyingine wakati mmeshindwa kukusanya asilimia hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kabisa jinsi ambavyo wameweka, kwamba makadirio ya mwaka 2023/2024 ni bilioni 10, basi wangeenda waweke makadirio hata iwe bilioni moja ambayo mtaifikia kuliko kuweka bilioni 10 ambayo hamtaifikia kama mlivyokuwa hamjaifikia hiyo mliyoifanya. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa niombe atupe maelezo; nini kinaleta utofauti huo mkubwa wa ukusanyaji wa maduhuli? Ama makadirio hayako kiuhalisia? Mnakwama wapi? Ningependa hilo aweze kuja na utuambie changamoto iko wapi ama hawana uhakika wa vyanzo vyeo vya makusanyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Tume ya Umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri wakati anasoma taarifa yake katika ibara ya 247 ameeleza kuwa tuna hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, zinazotumika sasa ni hekta laki 727.2, tu ambayo ni asilimia 2.5 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kati ya hekta 29.4 tunatumia asilimia 2.5 tu kwa umwagiliaji. Ndiyo maana unakuta kwamba tunaenda kuagiza ngano nje, tunakwenda kuagiza bidhaa zingine kule kwa sababu hatujaweza kutumia vizuri ipasavyo sekta hii. Ukiangalia kwa mwaka wa fedha uliopita tulipitisha bajeti, na tunamshukuru Mheshimiwa Rais aliongeza ile bajeti ikawa kubwa sana. Sasa twende kwenye sekta ya umwagiliaji ilivyopata fedha. Katika mwaka huu tume iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 257.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji. Hadi Februari 2023 bilioni 46.687 tu ambazo ni sawa na asilimia 18 ndizo zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya kutumika, asilimia 82 hazijatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika hii maana yake nini? Hii maana yake ni kwamba, tunapitisha bajeti na tukishapitisha bajeti zile fedha hazitoki, matokeo yake huko nje tunaonekana tuna bajeti kubwa, Waziri wa fedha yuko hapa lakini fedha hazijaenda, Kwa hiyo ndio maana unakuta kwamba miradi mingi haitekelezwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nishukuru, kuna Skimu ya Mkombozi ambayo iko Isimani katika Mkoa wangu wa Iringa ambayo mmeipa shilingi bilioni 55 na kwa kweli inaenda vizuri, hii skimu mmeipa fedha. Lakini skimu nyingine zote zimekosa, ni kwa sababu hizo fedha hazikutolewa zote. Ni ombi langu, Skimu ya Magozi ambayo iko Pawaga Jimbo la Isimani naomba nayo muipe fedha, Skimu ya Nyabula naomba nayo muipe fedha ili wananchi waweze kufanya kazi ya umwagiliaji wapate mazao kwa sababu ndiyo wanayoyategemea katika uzalishaji mali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho ninataka nikizungumzie hapa ni nini? Usipopeleka hizo fedha wananchi wanakuwa na hali ngumu ya maisha, wanakosa vyakula kwa sababu kule wanategemea sana hizo skimu, kwa hiyo wananchi wetu wametutuma tunaomba fedha ziende kwa ajili ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika changamoto ya watumishi katika sekta hii, hasa maafisa ugani. Tuna mahitaji ya watumishi 20,000 waliopo ni 6,000, tuna upungufu wa asilimia 67 wa maafisa ugani. Sasa hii ukiangalia na namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine ambavyo wamezungumzia kuhusu uzalishaji, unaona jinsi ambavyo tunashindwa kufikia targets zetu za kilimo. Kwa maana hiyo hatuwezi kuchangia pato la taifa vizuri kama hatuna maafisa ugani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sisi tuko huko vijijini tunakua ilikuwa maafisa ugani wakija pale kijijini kwa ajili ya kutoa maelekezo wanaitisha mkutano, wananchi wanakwenda kwenye shamba moja lililochaguliwa na wanatoa malekezo. Ningependa kujua, utaratibu unaotumika sasa hivi ukoje? Ili tuweze kuutambua. Kwa sababu kweli mmewagawia pikipiki na kwenye bajeti yenu mmeonesha kwamba mtawapa magari. Tunataka kujua utaratibu uoje ili wananchi wale wa chini waweze kutumika vizuriā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie. Kuna vijana tumewapeleka Israel, wanarudi wakiwa na ujuzi mkubwa. Niwaombe muwaunganisha katika mradi wa BBT ili waweze kuwa saidia vijana wetu kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.