Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukupongeza wewe kwa kuongozo kikao hiki. Pia nimshukuru Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, nimshukuru Waziri Bashe kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwanza niombe Waziri, Mheshimiwa Bashe na Naibu wake, wapokee pongezi za dhati kutoka Muleba kwa kumteua ndugu yangu na ndugu yetu Rugambwa kuwa Wakala wa Mbolea, hongera sana. Wametusogezea mbolea karibu na wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo ombi Muleba, naunga hoja mkono lakini tuna ombi. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yake akiongelea pampu na matenki madogo ya kumwagilizia mashamba. Kule Muleba tulikuwa tukilima kahawa na asilimia zaidi ya 40 ya kahawa yote Tanzania inatoka Mkoa wa Kagera na zaidi ya nusu ya kahawa inayotoka Mkoa wa Kagera inatoka Muleba. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri sasa kule Muleba akatusogezee karibu zile pampu. Hatutakubali visima, tunayo mito, tuna Mto Ng’ondo na mito mingine mingi tutavuta maji kutoka kwenye, mito tutamwagilizia kahawa. Nimhakikishie Mheshimiwa Waziri akifanya hili kwa kutuletea pampu pale Muleba sasa mavuno ya kahawa yanakwenda kuongezeka mara dufu. Natumaini Mheshimiwa Waziri amelipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tunazalisha kahawa, tumekuwa na matatizo makubwa sana hasa kwenye Mkoa wa Kagera na pale Muleba, lakini nimshukuru tena Mheshimiwa Waziri, mwaka huu soko la kahawa Wilaya ya Muleba limetulia, namshukuru sana na nimwombe aendelee kutia msisitizo kwenye hili. Kama hakuna utulivu kwa wakulima, kahawa itapotea lakini kwa kuwa tumewekeza na ametoa maelekezo thabiti tunamshukuru sana na aendelee kutusaidia. Wakulima wanamshukuru sana na wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Mama Samia kwa kuwapa utulivu kwenye mazao yao. Tunaendelea kulisema na Waziri namshukuru kwa kulisema hili, kahawa ni mali ya wakulima, tuwalinde na tuhakikishe kwamba tunalinda mipaka ya nchi kahawa isitoke nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Muhongo amesema asubuhi na Kaka yangu Mwijage amechangia. Tukiangalia na tukifanya ulinganisho kati ya wakulima wa kahawa Nchini Tanzania na jirani zetu Uganda ni aibu kwa kweli. Mheshimiwa nakuomba Waziri kwenye hili tubadilishe mizania ya mauzo yetu nje ya nchi. Tunapolinganisha na nchi Jirani, hatupashwi kulingana nao, basically tunapashwa kuwa mbele yao, tukichukulia ukubwa wa Taifa letu, tukichukulia mikakati tuliyonayo na nimshukuru kwa mkakati aliokuja nao. Tunawaomba wakulima wetu hasa Wilaya ya Muleba.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naongelea Muleba, Jimbo langu, tunaomba miche bora kwa ajili ya kilimo na ulimaji mpya wa mazao ya kahawa. Tunalo eneo kubwa na tumekuwa tukiongelea masuala ya Mwisa, kama utafuatilia mchango wangu kwenye mifugo na kilimo, tulisema badala ya kutuletea vitalu pekee yake tutenge eneo kwa ajili ya kilimo cha kahawa, tutenge eneo kwa ajili ya kufuga. Tunapoongelea kufuga na kulima ina maana tukipata mbolea kwenye vitalu vyetu tunaweka kwenye mashamba yetu ya kahawa na tunaongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili lazima tulifunganishe na uongezaji wa thamani wa kahawa tunayozalisha. Kagera tuna Kiwanda chetu cha TANICA pale. Sasa ni muda muafaka kwa Mheshimiwa Waziri akiangalie hiki Kiwanda cha TANICA ili kahawa inayozalishwa ikawe processed pale, tukiongezee nguvu, tukiongezee mtaji. Namshukuru Waziri nilipouliza swali juzi ameshachukua hatua. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia mizania hapa, Tanzania amesema kwenye Hotuba yake Mheshimiwa Waziri, mwaka jana tumeuza kahawa yenye thamani ya milioni 200 USD, lakini jirani pale ambaye ana eneo dogo ameuza zaidi ya milioni 862. Sasa tuna mkakati gani kuhakikisha kwamba tuna overtake huyu ili na sisi tuonekane, sisi ni wa 26, yeye jirani yetu ni watatu. Lazima tuwe na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba huyu jirani yetu tuna mpiku na sisi tunakuwa mbele yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, Kagera tuna zao la vanila, Mheshimiwa Waziri zao la vanila Kagera ambalo linalimwa na wakulima wengi na linalimwa kwenye mibuni yetu hiyo yaani inter-cropping tuna ndizi, tuna migomba, tuna kahawa, tuna pamba na vanila mle, lakini tuna tatizo moja, hatuna soko la uhakika la mazao ya vanila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono. (Makofi)