Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana huu na kwa namna ya pekee sana nipongeze Wizara ya Kilimo kwa mitazamo yao chanya, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukubali kuwasaidia sana Wizara ya Kilimo kwa sababu nimeona hizi siku chache zilizopita Wizara ya Kilimo wamekuwa wakipata fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa BBT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri kwenye mradi huu wa BBT Mheshimiwa Waziri hakikisha Wizara yako inaungana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuweza kuona mnyororo mzima wa thamani na kazi zinazofanywa na vijana kwenye hili suala la BBT linaingia sasa masokoni kwa maana ya kuwashirikisha TANTRADE lakini pia na kuwashirikisha watu wa Warehouse Receipts ili kuweza kupata matokeo mazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ndani ya Bunge hili imetolewa michango mingi sana inayohusiana na kuongeza thamani ya vitu mbalimbali ikiwemo mazao na mwenyewe umekiri kwamba una mikakati ya kutaka kuongeza thamani ya mazao ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wazalishaji wa korosho kwa maana ya wenye viwanda vidogo na viwanda vikubwa na umeomba shilingi zaidi ya bilioni 10 ili kuweza kuwasaidia hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikukumbushe kwa dhati kabisa kama utakumbuka wakati wa kikao chetu cha wadau wa korosho kuna mwenye kiwanda mmoja anayo experience ya kutosha tu alikuwa anatokea Mtwara, Ndugu Mkimi alikuwa na malalamiko yake mengi sana, sasa sina hakika baada ya maelekezo yako kama kuna chochote kimefanyika mpaka sasa hivi. Kwa hiyo, niombe ufuatilie hili ili uweze kuona maelekezo unayoyatoa yanatekelezwa kuweza kuwasaidia watu hawa wenye viwanda tusiwakatishe tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri upo hapo lakini nataka ufahamu kwamba wakulima wa nchi hii walikuwa wamekata tamaa kabisa na wengi walikuwa wanataka kuacha shughuli za kilimo lakini baada ya kuja wewe sasa unaonekana kama mkombozi na tunataka tukuongezee machache ili uweze kufanya vizuri zaidi kazi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwenye Wizara uliyoko ndiko ambako kinafanyika kilimo cha korosho na kilimo cha kahawa na lazima utambue kwamba kuna watoa huduma kwa maana ya wanaopeleka magunia, wanaopeleka viuatilifu pamoja na dawa. Toka mwaka 2017 kuna ambao wanadai nao wanadaiwa na mabenki na wengine wanafilisiwa na mabenki haya kwa sababu mikataba yao ilikuwa ni kwamba watalipa immediately baada ya ku-supply Serikalini. Sasa na wewe wasitake kukuingiza kwenye kichaka hiki cha neno la uhakiki kila mara wanapokwenda kudai madeni yao wanaambiwa uhakiki unafanyika, ama uhakiki haujafanyika lakini ni kama tu utaratibu fulani wa kutaka kuchelewesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani ya Bunge lako hili Tukufu palipita azimio hapa baada ya kuletwa Taarifa ya PAC kwamba watoa zabuni hasa wa ndani pamoja na wa nje walipwe fedha zao ili waweze kuhudumia vizuri zaidi wakulima. Kwa hiyo, tukuombe na Mheshimiwa wakati unapokuja hapa ku-windup na hili ndiyo eneo la kuweza kukushikia hata shilingi yako kwa sababu ni jambo la kisera. Hakikisha unatueleza mkakati wako wa kuwalipa wazabuni ili waweze kuwahudumia zaidi wakulima na tuweze kupata tija kwenye kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Waziri ni suala la vinywaji. Tunapozalisha korosho asilimia zaidi ya 30 ama 40 ya korosho panapatikana matunda yanaitwa mabibo, yakikaushwa haya yanaitwa kochoko, ukiyapika, kabla haujayapika unapata kinywaji fulani kinaitwa uraka hata uki-google hapo utaona inaitwa urak kwa sababu imeanzia huko kwa wazungu na maeneo ya India imekuja mpaka huku kwetu, kinanywewa, hii inaitwa pombe halali. Ukikausha, ukaloweka, ukachemsha ukapata mvuke inapatikana pombe ya moshi ndiyo hii inayoitwa gongo, lakini Wizara yako wewe mwenyewe na Wizara ya Viwanda na Biashara walipeleka fedha za utafiti Chuo cha Naliendele ili kuweza kuona kama kutokana na gongo hii kinaweza kikafanyika kitu kizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuja kugundua gongo inayopatikana kwenye mabibo inatoa ethanol, inatoa methanol, unapata pale ndani alcohol, unapata chakula cha mifugo lakini pamoja na juice ya mabibo ambayo inaitwa cashew apple. Sasa Serikali imeshawekeza, utafiti umekamilika, kilichobakia sasa ni kufanya implementation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoeleza kuhusu mnyororo wa thamani wa zao la korosho pamoja na mambo ya imani na mengine lakini hii ni bishara na ni ajira na nataka nije kusikia unasema nini kuhusu gongo inayopatikana Mikoa ya Mtwara na Lindi na maeneo mengine, ninakumbuka hapa Mheshimiwa Sichalwe juzi wakati anachangia alileta hapa vinywaji vingi sana vinavyozalishwa nje ya nchi lakini vinaletwa Tanzania. Kwa hiyo, tuone sasa Wizara yako ina mkakati gani wa kusaidia kufanya saving kwenye hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine wakulima wa korosho wametuagiza na mimi wameniagiza nije kwako niseme makato yanayokatwa kwenye zao la korosho ni makubwa sana. Tunaomba kufanya review kwenye zao hili ili kuweza kupata bei bora. Kadri ya makato yanavyokuwa mengi, yawe ya mkulima au yawe ya mnunuzi kwa vyovyote vile mwisho wa siku haya yote yanakwenda kuwekwa kwa mkulima. Hatuwezi kupata bei bora kama haya tunayaacha kama yalivyo. Kwa hiyo tuone namna ambavyo utakuja kuleta hapa hiyo taarifa yako tuweze kukusaidia kuchambua na kupunguza baadhi ya tozo zilizopo kwa mkulima na tozo zingine ambazo ziko kwa mnunuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunataka tuiombe Serikali kwa sababu ya muda sasa tuishauri kwamba makato kwa ujumla ni shilingi 1,130. Sasa mlete hapa taarifa na mtuchambulie tuone namna ya kuwasaidia lipi liondoke, lipi libaki. Ukienda kwenye kahawa wanakata kama shilingi 200 lakini hiyo ndiyo italipa TARI, italipa kule Bodi yao ya Kahawa, italipa zile union zao, italipa AMCOS, italipa na mambo mengine isipokuwa CESS na hayo yanayobakia. Kwa hiyo, tukuombe Mheshimiwa Waziri ulete hapa tukusaidie kuchambua ili tuweze kuona tozo hizi zinazofanana ziondolewe kwa sababu zimekuwa zinawaumiza sasa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine tunaomba na tulikuambia wakati wa kikao cha wadau, hebu muombe CAG akatusaidie kukagua Mfuko wa Ununuzi wa Pamoja wa Pembejeo. Wakulima tunaotokea kwenye eneo hilo haturidhiki na namna manunuzi yalivyofanyika kwenye miaka iliyopita hasa zaidi 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na ndiyo maana unapata ugumu wewe mwenyewe binafsi kuwalipa suppliers walio supply magunia lakini pia pamoja na walio- supply pembejeo kwa sababu ukamilifu wake haukuwa mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine Serikali ifute ushuru huu wa shilingi 81 ambao unatozwa kwenye magunia, kwa sababu yale ni vifungashio. Tuwape uhuru wanunuzi wa kuamua watasafirisha mizigo yao kwa kutumia kifungashio cha aina gani. Kuna ambao wanasafirisha kwenye makontena lakini bado utawachaji fedha ya gunia. Kuna ambao wanasafirisha kwa kumwaga kwenye meli kwa maana ya zile bulk supplier lakini bado utaendelea kuwachaji kwenye magunia na hizi gharama zote mwisho wa siku zinarudi kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mfuko wa Ununuzi wa Pembejeo wa Pamoja, achia hii kazi ikafanywe na CBT kwa sababu kuna fedha ya Serikali na niombe sasa upeleke kwenda kukagua.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana pamoja na muda mfupi, lakini naamini mawazo yangu Mheshimiwa Waziri ameyasikia, hata hivyo nimechangia kwa maandishi kwa sababu muda ni mfupi na mambo ya kuishauri Wizara hii tunayo mengi sana. Nikutakie kila la kheri wakati unahitimisha. (Makofi)