Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Kilimo, Wizara ambayo ni tegemeo kubwa kwa Taifa, Wizara ambayo imebeba uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Watendaji, Katibu Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri na matumaini makubwa yaliyosheheni ndani ya hotuba yao kwa kuelezea kwamba ni jinsi gani wanakuja kutatua suala zima la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe tu kwamba kama nchi tunategemea sana mvua lakini katika Hotuba yake Mheshimiwa Waziri alivyoielezea ni kweli inakuja kujibu matatizo ya wakulima wa Tanzania. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri zaidi lakini itakumbukwa sana mwaka huu, tumeona mazao mengi sana yakikosa mvua na kukosa wakulima mazao ya kutosha kwa ajili ya nchi yetu. Katika suala zima kwenye hotuba yako jinsi ulivyoelezea kwamba unahakikisha utachimba mabwawa na kuleta zana bora za kilimo, haya tukiyachukua naamini kabisa nchi itakuwa imepiga hatua na tutakuwa hatuna changamoto ya kufukuzana na wakulima wanavyotaka kuuza mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la maafisa ugani. Maafisa ugani wetu sawa tunajua wana changamoto lakini ni watu ambao wakitoka kwenye vyuo wanapelekwa kwenye maeneo ambayo sasa waende hawajui wanaenda kukutana na nani. Ikumbukwe miaka ya zamani kulikuwa na nyumba za maafisa wa kilimo kwenye Utawala wa Hayati Baba wa Taifa alikuwa ni afisa ambaye anaheshimika kwenye maeneo, kwa sababu ndiyo mtu pekee anaweza akabadilisha mazingira ya nchi hii kwa maana ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukuombe Mheshimiwa Waziri na Wizara yako hebu weka mkakati mzuri kwa Maafisa Ugani hawa, tukiwawezesha vizuri najua umeanza hatua nzuri za kwanza umewagawia piki piki na umewafungia vifaa kwa ajili ya kuwa-trace lakini siyo hivyo tu na mazingira wanayofanyia kazi yafanane na elimu waliyoipata. Naamini kabisa tutakuwa na uzalishaji ulio na tija ndani ya nchi kwa sababu tayari ni watu ambao wamesomea utaalamu utakaokidhi kwenye mahitaji ya wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza Wizara kwa miradi mizuri mnayobuni kwenye Mradi wa BBT ambao mmeanzisha, ni jambo zuri, lakini tuanze turudi na huku nyuma kwa wakulima walioko vijijini, naamini kabisa hawa wakulima walioko vijijini wakiwezeshwa wanaweza wakafanya kazi kubwa na nzuri zaidi. Maana yake ni kwamba kwa sababu tayari wao wana zana wakonayo tayari, hawa vijana tunaowatengeneza wengi wao wanatoka kwenye vyuo wanakwenda kupewa maeneo, lakini kule kijijini kuna wakulima ambao tayari wao wameshajiajiri miaka na miaka na ndiyo waliotufikisha hapa. Kwa hiyo, ombi langu hebu sasa mawazo ya Wizara tuyahamishe tuwapelekee miundombinu iliyosahihi kwa wakulima wetu walioko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mababu zetu, mama zetu tukiwawezesha na sasa hivi tuna changamoto kubwa. Kila humu ndani kuna kesi za uhifadhi, malisho ya ng’ombe na vitu vingine, kila siku kelele ya namna hiyo. Mheshimiwa Waziri wale wakulima walioko vijijini, ukiwapelekea zana kuwawezesha matrekta mimi naamini tutafanya kazi kubwa ukija kulinganisha na hawa BBT utajikuta umefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata fursa nzuri katika mnyororo mzima wa thamani ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine sambamba na hayo, tunakaa hapa kama Bunge la Bajeti tunazungumzia mapato. Mapato yanatokana na nini? Mheshimiwa Waziri ameyataja lakini tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwaamini nyie vijana kwa kazi kubwa Mheshimiwa Waziri kwa kuwapa fedha nyingi shilingi bilioni 970. Kwa hiyo tuna imani na ninyi kwamba mnaweza mkafanya vizuri zaidi, kwa umri wenu huo msipotenda mema hamtaenda Mbinguni kwa sababu naamini Watanzania wote wanawategemeeni sana ninyi. Tukisimamia kilimo, mifugo, nyuki na uvuvi naamini kabisa tunaweza tukapiga hatua na nchi yetu ikawa vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye sera zetu za kilimo. Mheshimiwa Waziri umetaja unakuja kufanya mabadiliko makubwa kwenye ushirika na kwenye sera nzima ya kilimo. Hilo ndiyo jambo la muhimu maana matamko yanayotokea kila mwaka yanachanganya na kufedhehesha kilimo cha mazao. Mfano tunaotoka Kanda ya Ziwa, ukichukua takwimu za miaka mitatu ya nyuma na mpaka leo tulifika mpaka milioni 350, leo tunazungumzia milioni 170, kwa hiyo tumepoteza kiase gani cha fedha za kigeni tungeingiza kwenye nchi lakini kwa sababu ya kutokuwa na sera iliyobora na iliyo imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa mipango yako mizuri hii ya kusimamia ushirika pamoja na kilimo ni jambo jema, lakini lazima kwenye ushirika muende mkafanye mabadiliko makubwa kwa sababu mtu mzuri akifanya miaka mitatu lazima atoke. Sasa siamini kama mfumo huu unaweza ukatengeneza mazingira unayoyafikiria wewe, lakini tukiyaacha yakawa open kwamba kiongozi aliyeaminiwa na ushirika au na jamii kwenye eneo husika atatolewa kulingana na changamoto zake lakini kwenye mpango huu wa kuchukua miaka mitatu akishamaliza anaondoka tutapiga kelele kila kukicha hautabadilisha mfumo mzima wa ushirika, kwa sababu ni sehemu ambayo wanaamini wasipomsikiliza boss fulani mambo hayataenda kama inavyotarajiwa. Kwa hiyo niombe sana Wizara haya mambo iyachukue na iyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)