Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana namimi kunipa fursa hii ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu wa 2023/2024. Kwanza naipongeza Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kuongeza Bajeti hii ya Kilimo tena mwaka huu kwa asilimia 29, ni pongezi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo mawili tu. Nitachangia zao la tumbaku lakini pia kilimo cha umwagiliaji. Kuhusu zao la tumbaku, kwa kipindi cha miaka minne zao la tumbaku lilikaribia kufa kabisa. Mimi humu ndani Bunge lililopita walikuwa wananiita mzee wa matumbaku, kwa sababu nilikuwa napambana kweli kweli kuleta kilimo cha tumbaku juu lakini bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alisikia kilio hicho vilevile akafanya hatua kubwa sana, leo anastahili pongezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule tunapambana kulikuwa hakuna ununuzi wa tumbaku na wakulima walikuwa tumbaku yao hainunuliwi na wakati fulani ikiitwa makinikia, lakini hivi sasa tunaongelea masoko ya tumbaku yanarindima huko Tabora na maeneo mengine ya tumbaku. Hili siyo jambo rahisi, tulikuwa na wanunuzi watatu na mmoja akaondoka akiwa TLTC lakini tumepata sasa wanunuzi wa tumbaku sita kutoka wawili. Hongera sana Serikali na Mheshimiwa Bashe hatua kubwa waliyochukua ya kutafuta wanunuzi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi Mheshimiwa Rais ametuteulia Waziri wa Kilimo ambaye ni mtoto wa matumbaku. Mheshimiwa Bashe siyo kwamba tu anayasikia matumbaku, kaona tumbaku inavyolimwa na alishuhudia jinsi ilivyokuwa tabu wakulima wakivaa ukosi wa shati kwa sababu tumbaku wanayo, wamelima na hawana pa kuiuza. Leo tumbaku imepanda bei kutoka senti 65 ya dola mpaka dola 3.2 kwa soko la leo. Hii ni hatua kubwa sana na mapato makubwa kwa wakulima wangu wa tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikutosha hiyo, Mheshimiwa Rais ametuteulia mtu mmoja muhimu sana. Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Mwambalaswa ambaye alikuwa Mbunge humu ndani kabla ya kutoka kwenye tumbaku amekulia kwenye zao la tumbaku. Matokeo haya chanya yanayotokea yanatokana na malengo ya Mheshimiwa Rais kumteua pia Mheshimiwa Bashe lakini pia kumteua Mheshimiwa Mwambalaswa. Tunampongeza sana sisi wakulima wa Tabora Mheshimiwa Rais kwa mambo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo matatizo ya tumbaku yaliyokuwa yanatukabili miaka iliyopita sisi tumekulia tumbaku, tulipoona inazama tukaona kama nchi hii imetutupa. Imekuwa historia, tunachekelea, lakini pia juhudi kubwa sana imewekwa. Wabunge humu ndani tumepambana sana kutetea zao letu la tumbaku lakini Waziri Bashe amekuja ametetea sana, Serikali Mama Samia imetetea sana, mpaka kuliweka sawa zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mnunuzi mmoja anasema yeye yuko tayari kununua tani 90 za tumbaku, ambazo ni sawa sawa na kilo milioni 90 za tumbaku kwa mwaka yeye pekeyake. Pia anajenga kiwanda cha tumbaku cha kutengeneza sigara hapa Morogoro. Hii ni hatua kubwa sana na hili zao linaingiza fedha nyingi sana. Kama nimesema tunalima kilo hizo nilizozitaja 120 milioni, kwa kila kilo ikiuzwa kwa shilingi dola 3.2 ni mapato mengi ya fedha za kigeni katika zao la mkakati la tumbaku. Tuipongeze sana Serikali kugundua hilo na kuitendea haki tumabku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusemea pia mambo mengine katika kilimo, hasa kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kuendelea na kutoboa au vijana wanasema na kutoka kwa kutegemea kilimo cha kudra za Mwenyezi Mungu cha mvua. Mvua na hali hii ya tabianchi inaanza kunyesha, wakulima wakianza kulima inanyesha katikati ya mazao kutaka kukua, mvua imekatika. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, ameweka fedha nyingi sana kwenye umwagiliaji na ndiYo njia pekee itakayotutoa sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawapati mvua, hakuna mvua kabisa. Wanaishi, wanalima kwa sababu ya kumwagilia. Sisi hapa tuna nchi kubwa sana, tuna maji mengi sana chini, tuna mvua zinanyesha, maji yanapita madarajani. Maji haya yakusanywe kama ambavyo imeonyeshwa katika mradi unaokuja sasa hivi wa kilimo cha umwagiliaji. Tukifanya hatua kubwa mbili tu; moja, kilimo kiwe cha mashamba makubwa na tunakwenda huko, BBT; mashamba ya block farms; lakini yawe mechanized, yawe ya ulimaji na umwagiliaji wa mitambo kwa maji kutoka kwenye mabwawa. Hii ndiyo njia peke yake naiona ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imeiona itatutoa. Hatuwezi kunyamaza Wabunge bila kuipongeza Serikali. Hongera sana Mama Samia, hongera sana Mheshimiwa Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni muhimu sana kukumbuka kwamba kilimo hiki kimebadilishwa sasa kimekuwa cha kibiashara. Kwa hiyo, vijana wanaofundishwa kilimo, watakaolima sasa, licha ya kuwa na kilimo cha kujikimu tu pekee, sasa kitakuwa kilimo cha kibiashara, watu watapata hela mashambani na watapata hela za kula. Hili ni wazo kubwa ambalo tumechelewa kulipata, lakini kwa bahati nzuri, Wizara hii ya Kilimo imechukua suala hili la kilimo cha biashara na kilimo cha mashamba makubwa kuwa mfano katika nchi ya Afrika Mashariki. Hili litatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tupongeze kwamba hela zipo katika bajeti hii ya sasa za kufanya mabadiiliko haya makubwa ambayo tunayasema. Hili likibadilishwa kama tunavyoliona kwenye maandishi haya ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, basi kilimo cha nchi hii kitabadilika na baadaye tutakuwa katika hali ya kujilisha, na pia uchumi wa nchi utakua na kilimo sasa kitachagia kiasi kikubwa katika mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina suala lingine dogo. Wakulima wa tumbaku baada ya kuamka sasa, wana mamilioni ya fedha, wanauliza kwa nini wasilipwe kwa Dola? Wana sababu. Wakulima hawa wanakopesha pembejeo kwa Dola, mabenki yanalipa vyama vya ushirika kwa Dola, lakini vyama vya ushirika vinawalipa wakulima kwa Shilingi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Almas.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kukushukuru sana, lakini naomba sasa vyama vya ushirika viwalipe wananchi, wakulima kwa Dola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.