Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Kilimo. Kwa niaba ya wananchi wa Lupembe na Mkoa wa Njombe kwa ujumla nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa sana ambayo anafanya kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa Waswahili unasema, mzigo mzito mpe Mnyamwezi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, katika Awamu hii ya Sita amempata Mnyamwezi Waziri wa Kilimo, kaubeba huu mzigo. Mheshimiwa Bashe hongera sana, unafanya kazi nzuri, umetoa matumaini kwa Watanzania, na Bunge tunakuunga mkono. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuja kwenye Bunge hili la bajeti, nilikuwa ziara jimboni. Wananchi wa Jimbo la Lupembe kwa upekee walinituma nipeleke salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kuwapelekea mbolea ya ruzuku na wananchi wa Jimbo la Lupembe wameitikia vizuri sana mpango huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe ni kati ya majimbo ya mfano ambapo wananchi wetu wamelima vizuri na kuna mazao ya kutosha. Kama kuna Mbunge hapa kwao hakuna chakula, waje Lupembe chakula kipo kingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, wananchi wa Lupembe pia walinituma kumwambia Mheshimiwa Waziri mambo yafuatayo: Jambo la kwanza, mpango wa mbolea yetu ya ruzuku umekuwa ni mzuri lakini umeibua changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza kubwa ambayo imeibuka na pembejeo za ruzuku ni vituo vya wakala kuwa vichache…
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Enosy kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Almas Maige.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
TAARIFA
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, anayechangia hoja ameongelea ile methali ya kizamani, “Mzigo mzito, mpe Mnyamwezi.” Sisi Wanyamwezi tunapeleka jambo hili kwenye Baraza la Kiswahili ili isemekane “mzigo mzito, punguza, beba mwenyewe.”
MWENYEKITI: Mheshimiwa Enosy taarifa unaipokea.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Bashe, siipokei taarifa hiyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Wananchi wa Lupembe wamepata shida sana kwenye kupata hizi pembejeo. Yako maeneo wananchi wetu walikuwa wanaamka saa tisa mpaka saa kumi, wanakwenda zaidi ya mara mbili hawapati mbolea, kwa sababu zilikuwa chache na vituo ni vichache. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kati ya mambo wananchi wetu wanatamani kusikia ni mpango tulionao kwenye msimu wa kilimo ambao unafuata sasa hivi, Serikali imejipangaje kuongeza mawakala wawe karibu na wakulima wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pamoja na kuongeza wingi wa mawakala, hizi mbolea pia zilikuwa hazipatikani sana, hasa mbolea kama ya Urea na CAN. Wananchi wetu wa Mkoa wa Njombe wameteseka sana. Tungetamani kumsikia Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge na nchi kwa ujumla, watu wa kilimo wamejipangaje kupanua wigo wa kupatikana hizi mbolea kwa wingi na kwa wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wa Lupembe walinituma kulisema kwa Mheshimiwa Rais ni kwamba hizi mbolea za ruzuku kabla ya kuja ruzuku, wananchi wetu sio wote wenye uwezo wa kununua hizi mbolea za kilo 50 kwa Shilingi 70,000/=. Wapo wananchi wengine wamekuwa wakinunua mbolea kwa kupima kwenye kilo na kadhalika. Ushauri wangu kwa Serikali, tunaomba hizi mbolea pia waweke na kilo kama 25 ama 20 ili hata wenye kipato cha chini wamudu kununua hizi mbolea kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, amelisema Waziri kwenye hotuba yake naomba nilirudie. Waziri wetu amekuwa ni sauti halisi ya wakulima wa Tanzania, na amesema hapa kwenye hotuba yake vizuri sana. Anasema, “mazao mengi yamekufa nchini kutokana na kushindwa kuwalinda wakulima.” Nataka nikubaliane na Mheshimiwa Waziri kwamba mazao mengi ya kimkakati yameporomoka na mengine kufa, kwa sababu wakulima wetu walikosa mtu wa kuwasemea na kuwalinda kwenye soko lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wetu maeneo mengi ikiwemo Jimbo la Lupembe wana madai makubwa na wafanyabiashara kwenye mazao yao. Vipo viwanda vingi, wapo wafanyabiashara wanawakopa wakulima, hawawalipi kwa wakati. Jambo hili nitaomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kufunga kwenye bajeti yake atoe tamko la kitaifa juu ya msimamo wa Serikali kwa wafanyabiashara na mawakala wanaowakopa wakulima halafu hawalipi. Wao wanavaa suti, wanabadili magari, lakini wakulima wanaendelea kuwa masikini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Lupembe na Mkoa wa Njombe, yuko mfanyabiashara mmoja wa parachichi anaitwa Olivado, amewakopa wakulima kila mahali. Olivado amekuwa ni tatizo. Zao la parachichi ambalo Mkoa wa Njombe kwa sasa ni zao kubwa sana, lakini wananchi wameanza kukata tamaa kwa sababu wakichuma haya mazao yao hawalipwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, zao kama la parachichi tunaomba Serikali itoe bei elekezi. Wananchi wetu wananunua parachichi, wanauza kwa bei ambazo hazieleweki. Kuna msimu wanauza shilingi 300, kuna msimu shilingi 600, shilingi 1,500 na kadhalika. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa ameanza vizuri, atusaidie kuweka mwelekeo wa Serikali, bei elekezi ya mazao haya muhimu ya wakulima ni nini? Kwa sababu zao la parachichi linachangia sana uchumi na kodi ya nchi yetu kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nataka pia nimwombe Mheshimiwa Waziri, sisi Jimbo la Lupembe na Mkoa wa Njombe, tunayo maeneo mengi, nasi Lupembe tunalo eneo kubwa tumetenga zaidi ya ekari 89,000. Tuko tayari kama Serikali iko tayari, ikafungue kitalu cha mbegu bora kwa ajili ya kilimo. Ardhi ipo, na wakulima wetu wako tayari. Tunaomba utayari wa Serikali tufanye kazi. Nasi Mkoa wa Njombe ni kati ya mikoa ambayo inafanya vizuri sana kwenye kilimo, na ikimpendeza Mheshimiwa Waziri, afanye Mkoa wa Njombe kuwa Mkoa bora wa kilimo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na siyo kwa umuhimu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aendelee kupokea maoni ya Wabunge, tutamsaidia kufika mbali sana kwenye hii Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)