Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa nafasi ya pekee ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu na kuweza kuchangia Wizara ambayo mimi naiita ni uti wa mgongo wa nchi yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kututeulia Mheshimiwa Bashe kuwa kwenye Wizara hii ya kilimo ambayo wananchi wengi, Watanzania wengi wanaitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana kwa kazi kubwa ambayo ameifanya; mawazo yake, amaimarisha wakulima na ushirika kwenye nchi yetu. Mimi niseme tu, mama yetu Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa, ametunukiwa udaktari wa heshima. Mheshimiwa Bashe anastahili na yeye atunukiwe udaktari wa heshima kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo hii wananchi wa Ushetu wamekuwa wakipokea mahindi ya kutosha, hawakuhangaika na njaa, lakini wananchi wa Ushetu ambao ni wakulima wazuri sana wa zao la tumbaku wanafurahia masoko yanavyokimbia kwenye mjengeko wetu wa bei. Ukiangalia madaraja ambapo L10F ambayo ilikuwa inauzwa dola 2.9 leo chini ya utawala wa Mheshimiwa Rais na Waziri wetu Bashe ni dola 3.200, wananchi wanachekelea. L10 ambayo ilikuwa ni dola 2.2, leo ina dola 3.1. L1L ambayo ilikuwa ni 2.9 leo ina dola 3.70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna daraja moja ambalo lilikuwa linapewa dola 0.9 lakini chini ya Utawala wa Mheshimiwa Rais, Comrade Mheshimiwa Bashe na Naibu wake, leo lina dola 3.039. Ni pongezi kubwa kwenye Wizara ya Kilimo na kwa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi kwa Mheshimiwa Waziri, kwenye hotuba yako umesema Serikali imejipanga kutoa ruzuku ya mbolea kwa mazao yote nchini. Sasa wakulima wa tumbaku wanalalamika, hawapo kwenye ruzuku ya mbolea, hawajapata kwenye ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima tu kwa msimu huu, mbolea zilizoenda kwa wakulima ni mifuko 802,000 ambapo kwa bei waliyouziwa ni 166,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50. Sasa tumeombe Mheshimiwa Waziri kama wangeuza kwa shilingi wangelipa kwa shilingi 70,000 inamaana wakulima wangebakiwa na bilioni 77 ambazo zingeenda kuwajengea maisha yao, wangeenda kufanya shughuli zao nyingi za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu uchapakazi wako ni mzuri ebu naomba hili muwafikilie hawa wakulima, wakulima hawa wametumia mbolea nyingi, wamechukua fedha nyingi kwenye mabenki ni zaidi ya bilioni 99 zimetumika kwenye kuwapelekea wakulima mbolea. Sasa wasipopata ruzuku pamoja na bei nzuri ya tumbaku bado tutakuwa hatujawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana ndugu yangu na mimi term hii nitajipanga kushika shilingi tusipopata tamko la kuhusu mbolea za ruzuku. Niendelee kukuomba Mheshimiwa Waziri unapokuja na hili njoo wakulima hawa wa tumbaku nini hatma yao kuhusu ruzuku ya mbolea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala jingine ni suala la tija kwenye uzalishaji. Tumekuwa tukishuhudia bajeti inaenda fedha nyingi kwenye eneo la kilimo lakini hatushuhudii nani anaenda kukagua uzalishaji wa tija kwenye mazao yetu. Tuangalie tu, tumekuwa wakaguzi wazuri wa miradi unaona Waziri ameenda kukagua barabara mpaka wakati mwingine wanaenda na nyundo kubomoa zile barabara kwamba haijajengwa vizuri. Tumeona viongozi wanaenda kukagua majengo lakini hatujaona wameenda kukagua uzalishaji wa tija kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie tunajiwekea mikakati kwamba labda zao la pamba tutazalisha kutoka kilo 200 kwa heka moja, tunaenda kilo 800 je, tunapoenda kufunga msimu uzalishaji umefikiwa? Angalia kwenye korosho nchi zote zilizojifunza mazao kwetu nchi ya Vietnam pamoja Ivory Coast wamejifunza uzalishaji kwenye nchi yetu ya Tanzania lakini angalieni wenzetu sasa hivi uzalishaji wao uko juu. Angalia Misri pamoja na Algeria kwenye pamba wanazalisha kilo moja kwa heka moja 800 mpaka 1,500. Uturuki ndiyo inaongoza ambayo ina kilo 1,500 kwa heka moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pamoja na nguvu zote tunazozitumia bado tuko kwenye uzalishaji wa eka moja kilo 200, bado tuko chini. Tutapeleka fedha nyingi, tutapeleka fedha za kutosha lakini bado tutahitaji wakulima hawa wakaelimishwe namna bora lakini usimamizi uwe mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wakuu wetu wa Mikoa tuwatumie vizuri Mheshimiwa Waziri nikuombe ebu tenga fungu wakabidhi kazi wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya ma-RC wako kule, ma–DC wako kule waende wakasimamie uzalishaji wa tija kwenye nchi yetu. Wakulima wetu walime kidogo wazalishe kwa wingi kwa sababu sasa hivi wanalima eneo kubwa lakini uzalishaji unakuwa ni changamoto. Kwa hiyo, nikuombe kwamba tunapoenda kwenye uzalishaji sasa hivi kuingia kwenye uzalishaji twende tukazalishe kwa tija tuwasaidie wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri, kwa upande wa wakulima wetu wa tumbaku kwa mwaka huu wana uwezo wa kupata zaidi ya dola milioni 350. Kwa sababu ya soko zuri la tumbaku kama alivyosema Mheshimiwa Almas Maige, ni kazi nzuri ambayo imefanywa. Mheshimiwa Waziri, kazi nzuri ambayo amefanya Mheshimiwa Rais milioni 350 wanazipata wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi inayosimamia zao hili halina fedha ni Mkurugenzi pekee ambaye zao lake linalouzwa kwa dola hana gari ya kutembelea. Lakini watumishi mishahara inayolipwa iko chini na wanaenda kuwasimami wanunuzi, makampuni ambayo mishahara yao ni minono sasa mwisho wa siku tunawashawishi kuingia kwenye vishawishi vingine nikuombe Mheshimiwa Waziri, liangalie hili Bodi ya Tumbaku hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Tumbaku sasa kwenye masoko wanatumia gari moja na vyama vya ushirika. Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku asingekaa na wakulima wakaamua kutoa magari kuisaidia bodi leo hii. Kwenye masoko angeendelea mkurugenzi wa bodi, wanunuzi wake na classifier wanakuwa gari moja na wanunuzi wa wanaoenda kuadhibu wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuomba Mheshiiwa Waziri hii bodi iangalieni kwa macho mawili, mkisubiri mpaka ichangiwe shilingi 30 kutoka kwa wakulima mtatengeneza mgogoro mwingine. Kwa muda huu nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu ukiangalia bajeti unayotengewa na Mheshimiwa Rais ni kubwa sana nenda kaingalie Bodi ya Tumbaku namna nzuri ambayo utaweza kuisaidia ili inapoenda kusimamia masoko vijana hawa wanapoenda kupambana uzalishaji kama Serikali wakulima tu wanaingiza tu milioni 300 za dola? Nchi inapata shilingi ngapi kama mapato? Ukiangalia halmashauri zetu zinapata bilioni 17 kama halmashauri ushuru lakini sasa hawa wanaosimamia hili zao wana hali gari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho mimi kwa sababu leo nampongeza tu Mheshimiwa Waziri, vyama vya ushiriki. Nimpongeze sana Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amefanya kazi nzuri. Sasa tunaenda vyama sita vikanunue pamba ningekuomba Mheshimiwa Waziri Simiyu, Nyanza naomba hawa pamoja na Shileku waingizeni kwenye mfumo wa kununua pamba. Tunataka competition iwe kubwa kwa wakulima wetu ushindani uwe mkubwa wakaende kuhudumia wakulima wetu kwa sababu bila vyama vya ushirika, bila muungano hivi hatuwezi angalia Nchi ya Kenya Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wamekuja kujifunzia pia ushirika kwetu kwenye upande wa mikopo lakini angalia leo benki kubwa ambayo iko Kenya ni benki ya ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningekuomba Mheshimiwa Waziri, haya yanaangalie kwa mapana sana haswa suala la tija, tuongeze tija tuondokane, sasa kilo kwa kuzalisha eka moja kilo 200 basi twende kwenye kilo 800 mpaka 1,500 mkulima analima kidogo eneo dogo anazalisha kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, ninaunga mkono hoja lakini suala la ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa tumbaku hili ndilo linanifanya leo nikamate shilingi ya Waziri. (Makofi)