Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia. Niungane na wenzangu kwa kumpongeza sana Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kazi nzuri anayofanya lakini hasa hasa msimamo wake thabiti kabisa kuhusu bei ya mazao ya wakulima ili wasipunjwe wauze kwa tija. Mheshimiwa Waziri ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Anthony Mavunde, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kazi wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye item namba 33 ukurasa wa 14 kwenye Hotuba ya Waziri, Kuhusu Kilimo cha Umwagiliaji kama walivyosema wenzangu kwa sasa hivi ndiyo jawabu la kudumu kwa mapinduzi ya kilimo Tanzania kama ambavyo tuliazimia Bunge hili la kumi na mbili kwamba tuhakikishe kuna kuwa na mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Tume ya Umwagiliaji ya Taifa kwa mipango mizuri, ambayo kwakweli inaainishwa vizuri sana kwenye randama yao, tatizo pale ninaloliona ni bajeti. Kwa mfano walitengewa bajeti ya shilingi bilioni 257.5 kwa mwaka uliyopita, lakini mpaka mwezi Februari ni shilingi bilioni 46 tu ndiyo zimeweza kutolewa sawa na asilimia 18. Sasa hii ni fedha kidogo sana kwa mipango mikubwa waliyonayo ya umwagiliaji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekit, tuchukulie Mbarali tuna mabonde makubwa mazuri katika Milima ya Ulanji ambayo kama Serikali itatengeneza mabwawa na naamini katika mabwawa 22 ambayo yamefanyiwa utafiti. Naamini mabwawa sita yanatoka Mbarali sasa kama tutakuwa na mabwawa hayo sita nina uhakika kilimo cha umwagiliaji Mbarali kitastawi sana na nishukuru Serikali imeashaanza ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji Mbarali sasa tukijengewa na mabwawa nina hakika kilimo kitakuwa bora sana na tutalisha nchi hii mchele bila wasi wasi wote na tutauza nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mbarali shida kubwa tuliyonayo ni mashamba, mashamba kwakweli ni haba sana. Kwa mujibu wa sensa, wananchi Mbarali sasa hivi tumefikia takribani 446,336 karibu laki nne na nusu kutoka laki tatu lakini mashamba ni yale yale. Sasa mashamba yakipungua maana yake nguvu kazi tutaipoteza, wananchi hao wameongezeka sana, mashamba yanapunguzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali hebu iangalie kwa jicho la uhuruma Mbarali, Mbarali tunahitaji tujengewe mabwawa ili wananchi wale waendelee na kulima yale mashamba, maji yawe yanapitiliza yanaenda Mtera yanaenda Bwawa la Mwalimu Nyerere bila wasi wasi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la mabadiliko ya tabianchi kwakweli ni global si Mbarali tu tunaosababisha kama walivyosema wenzangu na nchi jirani zinachangia na pengine ulimwengu kwa ujumla. Tulitembelea na Kamati TMA pale Mamlaka ya Hali ya Hewa Dar es salaam, naipongeza Serikali imewekeza mitambo mikubwa sana yenye kiwango cha kimataifa na accuracy yake kwakweli ni nzuri sana na watalamu wale wana weredi wa hali ya juu, wana mawasiliano na nchi mbali mbali ulimwenguni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wametupa mfano kwamba sasa hivi wanachopata tabu sana ni sura ya mabadiliko ya tabianchi inakuja kivingine tofauti na tulivyo zoea nyuma kuona mvua zinakuwa haba, zinachelewa kunyesha, zinaondoka mapema lakini sasa zinanyesha kwa wingi lakini kwa kipindi kifupi walitupa mfano tarehe 12 mwezi wa kwanza juzi 2021 Mtwara waliweza kupima kiwango cha milimita 369.7 wakati wastani huwa ni milimita 133. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa muktadha huo, utaona kwamba kumbe sasa hivi tuelekeze nguvu kubwa kwenye mabwawa fedha nyingi zipelekwe kwenye Tume ya Umwagiliaji waweze kujengwa mabwawa ili tuwe na maji ya kutosha ndipo sasa tuweze kupanda miti istawi turudishie uhalisia. Lakini tukiendelea kupanda miti huku mvua za wasiwasi miti yenyewe inakauka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijaribu kupanda Mbarali mikorosho, mikorosho ilikauka kutokana na mvua haba na maji hakuna. Kumbe kukiwa na maji ya kutosha na wananchi hawa wataendelea kulima huku tunapanda miti, tunamwagilia na maji haya bila shaka tutapata majibu chanya kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti na nisisitize Serikali, kwamba sisi Mbarali tuko tayari kupokea maelekezo ya Serikali, na huku wanavyojipanga kuweka MKUZA, kutathmini maeneo, nani walipwe fidia kiasi gani, tunaomba Serikali iruhusu wananchi hawa wa Mbarali waendelee kuyatumia mashamba haya wakati Serikali inaendela kujipanga. Kwa maoni yangu nadhani mabwawa ni kipaumbele namba moja, hebu mambo mengine yasimame, tuboreshe haya mabwawa ili tupate tija kwa kilimo cha mbarali na maji kwa ujumla, yanayoenda Bwawa la Nyerere na Mtera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee kidogo ugonjwa wa mnyauko uliotokea Mbarali kuhusu mpunga. Nashukuru wataalamu wa TARI wamefanya utafiti na wanaendela kutoa elimu kwa wakulima. Lakini niombe wataalamu hao wafanye mambo mawili; moja, ni kutathmini mbolea tunayoitumia kwa sasa. Nashukuru mbolea ya ruzuku wananchi wamenunua kwa bei nafuu na wameitumia kwa wingi, lakini sehemu ile waliyoweka mbolea kwa kweli kwanza ndio iliyoathirika zaidi kuliko mashamba ambayo hayakuwekwa mbolea kabisa au yaliwekwa mbolea kidogo. Wafanyie utafiti hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niombe wafanye utafiti wa dawa ambayo inatibu, kama ni dawa ya ukungu au kama ni dawa gani ambayo itatibu ugonjwa huu kwa haraka kwa sababu unaathiri kipato cha wakulima Mbarali. Nirudie kusisitiza kwamba kwa kweli Mbarali tumeongezeka tumekuwa watu wengi sana, tuna shida ya mashamba; hivyo basi niombe Serikali itujengee mabwawa kwa kuanzia yawe sita, kama Bwawa la Mtera, ili tuendelee kulima bila wasiwasi wowote na maji yaende mabwawa ya Mtera na Nyerere. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)