Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi niungane na wabunge wenzangu kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa anaoendela kuufanya kwenye sekta ya kilimo. Lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri Pamoja na Katibu Mkuu kwa ushirikiano ambao wananipa mimi pamoja na wananchi wa Kilolo katika miradi mbalimbali. Yapo mambo mengi ambayo tumeshirikiana na Wizara ya kilimo, lakini nishukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa uungwana wake, kwamba ameungana na sisi katika ufufuaji wa zao la chai katika Wilaya ya Kilolo, na kwamba Wizara yake itaenda kuweka historia ya kukuza uzalishaji wa chai kupitia Wilaya ya Kilolo. Napenda kumshukuru sana, kwa sababu hata ninavyozungumza hivi sasa kazi inaendela ya kufyeka mashamba pia na kazi mbalimbali kuhakikisha kwamba Kilolo na yenyewe chai sasa inafufuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo napenda kushukuru ni uanzishwaji wa kitalu cha miche ya parachichi. Jambo hili nililizungumza kwenye bajeti iliyopita na limefanyika kwa umakini mkubwa. Hivi ninavyozungumza TARI wameanzisha kitalu pale na nina hakika kwamba msimu ujao tutapanda miche kutoka TARI. Ombi langu dogo ni kwamba bei ya miche ile iangaliwe au kama ilivyo kwa mazao mengine wakulima hasa wale walio masikini wapewe miche ile 20 bure watunze vizuri ili waje wavune kwa sababu kuna mazao mengine pia wananchi wanapewa miche bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo ningependa kushukuru ni ile scheme ya Ruaha Mbuyuni, kwamba baada tu ya kupata madhara, majanga ya scheme ile umetusikiliza, umetuma wataalamu kufanya tathmini na hivi tunavyozungumza tathmini imeshafanyika na mimi kwa niaba ya watu wa Kata ya Ruaha Mbuyuni nitoe shukrani za dhati kwa mwitikio wa haraka. Lakini nitoe ombi kata ya Ruaha Mbuyuni Pamoja na Kata ya Mahenge ni kata ambazo ziko maeneo makavu sana. Hivi tunavyozungumza ile sehemu ambayo ilikuwa imwagiliwe kwa scheme ile maana yake mazao yanaendela kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafahamu kwamba suluhisho la pale ni lazima kuwe na mpango wa muda mrefu; lakini kama kuna uwezekano wa kuwa na mpango mdogo wa muda mfupi wa kuokoa mazao wakati ule mpango wa muda mrefu unaendelea nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, pale Ruaha Mbuyuni iangaliwe ili wananchi wasipoteze mazao. Hasara itakayopatikana kutokana na mazao kuharibika kwa scheme ile ni kubwa kuliko fedha tunayoweza kuwekeza ili angalau maji yaende kumwagilia wakati tunaendelea na zoezi la mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, ninapozungumzia scheme za umwagiliaji, Tarafa ya Mahenge ina scheme tatu lakini zote ziko kwenye hatua mbalimbali hamna iliyokamilika. Scheme ya Mgambalenga ilianza kujengwa miaka mingi kweli wakandarasi wako site lakini haijakamilika. Scheme ya Nyanzwa tuliiomba huu ni mwaka wa tatu iko kwenye usanifu sasa hivi ndio imewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya usanifu wa kina. Sasa mimi niombe sana, kwa sababu usanifu ulifanyika kwenye mwaka huu wa bajeti unaoisha kama inawezekana Scheme ya Nyanzwa iwekwe kwenye bajeti ianze kujengwa lakini sasa Scheme ya Ruaha Mbuyuni nayo hii iko kwenye changamoto. Kwa maana hiyo tarafa yote scheme zote hamna inayofanya kazi, na ni sehemu kavu. Kwa hiyo kama tukiacha vile maana yake ni kwamba tutakuwa kwenye changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, hasa Scheme ya Ruaha Mbuyuni angalau ifanye kazi wakati tunasubiri hizi nyingine; na hizi nyingine ziangaliwe kwa sababu eneo lile ni kavu na tusipomwagilia maana yake kilimo katika eneo lile hakutakuwa na namna kinaweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja ambalo ningependa kushauri kuhusu kilimo, hasa kilimo cha mahindi. Kumejitokeza fursa nyingine katika maeneo ambayo tunalima mahindi. Fursa ya wafugaji wakubwa kununua mahindi kwa ajili ya chakula cha mifugo. Sasa changamoto iliyopo ni kwamba wakulima hawa hawakuandaliwa kulima mahindi kwa ajili ya chakula cha mifugo. Walilima mahindi kwa ajili ya chakula chao, inapofika mahindi yamekomaa lakini hayajakauka wale wakulima wanashawishiwa kuuza yale mahindi na bei yake inakuwa kubwa kuliko akivuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakachokipata ni kwamba hata nyinyi takwimu zenu mnaposema tunatarajia kuvuna mahindi kiasi fulani hamjazingatia hilo kwamba kuna mahindi mengine ni kwa ajili ya mifugo. Sasa tunaweza kuja kupata changamoto ya njaa kwa sababu hii fursa wakulima hawakuandaliwa vizuri kujulishwa kwamba walime mashamba ya chakula lakini pia kuna fursa ya mazao kwa ajili ya chakula cha mifugo na pengine hata aina za mbegu zingekuwa tofauti; mbegu ya chakula cha mifugo na mbegu ya chakula cha binadamu. Mimi hii fursa naiona lakini nadhani Wizara ni vizuri ikaielezea vizuri kwa wakulima ili tusije tukaleta changamoto ya njaa kwa sababu hivi tunavyozungumza ni muda mahindi ni mabichi na uvunaji wa mahindi kwa ajili ya chakula cha mifugo ni mkubwa bila kuzingatia wale wakulima walilima kwa ajili ya nini; na wakati utapofika wa kuvuna tunaweza tukajikuta tunaingia kwenye changamoto ya njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni kuhusu udhibiti wa ujazo. Nishukuru kidogo sasa hivi wakala wa mizani wanajitahidi, lakini mara nyingi tumesimama hapa na kuzungumza kuhusu namna gani mazao ya mbogamboga yanavyoteseka kwenye bei, na mazao haya ni yaleyale ambayo yanalimwa, ndiyo ambayo bei zake hazina bei elekezi na wakulima wakati wote wanateseka na ujazo wake haujulikani vizuri. Mazao ya nyanya, viazi, vitunguu, njegere, karoti pilipili hoho, ndiyo mazao ambayo yanalimwa sana kwa mfano kwenye maeneo ya Kilolo; lakini wakati wote wakala wa mizani bado hawajaja na suluhisho la kuhakikisha kwamba sawa wanapambana na lumbesa lakini bei zinabaki zikiwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wamepambana kupunguza ujazo, lakini sasa wakipunguza kunakuwa na bei ya lumbesa na bei ambayo ule ujazo uko flat. Sasa mimi ningeshauri kwamba kuwe na utaratibu mzuri wa kuendelea kudhibiti bei na pia kudhibiti ujazo. Hili linawezekana kama mazao haya yatauzwa kwa kilo. Kwamba kilo moja ni shilingi kadhaa, kilo 10 ni shilingi kadhaa badala ya kuzingatia kifungashio kama ndicho kinachoamua bei ya mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu miundombinu hasa kwenye miradi ambayo inatekelezwa, na hapa niende moja kwa moja kwenye kushukuru sana hii mradi wa Agri-connect ambao umekuwa ukisaidia sana kutengeneza miundombinu kwenye maeneo ya kilimo, hasa barabara. Na ujenzi huu Mheshimiwa Waziri unajua mara nyingi umekuwa ujenzi wa barabara za lami. Sasa barabara ya lami inaweza ikawa kilomita 18 au 20, lakini barabara za kuingia sasa kwenda ndani kwenye yale mashamba zinabaki zikiwa hazijalimwa. Lakini pia semina na workshops ni nyingi sana kwenye miradi hii. Mimi nikuombe sana, bajeti ziende kwenye ujenzi wa miundombinu na si semina na warsha, kwa sababu Watanzania wameshaelimika, wanataka miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.