Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya kilimo. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kufika siku hii ya leo, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoiongeza bajeti ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru na niwapongeze Mawaziri, Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Mavunde pamoja na watendaji wote ambao wanaifanya kazi ambayo Watanzania wote wanaiona, kazi inayofanyika katika Wizara hii ya Kilimo. Mimi nitachangia kuhusu zao la parachichi Mkoani Kilimanjaro, nitachangia kuhusu umwagiliaji wa zao la mpunga na nitachangia kuhusu Benki ya Wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na zao la parachichi Mkoani Kilimanjaro. Sisi Wanakilimanjaro tunaona wivu wa kilimo wa zao la parachichi. Zao la parachichi aina ya Has ni zao ambalo sasa hivi linawika sana, linauzwa nje ya nchi, linaingiza kipato kwa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, lakini zao hili kule kwetu bado kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vikundi ambavyo vinazalisha mbegu ya has, lakini vikundi hivi pamoja na kuzalisha mbegu hiyo, bado bei yake ni kubwa sana, bei ya mche mmoja inaanza kuanzia Sh.6,000/=, Sh.5,000/=, ukiomba sana Sh.4,000/=. Kwa mwananchi wa kawaida wa hali ya chini kutoa Sh.6,000/= au Sh.5,000/= au 4,000/= kununua mche mmoja kwa kweli ni mtihani mkubwa. Tuiombe Serikali sasa itoe ruzuku kwa vile vikundi ambavyo vinazalisha miche ili viweze kuzalisha kwa wingi, ili pia viweze kuuzia wananchi kwa bei nzuri ambayo zao hili litalimwa kwa wingi sana na litawaingizia kipato na kukuza uchumi kwa mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea kuhusu zao la parachichi, nitaongelea kuhusu zao la mpunga. Katika Mkoa wa Kilimanjaro tuna mabonde mengi sana, tuna mabonde ambayo yanafaa kilimo cha mpunga na tuna mabonde ambayo pia hayo hayo yanafaa kilimo cha vitunguu, lakini hatuna skimu za umwagiliaji za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilimanjaro ni wakulima wazuri sana wa wa mpunga na kama tunavyotambua kwamba, kilimo cha mpunga ni kilimo ambacho ni cha chakula pamoja na biashara. Kwa maana hiyo, basi, tunaiomba Serikali kule ambapo tunayo mabonde mengi ambayo hayana skimu, Serikali isaidie kujenga skimu za umwagiliaji, ili kukuza kilimo cha mpunga katika Mkoa wa Kilimanjaro. Hii itasaidia wananchi mmoja mmoja kuongeza kipato na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwenye suala la Benki ya Kilimo. Ni ukweli usiopingika kwamba, unaposema kilimo ni vijijini, lakini benki hizi ziko maeneo ya mjini. Wakulima wengi wanatamani sana kukopa, lakini je, wanafikaje mjini? Kuna mkulima ambaye anakaa kule Gonja Maore hajui Makao Makuu ya Mkoa, Moshi. Kuna mkulima anakaa kule Mamba Juu hajui Makao Makuu ya Wilaya, Same. Huyu mkulima ambaye ndiye mkulima anayetarajiwa alime ili auze, je, anaifikiaje hii benki? Naiomba Serikali hii sikivu, iangalie sana suala hili la kuwapelekea huduma kwa karibu walengwa wa kilimo kwa maana ya wakulima katika maeneo yao, ili waweze kulima na kuuza mazao yao katika masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, niongelee suala la masoko. Ni ukweli kwamba, wakulima wanajitahidi sana kulima, lakini hapo katikati kuna masuala ambayo yanajitokeza katika kutafuta masoko. Wanaofaidi nguvu za wakulima ni madalali. Mkulima atachukua muda mrefu wa kulima mpaka kuvuna, lakini dalali atakuja atanunua gunia la mpunga au la tangawizi au la mahindi kwa bei ndogo sana na akienda kuuza zao hilo atapata faida zaidi ya mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iangalie sana. Kama ambavyo tumeongeza bajeti ya kilimo, lakini pia tuangalie suala la masoko ili tuweze kumkomboa mwananchi au mkulima huyu katika suala zima la kuuza mazao yake. Pia tuangalie suala la lumbesa, lumbesa kila mtu anaisema. Wafanyabiashara wanafaidika, wakulima wanaumia. Ifike mahali sasa Serikali itoe tamko kwamba, mizani ipelekwe katika maeneo ya kuuza na kilo ya gunia moja, kama inavyofahamika, kilo 100, ndio kilo halali ya zao la aina yoyote. Masuala ya lumbesa tuhakikishe kwamba, sisi tunayakomesha ili kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kuuza mazao yao kwa bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo, naomba pia niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kupeleka miradi katika Mkoa wa Kilimanjaro. Serikali imepeleka miradi katika wilaya mbalimbali katika Mkoa wa Kilimanjaro ikiwepo Same, Mamba Miamba, ikiwepo Kalemawe, Wilaya ya Same, Manispaa ya, I mean Moshi DC…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zuena, muda wako umeisha, unga mkono hoja.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja naipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya katika Wizara ya Kilimo. Ahsante sana. (Makofi)