Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nakupongeza pia kwa kukalia hicho Kiti umeweza kutupa nafasi Wabunge wengi kuweza kuchangia katika hotuba hii. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Bashe kwa hotuba yake nzuri na hili halitoki kwangu tu, nimpokea SMS nyingi kwenye simu yangu hapa zikikupongeza Mheshimiwa Bashe kwa hotuba nzuri na mimi kwa kweli ningependa nisome message moja inatoka kwa ndugu yangu anaitwa Daudi Mpindasigulu wa Chabutwa anasema na mimi na nukuu kama alivyo andika. “Mheshimiwa, nifikishie salamu kwa Mheshimiwa Hussein Mbashe, ameandika tu Hussein Mbashe, Waziri wa Kilimo kupitia hotuba yake nzuli.” Sisi hatuna “R” kwa hiyo anasema nzuli. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa dondoo kwenye hotuba ya Waziri ambazo zimewafurahisha wananchi wa Sikonge ni ukurasa wa 135 Ibara ya 306 pale aliposema katika mwaka 2023/2024 Wizara imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji lenye jumla ya hekta 256,185.46 kwa kukarabati na kujenga skimu za umwagiliaji na kule Sikonge kwenye jedwali ameonyesha Skimu ya Umwagiliaji ya Ulyanyama, Skimu ya Kalupale na Skimu ya Usunga. Hii kwa kweli wamefurahi sana wananchi wa Sikonge na wanapongeza, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napongeza uteuzi wa Mheshimiwa Victor Mwambalaswa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku. Huyu alikuwa hapa Bungeni na wakati alivyokuwa Bungeni alikuwa Mwenyekiti wetu Wabunge tunaotoka kwenye maeneo wanayolima tumbaku. Kwa hiyo, hii mmelenga vizuri sana na ninawapongezeni sana hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zingine nampa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake mazuri kwa nchi hii na huruma yake kwa Watanzania jinsi anavyowaongoza na ndiyo maana ameongeza bajeti ya Kilimo kwa mwaka wa pili mfululizo kwa mabilioni. Kwa hiyo hongera sana. Pia nampongeza kwa ruzuku ya mbolea ambayo aliitoa mwaka jana ambayo ilipunguza bei kwa nusu kwa mazao ya chakula lakini vilevile kwa mahindi ambayo aliyatoa kwa ajili ya kukabiliana na mfumuko wa bei. Hizo ni hatua ambazo kwa kweli zilikuwa ni nzuri zenye faida kubwa sana kwa Taifa hili. Sikonge tulipata tani 764.7 ambazo zilipunguza bei kutoka shilingi 23,000 kwa debe mpaka shilingi 16,800. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa ni hatua nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kulikuwa na changamoto ambayo ningependa Mheshimiwa Waziri ai- note, kulikuwa na changamoto kwenye hatua hiyo nzuri, kwamba mbolea pamoja na mahindi yale ya kukabiliana na mfumuko wa bei, yalifika katika Makao Makuu ya Wilaya hayakufika kwenye Kata nyingi za mbali. Kwa hiyo, watu wa Kata za mbali kama Tarafa ya Kiwele iliwawia vigumu kuja Sikonge kupata huo msaada kwa sababu ya gharama za usafiri. Kwa hiyo, iatakapokuja msimu ujao ninaomba Wizara ya Kilimo ishirikiane na Halmashauri yetu ya Wilaya ya Sikonge kuhakikisha kwamba misaada kama hiyo ya Serikali inawafikia wananchi wengi kule ambako wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza kuna madeni ya wakulima wa tumbaku. Hili Mheshimiwa Waziri anafahamu vizuri haya madeni, msimu wa mwaka 2020/2021 kuna makampuni ya wazawa yalipewa kibali na Serikali kununua tumbaku. Kwetu Sikonge tumeathirika nadhani kuliko Wilaya yoyote nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sikonge kampuni inayoitwa PCL inadaiwa na wakulima dola 476,995.78. Kampuni ya NAILE inadaiwa na wakulima dola 218,510.66, Kampuni ya EMV inadaiwa na wakulima dola 90,772.42. Hizi ni dola 786,278.86. Hizi ni hela nyingi karibu shilingi bilioni mbili wanadai wakulima. Huu ni mwaka naona tunaingia mwaka wa tatu wakulima hawajapata jasho lao. Halmashauri inadai ushuru wa shilingi milioni 156. Kwa hiyo, naomba kwa sababu deni hili alipokuja Mheshimiwa Rais mwaka jana tarehe 18 mwezi wa Mei, kuzindua barabara ya Tabora - Mpanda, Mheshimiwa Rais alisimama akayataja haya madeni kwamba nimemuagiza Waziri wa Kilimo ayashughulikie. Sasa kama mpaka leo hayajashughulikiwa, wakulima hawajalipwa, hivi wakulima hawa wakimbilie wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, shilingi bilioni mbili ni fedha ndogo sana, Serikali ilipe shilingi bilioni mbili halafu yenyewe ndiyo ijue namna ya kubanana na hayo makampuni. Mimi nilikuwa naomba sana hatua hiyo ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, kuna ushuru wa kuni umeanzishwa kule na wenzetu wa maliasili kule Sikonge. Kila mkokoteni wa kuni ya kukaushia tumbaku watu wa maliasili wanachaji shilingi 6,000 na hii wataanza msimu ujao. Ni kilio kikubwa sana cha wakulima maana yake inakwenda kuongeza gharama za kuzalisha tumbaku na inakwenda kuchukua sehemu kubwa ya mapato ya mkulima. Nilikuwa naomba kwa sababu mkulima analazimishwa kupanda miti kabla hajalima. Mwaka jana msimu uliopita walipanda miti milioni mbili. Sasa kama mtu amepanda miti milioni mbili, kwa nini wewe mtu wa maliasili unakuja unamchaji tena kuni? Mimi nilikuwa naomba Serikali itoe msimamo kupitia Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe kwamba hiyo ushuru huo usimame kwanza mpaka hapo tutakapokuja kukaa vizuri tuweze kuelewana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naungana na wenzangu kudai haki ya wakulima wa tumbaku nao kupata ruzuku ya mbolea. Mwaka jana hawakupata ruzuku ya mbolea. Mbolea ile ya tumbaku ilipitia kwenye Vyama vya Ushirika moja kwa moja ikaja, wakulima wakachajiwa shilingi mpaka 160,000 kwa mfuko wa kilo 50. Mimi nilikuwa naomba sana kwamba nao wapate mbolea ya ruzuku wanajisikia kama vile wamebaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naomba Serikali iweke ruzuku kwenye bei ya mbegu za mahindi. Haiwezekani mbegu ya mahindi kilo mbili inauzwa shilingi 12,000 wakati ambapo debe la mahindi linauzwa shilingi 5,000 wakati wa mavuno. Sasa hiyo hakuna correlation. Naomba sana Serikali ifikirie na kukubali kuweka ruzuku kwenye mbegu ya mahindi ili kuongeza uzalishaji ambao tunautegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo tu. Nashukuru sana hotuba nzuri, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)