Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa nafasi hii ambayo umenipa. Kabla sijanza kuchangia nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu hii hoja ni hoja kubwa, Wizara ambayo inashika wananchi wote wa kawaida na tumekuwa tukisema kilimo ni uti wa mgongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe, naomba nianze kwa masikitiko kuonesha kwamba mimi msimu wa kilimo uliopita kwenye Wilaya ya Uvinza, Jimbo la Kigoma Kusini sikupata mbolea kabisa. Mheshimiwa Bashe tulikutana pale airport Dodoma nikakueleza jambo hili, ulinifahamisha kwamba mbolea ilikwenda pale Nguruka lakini baadae mbolea ile iliondolewa, ni kweli nilifuatilia mbolea ile iliondolewa. Sababu ya kuondolewa mimi sikuwa naijua, kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Bashe kwa kweli msimu huu wa kilimo naomba unikumbuke Wilaya ya Uvinza kwa sababu ni Wilaya ambayo kwa kweli inajishughulisha kwa kilimo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto iliyopo ya mifugo kwa sababu mifugo inapingana na kilimo, wenzetu wale wa mifugo hata mahindi, hata muhogo, chochote kinacholimwa na binadamu wao wanasema ni majani pia, kwa hiyo wanafyeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilete masikitiko yangu kwa mara ya kwanza, nadhani kwenye Wilaya zote msimu uliopita nimepata njaa kwa sababu debe la mahindi lilifika shilingi 30,000. Nilimuona Naibu Waziri kujaribu kuona na mimi nipelekewe mahindi kwenye Wilaya yangu lakini masharti aliyonipa ni kwamba Mkuu wa Wilaya aandike barua. Ni kweli Mkuu wa Wilaya nilimwambia aandike barua lakini sijui kama barua iliandikwa na ikaja. Kwa sababu tatizo ni kwamba Mkoa wa Kigoma ni Mkoa ambao haujawahi kuingia kwenye njaa tangu tumepata uhuru. Sasa nadhani Serikali walipata kigugumizi kuandika barua kwamba Mkoa wa Kigoma una njaa, kwa maana ya Wilaya ya Uvinza, lakini wananchi wangu kwa kweli walipata shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu ruzuku ya mbolea ya tumbaku. Wenzangu wamezungumza sana, tumbaku ni kilimo. Kwa nini tumbaku isiwekewe na yenyewe mfumo wa kupata ruzuku ya mbolea, kwa sababu ni kilimo. Naomba sana kwenye jambo hili kwa sababu Wilaya yangu pale Nguruka wanalima sana kilimo cha tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri lingine ni kwenye eneo la mbegu ya mchikichi. Mheshimiwa Waziri Mkuu amepambana kuhakikisha kwamba Mkoa wa Kigoma unakuwa miongoni mwa mikoa ambayo inazalisha chikichi kwa wingi kwa sababu kwa kweli kimsingi ndiyo Mkoa ambao una historia na chikichi, kwa bahati mbaya sana pamoja na juhudi za Serikali mbegu hizi bado. Kwa sababu mimi mwaka jana niliomba miche 7,500 kwa sababu mimi nina shamba la ekari 200, kwa kuzingatia kwamba ekari moja ni miche 58, niliomba nipatiwe 7,500 sikupata, niliambulia miche 1,000, unaweza kuona kwamba bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili Mheshimiwa Bashe lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba chikichi pamoja na alizeti yanakuwa ni mazao ambayo ni mkombozi ili tuweze kupata mafuta sisi wenyewe wananchi kwa maana ya nchi yetu ili tupunguze fedha ambayo inatumika kuagiza mafuta nje, bado Mheshimiwa Bashe wananchi hawa ni kweli wana vishamba vidogovidogo, nakuomba sana. Mpango wa kuhakikisha unapata wawekezaji kwa ajili ya zao hili kama ambavyo Serikali imekuwa ikihakikisha inashawishi wawekezaji kuweza kuchukua maeneo kwa ajili ya kilimo cha miwa ili tuweze kupata sukari na kwenye eneo hili naomba sana Mheshimiwa Bashe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi tukiwategemea sana uwezo wao ni mdogo. Utawapa miche lakini uwezo wa kifedha wa kulima na kupalilia hawana. Kwa hiyo kwenye eneo hili naomba sana Mheshimiwa uone namna ya kuweka wawekezaji waje kuwekeza kwa ajili ya kilimo ili sasa hawa ambao ni wakulima wadogo waweze kuuza kwa hao wawekezaji ambao nao najua lazima kutakuwa na viwanda vikubwa kwa ajili ya kuchakata hayo mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni eneo la kilimo cha umwagiliaji. Mimi nashukuru mwaka 2016 jimbo langu lilipata bilioni mbili kwa ajili ya skimu za umwagiliaji, lakini kwa bahati mbaya sana Mheshimiwa Bashe, skimu hizo zilikwenda kujengwa kwenye mashamba ya watu, hili ni jambo la kusikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya Kalya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Bidyanguze kwa mchango wako, na muda wako umekwisha.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)