Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo ametujalia amani kwenye nchi yetu ya Tanzania jamani, kwa sababu tuangalie hali halisi ya ulimwengu lakini Tanzania Mungu ametubariki mpaka leo nchi yetu imekaa vizuri. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuzungumza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Bashe na Mheshimiwa Naibu Waziri wake, tunakiri kwamba hawa ni Mawaziri vijana, wanafanya kazi vizuri na kikubwa ni wasikivu, wanapokea simu zetu, wanashirikiana na sisi, naomba niseme nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie dakika zangu nane vizuri. Kwanza naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujitofautisha. Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan imejitofautisha sana kiutendaji upande wa kilimo. Kwa nini nasema hivi? Tanzania nzima tuna Majimbo ya uchaguzi 264, katika Majimbo hayo, Tanzania Bara yako Majimbo 214, Tanzania Zanzibar yako Majimbo 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kidogo niongee upande wa Majimbo 214 ya Tanzania Bara. Haya Majimbo 214, Majimbo 188 ni Majimbo ya Vijijini na Majimbo ya Vijijini ni Majimbo ya wakulima. Kwa nini nilikuwa nasema Awamu ya Sita imejitofautisha. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kitu kikubwa sana kutuletea pesa za kutosha za barabara za TARURA. Tulipopata pesa za kutosha kwenye barabara za TARURA ina maana vijijini mazao yatatoka kwenda kwenye masoko makubwa kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme ukweli, mimi mazao yangu mengi yanatoka milimani. Tangawizi inatoka kwenye Tarafa mbili ambazo ni asilimia 70 ya Jimbo langu. Kule kulikuwa hakuna barabara. Walanguzi walikuwa wanafwata tangawizi milimani. Kwa hiyo wao walikuwa wanafaidi sana kilimo cha milimani pamoja na tambarare, lakini baada ya kupata pesa za kutosha za TARURA wananchi wangu sasa wanapeleka mazao yao kwenye masoko makubwa. Niipongeze sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Naona niishie hapo kwa hili la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije upande wa umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa kujali umwagiliaji kwenye Jimbo langu. Nitakushukuru halafu nitakuomba msaada. Mimi nina mazao mawili makubwa, tangawizi na mpunga. Tarafa mbili zinalima tangawizi, zinahitaji umwagiliaji. Nakushukuru sana Mheshimiwa Bashe, umeanza kuboresha umwagiliaji, umeanza na Kata mbili Kata ya Miamba na Kata ya Mpinji. Sasa naomba nikupe siri ambayo hujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu Tarafa ya Mambavunda inategemea mto mkubwa unaitwa Mto wa Saseni ambako ndiyo mto huu unamwagilia tangawizi yote kule juu, lakini Mheshimiwa Waziri ule mto umeteremka ukaja mpaka Kihurio. Kihurio mto ule unalima mpunga, nikwambie ukweli ule mto sasa hivi umekwisha, umeharibika upande wa huku tambarare. Wananchi wa Kihurio wanalima mpunga, wananchi wa Kalemawe wanalima mpunga, ule Mto wa Saseni umebomoka lakini siyo wa kutengenezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Same. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu umeshakuja Jimboni kwangu usije wewe aje Mheshimiwa Mavunde, auone Mto wa Saseni ili aje akueleze muuboreshe Mto Saseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukweli Kata ya Kihurio ndipo nilipozaliwa mimi. Sisi ni wakulima wa mpunga, tangu nimekuwa mtoto mdogo mpaka sasa bila ya Mto Saseni hakuna Kihurio, hakuna Kalemawe. Naomba Serikali mje muone mto muuboreshe Mto Saseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia upande wa mbolea ya ruzuku. Nakiri Waheshimiwa mmeliongea hili lakini na mimi niongelee kwa upande wangu. Mheshimiwa nakushukuru sana, mbolea ya ruzuku nilikusumbua kwelikweli na hukuchoka kupokea simu zangu. Ulipokea simu zangu na ulinisaidia, lakini nikwambie ukweli; kwanza naipongeza Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kutoa ruzuku asilimia 50 ni mara ya kwanza inatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatokea mara ya kwanza mfuko unaonunuliwa kwa shilingi 140,000, mwananchi anaununua kwa shilingi 70,000. Tumpongeze Rais, amefanya kitu kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kwamba kuanzia tarehe 21/12/2022 mpaka tarehe 21/1/2023, nikiri nilipokea mbolea ya ruzuku mifuko 4,240 ambazo ni tani 212. Mheshimiwa Waziri nikwambie ambacho wenzangu wamekwambia, hii mbolea yote ilikwenda Kata ya Ndungu. Kata ya Ndungu ni Tarafa ya Ndungu. Kwa hiyo, wananchi wa Tarafa za Milimani zote walikuwa wanakuja Kata ya Ndungu. Nashukuru, nakupongeza, umeanza vizuri, lakini changamoto ya kwamba haikufikia wananchi wengi ni kubwa sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini hili mlisahihishe. (Makofi)