Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kuweza kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii, moja kati ya Wizara muhimu sana kwenye ustawi wa nchi yetu, kwa namna ambavyo inaendelea kufanya kazi vizuri. Lakini pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri hakika anafanya kazi vizuri sana na sisi kama vijana wameendelea kutuheshimisha kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo ambazo tunawapa Wizara na Wizara hii ukizingatia kwamba ndiye mkombozi wa wananchi wengi, hasa wakulima wadogowadogo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba ustawi wa chakula katika nchi yetu unaendelea kuwa imara zaidi. Na ustawi wa chakula katika nchi yetu unategemea sana wakulima hawa wadogowadogo ambao takribani wanachukua asilimia 70 ya Watanzania wote. Hivyo tuweke jicho la kipekee kwa wakulima wadogowadogo hawa. Tunashukuru Serikali kwa kweli, tumeona ilileta ruzuku ya mbolea ambayo imepelekea wakulima wetu wadogo hawa uzalishaji wao kwenda vizuri zaidi na uhakika wa chakula kwa wananchi umekuwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mbolea hii kuwekewa ruzuku kumekuwa na changamoto ya mbolea hii kuweza kufika kwa wakati. Mbolea kwa wakulima wetu imechelewa sana kwenye msimu uliopita. Mbolea ya kupandia imeweza kufika mwezi wa 12 mpaka mwezi wa kwanza, hali ambayo ilisababisha wakulima wetu wengi, hasa wadogo hawa, kuweza kupata changamoto ya kuweka mbolea hii ya kupandia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai na nitoe wito sana kwa Serikali ihakikishe mbolea hii ya ruzuku inafika kwa wakati kwenye maeneo husika ili wananchi wetu wengi hawa waweze kunufaika, na hasa ukizingatia na maeneo tunatofautiana kutokana na msimu. Sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini tunajua kwamba msimu wetu ni kuanzia mwezi wa 11 na 12 ndipo tunapanda; lakini maeneo ya kaskazini huko pia wana msimu wao, na ile mbolea iweze kufika kwa wakati ili wakulima hawa waweze kunifaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la bei yake; mbolea hii imakuja kwenye package ya kilo 50. Wakulima wetu wanauwezo wa hali tofauti ya kununua mbolea hii. Tuiombe serikali kupitia Mheshimiwa Waziri iongee na wale mawakala wanaoleta mbolea hii ili waweze kuweka kwenye parkage tofautitofauti, kuanzia kilo 50,20,10 mpaka kilo tano, ili hata mkulima ambaye analima bustani nyumbani kwake, anayelima matuta matano nyumbani kwake aweze kununua mbolea hii na aweze kunufaika nayo kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili mbolea hii kwenye maeneo mengi imeweza kufika kwenye makao makuu ya wilaya. Sisi ndani ya Wilaya yetu ya Chunya ilifika makao makuu ya wilaya; na sisi kama unavyojua, kwa jiografia, kwa ukubwa wa Wilaya ya Chunya ukienda kwenye Kata za mwisho za Kambi Katoto na Mafyoko kule ni takribani kilometa zaidi ya 200 kutoka Makao Makuu ya Chunya Mjini. Na bahati mbaya sana mbolea hii wale mawakala hawakuweza kuifikisha kule, kwa hiyo ilipelekea sasa upatikanaji wa mbolea hii kuwa ni wa gharama kubwa ambayo wananchi wetu wengi walishindwa kuipata kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Wizara, kwenye Wilaya yetu ya Chunya na baadhi ya maeneo mengine ipeleke mbolea hii. Si makao makuu ya wilaya peke yake bali na kwenye baadhi ya maeneo ya centers zile kubwa kubwa ili wananchi wetu hawa wengi waweze kunufaika sawasawa na mbolea hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie suala la zao la tumbaku. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla chini ya Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kweli wameweza kusikia kilio cha Wabunge. Zao la tumbaku ambalo lilikuwa ni kilio kwa wakulima sasa hivi limekuwa neema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko sasa hivi yanafunguliwa, huko sasa hivi ni chereko chereko, sasa wanamwimba Mheshimiwa Bashe, wanamwimba Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ambayo wanaifanya. Naomba sana, kampuni ambazo zimeletwa kwenye msimu huu, ambazo zinaendelea kufanya kazi ziendelee kufanya kazi vizuri na zilindwe. Vilevile, ikiwezekana kampuni nyingine pia ziweze kuja ili ushindani uweze kuwepo na baadaye mkulima aweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana wanaposhindana sokoni kwa wakulima ndivyo bei inavyokuwa nzuri zaidi na wakulima wetu hawa wanaweza kunufaika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kwenye upande wa tumbaku, kama yalivyokuwa mazao mengine, tumbaku ni moja kati ya zao ambalo halijapata mbolea ya ruzuku. Niombe sana kupitia Wizara hii na Serikali kwa ujumla ione namna ya kuweka ruzuku ya mbolea kwenye zao hili la tumbaku ili hawa wakulima wetu nao waweze kunufaika kama ambavyo wakulima wengine wa mazao wanaweza kunufaika kupitia kilimo hiki hili litaweza kutusaidia sana. Lakini bei yake, wakati msimu huu wa mbolea unaendelea; mbolea waliyoleta mara ya kwanza ilikwisha. Walipoleta mbolea mara ya pili walileta mbolea kwa wakulima wa tumbaku ikiwa ina nembo ya mbolea ya ruzuku, hali ambayo imeweza kuleta mkanganyiko mkubwa sana kwa wakulima wetu. Hii ni kwa sababu mifuko ina nembo inayoonesha kwamba hii mbolea ni ya ruzuku lakini wao wanauziwa kwa bei ambayo si mbolea ya ruzuku. Hali hii imewanyong’oneza sana wakulima wetu kwa sababu sasa hivi imeleta hali ya sintofahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha uje utupe na majibu. Kwamba ile mifuko ambayo imekuja ina nembo ya mbolea ya ruzuku je, wakulima hawa watalipa kwa bei ya ruzuku au watalipa kwa bei ambayo itaendelea kuwanyonya wakulima wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nizungumze ni suala la block farming au BBT. Sisi Wilaya yetu ya Chunya ni moja kati ya wanufaika wa mpango huu wa BBT kwa sababu tuna eneo la takribani hekta 47,000 ambalo limeshatengwa kwa ajili ya mpango huu. Mpango ni mzuri na tunapongeza Serikali kwa kuja na mpango huu tuna Imani kubwa sana mpango huu ukitekelezeka vizuri utakuwa ni mkombozi kwa nchi yetu na kuifanya Tanzania kuwa hub ya chakula kwa nchi zote za Afrika Mashariki na ikiwezeanika mpaka nchi zote mpaka Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linavyokuwa linakwenda lazima pia tuweze kutoa maangaliazo ambayo tunakuwa tunayaona. Moja kati ya mambo ambayo sisi tunaishauri Serikali, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwachukua vijana na kwenda kuwapekea kwenye kambi, mpango ni mzuri. Lakini, mnapochukua vijana hawa na kwenda kule kwenye kambi kule pia tuweze kuangalia vijana ambao wao tayari wamesha jiajiri kwenye kilimo hiki, tuweze kuwapa kipaumbele. Hawa vijana ambao tutawapa kipaumbele wataweza kutusaidia sana kwenye maeneo yale pale ili na wao waweze kunufaika. Hata benki huwa wanamkopesha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana…

MHE. MASACHE N. KASAKA: …mtu ambaye tayari anafanya biashara, sisi wale ambao tayari wameshaaanza kulima tukiwawezesha hii itaweza kuwasaidia na wao watazalisha kwa wingi zaidi na baadae tuwachukue hawa ambao tumewapeleaka…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Njelu Kasaka muda wako umekwisha.

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja.