Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kusema namshukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa kutupa bajeti ambayo imekuwa ni nzuri. Lakini niseme wazi, napata tabu sana kusema naunga mkono kwa asilimia mia. Kama nitaunga ni kwa sababu tu bajeti hii bado inaendelea kuwapa ruzuku ya mbolea wakulima; lakini nina matatizo makubwa sana na maeneo ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeiangalia sana bajeti hii, na nimeangalia fedha tulizotumia kwenye eneo la umwagiliaji. Kuna skimu za kila aina hapa; skimu 42 mpya, kuna block farms zimeanzishwa, kuna mabonde ya umwagiliaji, kuna skimu nyingine 30 za hekta 69,000. Skimu zote hizi ukiziangalia kwa ujumla wake watu wa njombe hatumo. Kwa hiyo inanipa shida kuelewa allocation ya resources hizi muhimu kwa watu wa Njombe na mikoa mingi ya Nyanda za Juu Kusini, hatumo. Sasa, kinachonisikitisha zaidi…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba ukiangalia kwa karibu zaidi watu wa Njombe tuna zao la chai. Mwaka 2015 tulikuwa na chai vision ya kuweza kuzalisha chai na ku-recruit watu wakulima wadogo wadogo wa chai 2,500. Lengo hilo limefanikiwa, wameweza kulima takriban hekta 2,300 na tume-recruit wakulima wadogowadogo takriban 300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Njombe Vision kilikuwa na kujenga kiwanda, kiwanda kimejengwa, ni kiwanda kikubwa, kimejengwa na kampuni ya Uniliver kama package ya kusaidia wakulima wadogowadogo. Kiwanda hiki kinapokea majani kilo 50,000 capacity yake. Lakini wakulima wadogowadogo hawa wameshindwa kupeleka majani kufikisha kiwango cha capacity ya kiwanda, wanaweza kupeleka majani tani kilo 15,000. Na watu wa Lupembe wameongezea, tumefika angalau kilo 30,000, bado tuna deficit ya kilo 20,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kiwanda hiki kinatishiwa kufungwa kwa sababu capacity yake ni kubwa na uwezo wa kuleta majani ni mdogo. Kitakachotuwezesha pekee, ili kiwanda hiki kiweza kuendelea na wakulima wadogowadogo kuendelea ku-supply majani na wao kuongeza kipato na ajira ni kama tunaweza tukaongeza uzalishaji wa majani ya chai mabichi. Na itakayo tuwezesha ni umwagiliaji pekee. Katika mazingira kama haya nipende kusema nilitegemea sana kwamba, kwa kweli bajeti hii ingeangalia maeneo kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na turudi nyuma tuangalie; katika principle za uchumi ni vema ku-consolidate the game. Watu ambao wamejituma wamefia mahali wameanza, wadogowadogo wanauwezo, wamejiwezesha wenyewe, tuka wa-support kwanza kuliko kuchukua resources nyingi na kuzitupa na kuzituma kila mahali. Hakuna ubaya kuwa na block farms, lakini tuangalie tu-consolidate pale ambapo tumefanya vizuri kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ukisoma kwenye mpango mzoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo hayo ya chai si kwamba ameyaacha kabisa, anachosema wataendelea kufanya utafiti. Hivi, ni utafiti gani wa umwagiliaji wa chai unataka kuufanya? Mwaka 2019 Halmashauri ya Njombe ilianzisha mpango wa umwagiliaji wa chai kama pilot project. Mimi nilipoingia Bungeni mtu wa kwanza niliyemchukua na kumpeleka Njombe alikuwa ni Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Prof. Mkenda. Walikwenda, tukaangalia maeneo yale na ile project ni nzuri sana, ya block farming ya wakulima wadogowadogo. Hatuongelei large scale farming hapa, wakulima wadogowadogo wa kawaida akina mama, akina dada na akina kaka. Ile program ilitakiwa sasa i-run kwenye zile hekta 2,500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mazingira kama hayo kuna sababu gani ya Wizara kutoliangalia eneo hili na muhimu sana la umwagiliaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ukiangalia Mheshimiwa Bashe anasema yeye anaangalia bajeti yake inaangalia ilani ya chama inaangalia mpango wa miaka mitano. Lakini kwenye ilani ya chama akisoma vizuri page 38 mpaka 41 kifungu 37 “D” kinasema; Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ita- focus zaidi kuongeza uzalishaji wa majani ya chai na kuongeza tija kwa wakulima wadogowadogo wa chai. Sasa unawezaje kuacha hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuliongelea hilo kwa sababu ya muda, lakini niseme, chai ni ubora, Tanzania bado chai yetu haina ubora. Bodi ya Chai inatakiwa iongeze nguvu kwenye kusimamia ubora wa chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa haraka kwenye mbolea. Sisi tunaishukuru sana Serikali na wakulima wa Njombe wanaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutoa mbolea ya ruzuku, na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mpango huu mkubwa. Nipende kusema kwamba, tulitegemea kwamba dosari za mpango ule uliopita zingeangalia ili kuweza kuboresha mbolea ifike kwa wakati, kama walivyosema wenzangu, lakini kwa Njombe tuna kitu tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni wakulima wakubwa, Wananjombe ni watu wanaojituma, ni watu hodari wa kilimo na hili halipingiki mahali popote. Msimu wetu wa kulima ni tofauti na maeneo mengine. Mbolea ya kupewa mifuko mitatu kwa eka haitutoshi, hiyo mbolea ni kwa ajili ya mahindi pekee yake. Ukienda kwenye viazi tunalima misimu mitatu kwa mwaka mmoja, Oktoba, Novemba yaani tunavuna Desemba. Tukipanda Februari tunavuna mwezi Juni. Halafu wananchi wa Njombe wamejiongeza, wanalima kilimo cha kumwagilia cha asili ambacho na chenyewe mwezi Juni wanaanza kuvuna Mwezi Septemba. Tungetaka tuongezewe mifuko ya mbolea angalau sisi tupate kwenye kilimo cha viazi pekee yake mifuko minne mpaka sita, ingefaa kwa kila eka ili tuweze kuendelea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema kwenye hili unaona kunatokea uchakachuaji na hatuwezi kuwa-protect wachakachuaji, lakini ukweli ni kwamba demand ya mbolea kwa maeneo yale ni kubwa mno kuliko supply na haiji kwa wakati. Hiyo inasababisha watu wasiwe waaminifu kuingia katika schemes za kutaka kutengeneza na kuuza mbolea ili kujipatia fedha. Namuunga mkono Waziri kusema kwamba sasa tutafanya hili jambo liwe jinai na isiwe jinai tu, tulifanye kabisa liwe ni uhujumu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa parachichi kwa sababu muda unaniishia. Nimeona tuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa parachichi na wapongeza wakulima wa Tanzania na hasa wa Njombe maana yake ndio wazalishaji wakubwa wa parachichi katika nchi hii. Tunategemea tumefika tani 29,000 na tumepata karibu milioni 52, lakini tunategemea kwenda kwenye tani 50,000 by mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia hapo bado tunahitaji mambo mengi sana ya kufanya lakini mojawapo Njombe tunaomba kwenye viatilifu tuangaliwe kama vile ambavyo korosho wanapewa, ruzuku kwenye pamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwanyika.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: …na sisi tupate ruzuku kwenye madawa ya ukungu ili tuweze kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nitaomba maelezo mazuri kwa nini Njombe …

MWENYEKITI: Ahsante sana.