Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii uliyonipatia ya kuongea katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Pia nampongeza sana Mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa kutupa nafasi hii ya kuzungumza tena leo katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri, wataalam, Katibu Mkuu kwa kutupatia bajeti hii ambayo tunaizungumzia leo. Nilivyokuwa napitia nimegundua kwamba ukuaji wa sekta hii sasa uko 3.9. Hapo nyuma ulikuwa 4.9, maana yake kuna mahali fulani ukuaji kama unashuka hivi. Sasa unashuka kwa sababu gani? Nafikiri Waziri atakuja kutuambia, lakini mchango kwa pato la Taifa umekuwa 26.9 na tulikuwa tumekwenda 29, inawezekana kuna sekta imekua inaanza kuchangia zaidi kuliko kilimo. Ikumbukwe tu kwamba sisi Watanzania wengi tumeajiriwa kwenye sekta hii. Kwa hiyo, naamini kabisa ni sekta ambayo inabidi iangaliwe kwa umakini iwe na ukuaji mkubwa, ikikua maana yake na uchumi wetu utakuwa unakua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nijikite, naona zile taarifa za kimataifa na za Kitaifa zimezungumziwa sana, nataka nijikite kwenye Halmashauri yetu ya Geita ambayo inaitwa Geita DC. Mwaka 2020 kwenda 2021 sisi tulipanga kulima hekta takribani laki 115.4, lakini tuna hekta laki 327, maana yake tunalima kama asilimia 50 tu. Kuna kitu cha kufanya hapo. Tulitarijia vile vile tuweze kuvuna mazao ya wanga takribani tani laki 364.34 na mazao ya mikunde takribani tani 87,902 kwa kulima hekta 46,245. Hili limefanyika mwaka 2021 na tulipata mazao na ukamilishaji wake asilimia kama 99.9. Mwaka uliofuta makadirio yalikuwa ni hayo hayo na wakapata mafanikio hayo kama asilimia 99.9. Maana yake ni kwamba inawezekana makadirio tunayojiwekea sio makubwa sana kwa sababu eneo kubwa bado halijalimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini hapo? Inawezekana changomoto hii ya ukuaji wa sekta yetu tunayoiona ni kwa sababu kuna sehemu kubwa kule kwenye maeneo bado haijalimwa. Sasa naishauri nini Serikali? Naishauri Serikali kwamba kwenye mazingira haya tuliyonayo ziko changamoto kadhaa ambazo nazijua nikizitaja kwenye Geita DC zitakuwa ni changamoto ambazo zinaweza kuwa hata ndani ya nchi. Kwa mfano, sisi Jimbo la Geita na Jimbo la Busanda tuna takribani jumla ya kata 37, tuna Maafisa Ugani 23. Unaweza ukajua kama Maafisa Ugani ni 23, kuna kata 14 hazina Maafisa Ugani. Sasa hawa wanaendaje, maana yake ni kwamba hawa wanakwenda bila kuelekezwa nini cha kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, ukichukua tarafa kwa maana ya Tarafa ya Busanda, kuna kata 11, Maafisa Ugani wako saba. Tarafa ya Butundwe Maafisa Ugani wako tisa, Bugando wako watano, Kasamwa wako wawili jumla ni 23. Tuna kazi kubwa ya kufanya hapo kwamba hawa Maafisa Ugani sasa waongezwe kwenye maeneo yetu. Pia vipimo vya udongo ambavyo mwaka jana tulisema udongo utafitiwe, hakuna kipimo hata kimoja kilichokwenda, maana yake wakulima wetu wanalima kibubu hivi, hawajui udongo una hali gani na kitu gani kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha tatu ambacho nilikisema ni pembejeo kwa maana ya mbegu na mbolea. Hii mbolea mfumo uliowekwa mwaka jana na ruzuku iliyowekwa na Rais, nimpongeze Mheshimiwa Rais imeleta uchangamfu wa sekta hii, lakini utaratibu uliotumika, wakulima wengi hawakupata mbolea. Kwa nini? Umbali, kwa hiyo ni ombi langu kwamba sasa mbolea hii ipelekwe kwenye kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo naiona ni kwamba hata wale Mawakala ambao walifanya mwaka jana, wanaonekana sasa hawakwenda vizuri na mfumo wa Serikali, wengine wameanza kwenda TAKUKURU kuhojiwa. Kwa hiyo nina mashaka kwamba utaratibu wa mbolea wa mwaka huu huenda Waziri akapata Mawakala wachache kwa sababu ya hofu hiyo. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri waliangalie hiki tunalifanyaje kwenda kwenye kata zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye mbolea hii hii, wale waliokuwa wameandikishwa mwaka jana wako wakulima wengi hawakuandikishwa. Ningeomba sana hawa waandikishwe ili kusudi kila mmoja aweze kufaidika na hii mbolea ya ruzuku na uzalishaji wetu ukue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, nimeona kuna upembuzi yakinifu wa skimu kadhaa katika Kata ya Nyakagomba, Kata ya Nyachiluluma, Kata ya Bukondo na Kata ya Magenge. Naamini kabisa hili kama atalifanya kwa wakati huenda tukaona matokeo mapema, kwa sababu tuna takribani hekta 7,200 kwenye maeneo haya ambayo zikiwekewa umwagiliaji watalima mara tatu badala ya kulima mara moja. Kwa hiyo, niombe sana huu upembuzi yakinifu usichukue muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge na nchi nzima tuna matarajio kwa bajeti inayotolewa na Mheshimiwa Rais hapa tuone matokeo mapema na hayo matokeo najua kwa sababu ndio tunaanza yanaweza yakachukua muda mrefu kutokea. Kwa hiyo, niwaombe sana tujitahidi kufanya kadri inavyowezekana matokeo yaanze kuonekana. Kila anayesimama atakuwa anaongelea hili kwa sababu ndio tunaanza na matokeo yanazidi kuchelewa kuoneka, ianze kuonekana nini kinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambalo nataka kusema ni kuhusu hizi block farming ambazo wenzangu wamezisema. Kule Mkoani Geita sina uhakika block farming iko sehemu gani. Kwa hiyo kila unayemuuliza anakwambia hiki ni kitu gani. Niwaombe sana hii vocabulary ya block farming hii ije kule Geita watu watambue ni kitu gani kinatakiwa kufanyika, kwa sababu sasa hivi inaonekana tu iko mahali. Najua inawezekana ni kwa sababu ya mafungu, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri atembelee kule wamfahamu, wajue block farming ni nini kwa sababu sasa hivi definition yake kule kwetu wanaweza kukwambia ni uvuvi, kumbe block farming ni mashamba. Nimkaribishe sana Waziri aje eneo hilo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Magessa na muda wako umekwisha, lakini unayo hiari ya kuunga mkono hoja kama ulikua hujamalizia.

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)