Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii. Vilevile kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya. Nimeongea mara nyingi hapa, sisi Manyoni Mashariki tumepata miradi mingi sana ikiwepo hii miradi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Bashe pamoja na Naibu Waziri, ndugu yangu na mdogo wangu Mheshimiwa Mavunde, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini bila kuwasahau watendaji wetu wa Wizara ya Kilimo hususan, Bodi ya Korosho, lakini Bodi ya Umwagiliaji na Katibu Mkuu. Mheshimiwa Bashe ametusaidia sana kwenye kilimo cha korosho Manyoni. Najua kuna mambo mengi ameyafanya, sasa hivi kilimo chetu cha korosho Manyoni kinaenda vizuri sana. Sasa hivi anajenga maghala, lakini ametupelekea pikipiki, lakini kuna vitu vingi sana ambavyo amevifanya kwa hiyo, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nina ajenda kubwa mbili ambazo ningependa kuchangia kwenye Wizara ya Kilimo. Eneo la kwanza nitachangia upande wa skimu za umwagiliaji na eneo la pili nataka niishauri Serikali jinsi gani tunaweza tuka-transform Tume ya Umwagiliaji. Wachangiaji wengi wameeleza hapa kuhusu umuhimu wa Tume ya Umwagiliaji kwa hiyo, naomba nichangie eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa skimu za umwagiliaji; kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, alimtuma Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde alikuja Manyoni pale Chikuyu kwenye Skimu ya Umwagiliaji wa Chikuyu. Ile skimu ilikaa miaka mitatu wananchi hawajalima, lakini alikuja akatoa maelekezo na nimshukuru sana Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji walikuja wakaikarabati ile Skimu ya Umwagiliaji ya Chikuyu, lakini bahati mbaya mwaka huu tena ule mto ukaenda kubomoa sehemu fulani ya ile skimu.

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye bajeti ya Waziri kwamba, ameweka vilevile kukarabati hii Skimu ya Chikuyu. Nimwombe tena Mheshimiwa Waziri, tukamalizie ile kero ili tuwape matumaini wakulima wa hapo chikuyu.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Kintinku, Tarafa ya Bahi na Tarafa ya Kilimatinde sisi tunategemea kilimo cha mpunga na kilimo cha mpunga kinahitaji umwagiliaji. Nimeona kwenye bajeti ya kilimo wameweka ukarabati wa Skimu ya Ngaiti, Skimu ya Maweni, Skimu ya Lusilile, ya Udimaa hata ya Msemembo. Nimwombe sasa Waziri, ukarabati huu uende kufanyika, hawa wananchi asilimia 100 wanategemea kilimo cha umwagiliaji. Bila kuwepo miundombinu ya umwagiliaji ambayo ni mizuri maana yake tunatengeneza njaa kwa hawa watu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na mdogo wangu Mheshimiwa Mavunde wajitahidi wakawasaidie hawa ndugu zangu wa Ngaiti, Maweni, Mtiwe, Chikuyu, Msemembo, lakini Udimaa na Lusilile hizi skimu zao mwaka huu zikatengenezwe, zikakarabatiwe ili angalau mwaka unapoanza wa kilimo waweze kulima.

Mheshimiwa Spika, lingine, Waziri mwaka jana alikuja na bajeti ya kusema kwamba, anaenda kuanza kufanya feasibility study ya Mradi wa Bwawa la Mbwasa. Nimefurahi kwenye bajeti hii vilevile Waziri ameeleza hapa kwamba anaenda kufanya mapitio ya ile feasibility study ambayo ilishafanyika muda mrefu sana, lakini vilevile anaenda kuanza kujenga Bwawa la Umwagiliaji la huu Mradi wa Mbwasa.

Mheshimiwa Spika, huu mradi wananchi wameusubiri kwa muda mrefu sana. Nakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri Mavunde alipokuja wananchi walimuuliza na aliwaahidi kwamba, Serikali ipo mbioni kuhakikisha kwamba, huu mradi unaanza kujengwa. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri auchukue huu Mradi wa Umwagiliaji wa Mbwasa kwa sababu ni mradi ambao utawaokoa sana wananchi wa Manyoni, hususan Tarafa ya Kintinku ambako wanategemea zaidi kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, tuna bodi yetu ile Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, nilitegemea sasa tunapoongelea kilimo cha mpunga katika hizi tarafa tatu, Tarafa ya Bahi, Tarafa ya Kintinku na Kilimatinde, tuwe tuna uwekezaji wa masoko angalau katika hizi tarafa tatu. Hatuna masoko ya uhakika ya mpunga, tuna madalali tu na walanguzi ambao wanaingia kwenye eneo lile la Kintinku, Bahi na hata Kilimatinde.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Waziri, tuna Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, awa-task hawa watu waweke miundombinu pale, maghala, lakini watuanzishie masoko ili wananchi wetu wawe na uhakika wanapouza mpunga wanauza kwa bei ambayo itakuwa na manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kuhusu hii Tume ya Umwagiliaji. Watu wengi wamechangia kuhusu hii Tume ya Umwagiliaji. Niseme kweli na nimekuwa nikichangia sana, hatuwezi kuendeleza kilimo cha Tanzania kama hatutawekeza kwenye hii Tume ya Umwagiliaji. Ni eneo ambalo kwa kweli, tunahitaji kuwekeza. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais mwaka huu, kuanzia Rais Dkt. Samia alipoingia madarakani bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda sana, mwaka jana ilikuwa bilioni 700, mwaka huu tuna bilioni zaidi ya 900, lakini vilevile bajeti ya umwagiliaji imepanda, mwaka jana tulikuwa na bilioni 262, mwaka huu tuna bilioni 373, haya ni mapinduzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji kufanya vitu viwili. Eneo la kwanza ambalo naliona na ningependa kushauri, kwa nini hii Tume yetu tusii-transform? Hapa ukisikiliza Wabunge wengi wameongelea suala la umwagiliaji, we need a giant institution, tunahitaji kuja na kitu tofauti na tume, kwa nini tusifikirie kuja na authority, National Irrigation Authority? Kama tulivyokuja na RUWASA, TARURA, TANROADS, iwe giant? Tuipe meno, tuipe fedha, ili iweze ku-manage suala la irrigation kwa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri angeeleza kwamba, lini anakuja kuanzisha National Irrigation Authority ambayo sasa itaenda ku-spear head masuala ya umwagiliaji. La pili, tunapofikiria kuanzisha hii authority, lazima tufikirie kwenye financing frame work, fedha tutapata wapi? Ukiangalia kwa kiasi kikubwa vyanzo vya fedha vya hii tume ni zile tozo za wakulima kutoka kwenye skimu, skimu ambazo hatujazikarabati. Nashauri, tunahitaji kuja na mfumo mzuri wa kutafuta vyanzo vya mapato, mbona tunatoza maeneo mengine kwa nini tusitoze asilimia tatu kwa wakandarasi ile asilimia tatu ikaingia kwenye hiyo Tume ya Umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa kweli katika haya Mheshimiwa Waziri, alichukue hili, hasa hasa la kwenye suala la ku-transform Tume ya Umwagiliaji. Sisi Wabunge wengi tunategemea kwamba, kama tuta-invest kwenye suala la irrigation, umwagiliaji, tunaweza kwenda ku-transform kilimo cha Watanzania, lakini kama tutakuwa hatuna uwezo wa kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji uwezo wa ku- transform kilimo utakuwa ni mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nirudie tena kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwanza kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini nimshukuru sana Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, amefanya mambo makubwa sana Manyoni. Nimshukuru sana vilevile Mwenyekiti wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Mkurugenzi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)