Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hoja iliyopo mbele yetu, hoja ya Wizara ya Kilimo. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi ambazo amepeleka katika jimbo letu, lakini kwa bajeti hii ametukumbuka pia, ametupelekea fedha. tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia Mheshimiwa Waziri, msaidizi wake Naibu Waziri na watendaji wote kwa kazi kubwa na hasa ikizingatiwa kwamba, Wizara yao ni Wizara ambayo inachangia kutoa huduma kwa zaidi ya asilimia 65. Tunawashukuru na tunawapongeza sana Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naunga mkono hoja kwa sababu tu kwanza niliomba kwenye skimu za umwagiliaji mwaka jana na kweli mwaka huu wameweza kutuingiza kwenye ukarabati wa skimu ambazo zilikuwa na matatizo. Zipo Skimu za Mughwazi, Skimu ya Ruhwiti na Katengela, hizi zimetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati, sisi Kakonko tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo pia skimu ambazo ni mpya zinakwenda kuanzwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Ipo Skimu ya Ruhuru, Skimu ya Mgunzu, Skimu ya Kanyonza na Skimu ya Churanzi, hizi ni skimu mpya, tunashukuru fedha zimewekwa kwenye bajeti. Sasa niombe fedha zikishapitishwa, nina hakika bajeti ya Waziri itapita, watuletee fedha ili kazi iweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze vilevile kwa kuzungumzia suala la mbolea. Mbolea ni muhimu sana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kilimo kinafanyika, lakini nizungumze kwamba, mbolea na mbegu bora hazipelekwi katika majimbo yetu kwa wakati. Wilaya yetu ya Kakonko tunapata mvua kuanzia mwezi Septemba, lakini mbolea inakuja kufika mwezi Desemba, wakati huo mahindi yanabeba, mbolea ile haiji kutusaidia. Hii inakwenda sambamba na ubora wa mbolea hiyo, katika Wilaya ya Kakonko na mimi mwenyewe ni mkulima, tumepata mbolea lakini ubora wake sio sahihi. Hili nililiwasilisha katika ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikatoa taarifa kwamba, mbolea tuliyopata na ambayo nimeitumia hata kwenye shamba langu, shamba halina mabadiliko yoyote.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba, Wizara ilituma wataalam, wakaja kuchukua sehemu ya mbolea ile iliyobaki, lakini vilevile wakachukua udongo, sijapata majibu. Kwa hiyo, niombe atakapokuwa anahitimisha tuweze kupata majibu sahihi, kuna Mbunge mwenzangu amechangia hapa suala la ubora wa mbolea tunayoipata haiko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la bei ya mazao. Wilaya ya Kakonko moja ya zao letu ambalo ni la kimkakati ni alizeti. Alizeti ni zao la mkakati kwa Wilaya ya Kakonko likienda sambamba na zao la chikichi pamoja na muhogo, tatizo hatuna uhakika wa bei. Tuombe Serikali itusaidie kupata bei inayolingana na mazingira yetu, ili wananchi waweze kufaidi vizuri zao hilo la muhogo, ikiwa ni pamoja na zao la alizeti, ikiwa ni pamoja na zao la chikichi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla naomba nitoe sasa ushauri ufuatao: -

Mheshimiwa Spika, nina hakika Wabunge wametoa ushauri, wametoa maoni mbalimbali, haya yote hayawezi kufanyika bila kuwa na wataalam. Kwa hiyo, moja niombe Serikali iajiri watumishi na watumishi hao wapelekwe katika vijiji vyetu, wapelekwe katika mashamba yetu na wasimamiwe, ili waweze kufanya kazi ya kuwafikia wananchi, kutoa ushauri wa kitaalam. Nina hakika baada ya muda si mrefu Serikali yetu, nchi yetu inaweza ikapata chakula cha kutosha na kupata akiba kwa ajili ya matumizi mengineyo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu pia ni kuhakikisha kwamba mashamba yale ambayo yamepelekwa kwa ajili ya vijana maarufu kwa jina la BBT, hebu yapelekwe kwenye Mikoa ile ambayo ina mvua za kutosha. Asubuhi wamechangia kwamba imeletwa Dodoma, kwetu Kigoma limechukuliwa eneo dogo sana, ninaomba maeneo yale ambayo yana mvua za kutosha kama Mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Mbeya na Njombe, tupeleke huko,nina hakika mvua zipo za kutosha, ardhi ya kutosha na hivyo haitakuwa shida, vijana wetu wataweza kupata huduma hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni kuhakikisha kwamba mbolea mbegu pamoja na viuatilifu vinapelekwa kwenye Majimbo yetu na kwenye Mikoa yetu kwa wakati, isiwe tunahitaji mbolea ya kupandia inakuja tunamalizia palizi. Tunahitaji mbolea ya kukuzia inakuja mahindi karibu yanaiva. Niombe sana pembejeo zipelekwe mapema katika Mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia yapo mazao ya kimkakati ya chikichi na alizeti tuhakikishe kwamba nayo yanapewa bei ya kutosheleza kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, ninashauri kwamba Serikali ihakikishe kwamba inalinda bei ya mazao mbalimbali ambayo yanalimwa katika nchi yetu. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba mazao yanahifadhiwa ikiwa ni pamoja na kujenga maghala ambayo yatasaidia wananchi wetu kuweza kuhifadhi mazao na kuyauza kwa wakati ambao utakuwa unastahili na ambapo wataweza kuongeza bei yao.

Mheshimiwa Spika, nishukuru tena kwa nafasi ambayo umenipa, naunga mkono hoja. (Makofi)