Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ambayo ni muhimu sana kwetu. Nianze kwa kusema kwamba tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na kipekee kwa hapa, Waziri wa Kilimo, wametutendea haki kwa kuongeza fedha ambazo zinaenda kusaidia Watanzania wengi sana kama zitatumika ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kusema kwamba mkakati unaotekelezwa sasa hivi na Wizara hii ya Kilimo ni mkakati ambao ni tofauti sana na miaka yote ambayo tuliwahi kuutekeleza. Ni tofauti sana na ninaona kwamba lawama nyingi zinazojitokeza kwa wakulima na hata kwetu sisi Wabunge zinatokana na ukweli kwamba hatukuwa tumeidhinishwa vizuri, hatukuwa tumepata miongozo ya kutosha ili kuweza ku-communicate na wale watu wetu kule vijijini wakaelewa ni kitu gani kinakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo najua kwamba tunajifunza kwa kufanya na tunapojifunza kwa kufanya tunafanya makosa, kunatokea makosa na ninaamini kwamba kiongozi mwerevu ni yule ambaye sasa anachukua yale makosa na kuya-address ili huko mbeleni yale makosa yapungue tuweze kuona mkakati huu ukifanikishwa.
Mheshimiwa Spika, kusema kweli huu mkakati ni mkakati ambao ulihitaji uhamasishaji mkubwa na maandalizi mapema, ninaomba sasa kwamba Serikali iendelee kuwaandaa mawakala. Kule kwetu Vunjo tulikuwa na mawakala watatu tu kwenye Kata 16 zenye watu 255,000 ni wachache sana, kwa hiyo watu walikuwa wanatembea mbali kutafuta na mara nyingine wanakuta kwamba wale mawakala wameishiwa na mbolea au wana mbolea aina moja kwa hiyo unaenda unarudi. Kwa hiyo, kusema kweli ni mkakati ambao tunauunga mkono lakini sasa Serikali ijiandae vizuri kwa kutengeneza huo mfumo wa kugawa hii mbolea ya ruzuku, ninaamini kwamba itaendelea kwa sababu bei za mbolea duniani bado ziko juu kiasi, lazima tujue kama alivyosema mmoja wetu, kwamba tuna-subsidize au tunatoa ruzuku kwa bei tunayojua, tusitoe ruzuku kabla hatujajua kwamba bei ya kufikisha zile mbolea hapa Tanzania zitakuaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule kwetu Vunjo na Kilimanjaro kwa ujumla, natumaini tumenufaika kidogo sana kwa miradi ambayo imetekelezwa. Kitu cha kwanza ambacho ninataka niulize ni kwamba, vigezo vilivyotumika kugawa miradi mbalimbali ya umwagiliaji, miradi ya mabwawa, miradi ya maghala na miradi ya uhifadhi wa mazao imefanyika namna gani na vigezo gani vimetumika? Kwa sababu la sivyo, tutabaki kusononeka wenyewe, tunasema hapa kuna upendeleo. Kwa sababu ili kuondoa masuala ya upendeleo au siyo upendeleo, lazima kuwe na criteria na rules ambazo zinam-guide yule anayesema sasa napeleka ghala Songea au sehemu nyingine (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nashangaa kwa sababu kwa mfano kule kwetu tuna magulio au masoko ambayo toka kabla ya uhuru yapo, yamezeeka. Mama anakwenda ananyeshewa mvua wakati wa mvua, jua linampiga, hakuna hata paa, hakuna allocation yoyote iliyofanyika kusema kwamba hebu tusaidie wale watu wa kule Vunjo kwa mfano kwenye Masoko ya Himo, Mwika, Mombi, Kisambo, Marangu Mtoni na kadhalika, wakapata angalau mahali pa kujiepusha.
Mheshimiwa Spika, inavyotokea ni kwamba mkulima anapokwenda na mazao yake, mahindi au mbogamboga, akishindwa kuuza siku ile basi lazima ama aviache, avitupe au arudishe nyumbani ambapo hakuna walaji. Kwa hiyo, inakuwa kwamba kungekuwa na miundombinu hii ya maghala ambayo naamini kwamba haya ambayo yanatengenezwa sasa hivi na Mheshimiwa Bashe yana viwango vya kuweza kuhifadhi mbogamboga hizo, ndizi hizo baadaye zikauzwa kwa wale wachuuzi wanaojitokeza inakuwa ni vigumu sana kusema kwamba tumesaidika vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana ikiwezekana hiyo iangaliwe na ninaamini kwamba soko linakuwepo lakini wale madalali wanaokuja kununua kutoka Dar es Salaam lazima waweze kuhifadhi mahali yale mazao. Nashukuru pia Mheshimiwa Bashe ameona umuhimu wa ku-emphasize kwenye huu mkakati wake kwamba analenga kuongeza zaidi uzalishaji wa mazao ya chakula, maana yake nafaka, mbogamboga na matunda ambayo yana tija lakini ni very delicate haya mazao, ni perishable, ukiweka baada ya siku mbili, tatu, yanaharibika kama hayakuhifadhiwa sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naambiwa kwamba tani milioni 2.75 zinazozalishwa za mazao haya ya matunda na mbogamboga ni asilimia Nne tu inachakatwa. Kwa hiyo ina maana nyingine inaharibika na wale wanaobahatisha zinanunuliwa na wenzetu wa mpakani ambao wana chain nzuri ya kuweza kuhifadhi na kusafirisha haya mazao kupeleka sokoni, sisi tunabakia hapa kusema kwamba watu wanao-export maparachichi yetu ni majirani zetu! Ukweli ni kwamba kama hatujajenga miundombinu ya kufikisha mazao yetu sokoni yataishia kwa majirani, kwa sababu wale wana miundombinu, wanazo quality cold rooms za kusafirisha haya mazao ambayo ni perishable ambayo yanaharibika kwa haraka. Kwa hiyo, naomba katika mchakato huu Mheshimiwa Waziri aone namna gani atatusaidia kwenye kulinda hiki tunachozalisha kwa wingi kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naona wenzangu wamekuwa wanasema huwezi kutekeleza mkakati mmoja unaofanana kwenye nchi kubwa namna hii kwenye Kanda zote na Mikoa yote, it’s impossible. Huwezi kusema kwamba labda uanze kulima korosho kila mahali au kahawa kila mahali, haitawezekana! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba kwa mfano mwenzangu mmoja alitoa mfano wa Malaysia, lakini nataka kusema kwamba kweli kule kwetu Kilimanjaro ambako hatuna ardhi, mkakati wetu unataka intensive farming, kumuwezesha mkulima azalishe kingi kwenye kaeneo kadogo na azalishe kwa mwaka mzima, which means umwagialiji ni kitu cha msingi sana, azalishe kwa mwaka mmoja lakini atumie eneo dogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo mengine kusema kweli huhitaji hata mbolea. Kwanza maeneo mengi hayajatumika na mmomonyoko wa udongo haujaharibu sana kwa hiyo ukifanya extensive farming, ukawapelekea hizi tractors na mashine zikasaidia mechanization, utaongeza tija yao extensively, maana yake kwa kutumia maeneo makubwa. Kwa hiyo ninataka kusema kwamba kusema kweli tuangalie, bila kufanya vile tutapata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kingine ninacholalamika ni kwamba kule kwetu nimetafuta kila mahali kwenye hii document ya Mheshimiwa Waziri nione BBT kule Vunjo imefikaje. BBT iko wapi Vunjo? Huwezi kugawa vitalu kwa miaka 66 kwa mtu yuleyule! miaka 66 si atauza na yeye kwa sababu lazima i- rejuvenate. Kusema kwamba hii ingekuwa ni seed mtu anapewa kwa mwaka mmoja wa pili anakuwa amechota faida ya kutosha anapeleka ku-invest mahali pengine, anamwachia mwingine, wanapeana vijiti, nae anazalisha, akishakaa miaka miwili anaenda inakuwa ni rotation. Hata kama unasema unampa mtu mmoja, mimi sijui nani atapewa, lakini naamini kwamba hiyo kitu ambayo hata criteria ya kusema unachagua eti watu waombe, mtu aombe wakati hajawahi kuona shamba unamwambia omba! Kwa sababu ana uwezo wa kuingia kwenye kishkwambi anaomba, pengine hata siyo yeye atakwenda kufanya kazi. Halafu ukweli ni kwamba kwenye hivi vitalu hata ikiwa ni eka tano, watahitaji wafanyakazi pia. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei, muda wako umekwisha.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)