Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyekujalia wewe kuwepo leo hapo na kumjalia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiona nafasi ya bajeti hii ya Kilimo kama chachu ya maendeleo na sehemu ambayo tunakuja kukabiliana na suala la njaa, ameongeza asilimia 29 katika bajeti hii, tumpigie sana makofi, Insha Allah! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nataka nishukuru kwanza. Namshukuru sana Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Tumekwenda kwake kwa ajili ya kumwomba mahindi ya njaa kwa ajili ya kupunguza bei. Hali ya chakula Sengerema ilikuwa ni ngumu, gunia moja la mahindi liliuzwa mpaka shilingi 130,000 na baadaye tulikwenda kwa Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo na akakubali kutupatia tani 2,000. Ametuokoa sana, Mungu akujalie sana Mheshimiwa Waziri Bashe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nishukuru kwa suala la ndege waharibifu. Tumekwenda kwake kumwomba ndege kwa ajili ya kunyunyuza dawa ya kuwaua ndege waharibifu wa mazao kule Sengerema, akatutumia ndege. Ila ndege ile ilipokuja kwetu ilitokea Kilosa, na baadaye ndege ile ilikwenda kutua Mwanza halafu ikaja kupuliza dawa. Ikimaliza kupuliza dawa, ndege ile inarudi kwenda kutua Mwanza. Sasa naziangalia zile gharama za ile ndege, kwamba kama wanapulizia dawa, kwa mfano, wanapulizia dawa Bunda, lazima ije Mwanza halafu irudi kule Bunda.

Mheshimiwa Spika, nataka kutoa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo. Pamoja na msaada wake, sasa waende mbali Zaidi, wafikirie kupata helicopter ambayo itaweza kutua mahali popote katika suala la umwagiliaji. Kwa sababu kuua ndege waharibifu kwa kutumia gharama kubwa kama hizi, kwamba kama Kahama hakuna uwanja wa ndege, kwa mfano, labda Ngara hakuna uwanja wa ndege, ndege mpaka ikatue Bukoba halafu ijazwe dawa, irudi Ngara, hili ni jambo ambalo tunaona kama Wizara inatumia gharama kubwa sana. Kwa hiyo, watumie helicopter.

Mheshimiwa Spika, vile vile miradi iliyopo, na wao wataweza kusafiri na ile ndege. Siku ikihitaji kumwagilia, itamwagilia; lakini msafiri na helicopter, miradi ni mingi, mtazeeka. Sasa hivi Mheshimiwa Bashe umechoka kweli kweli nakuona, alhamdulillah unafanya kazi, lakini lazima ujionee huruma. Utaacha hii nafasi, unachoka, wanakuja wengine tena. Kama kuna suala la kununua ndege, peleka maombi, leta hapa, bajeti imeongezeka, wakuruhusu ununue helikopta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza kuchangia. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala la umwagiliaji. Miradi ya umwagiliaji ndiyo pekee inaweza ikalinusuru Taifa hili. Ni kwamba, tumeona kilimo chetu sasa hivi kwa kutumia hali ya hewa ya mvua, mvua zinabadilika. Leo kanda ya ziwa mvua zinanyesha mwezi wa Tatu, wakati mahitaji yetu ya kupata maji, ni mwezi wa Tisa, wa Kumi, na wa Kumi na Moja. Tungekuwa tuna miradi ya umwagiliaji; na ninakushukuru kwenye bajeti hii umeiangalia sana kanda ya ziwa. Ushauri wangu kwa Wizara, Wizara hebu njooni tumwagilie maeneo yetu yanayofanyika katika irrigation kwa kutumia pipeline kutoka ziwani.

Mheshimiwa Spika, wenzetu Misri wanatumia maji haya haya ya Ziwa Victoria, lakini yanapita katika mto. Sisi wenye ziwa hatupati thamani ya maji haya, kwa sababu hii miradi ya irrigation pia ukichimba bwawa tunategemea mvua inyeshe, maji yajae ndiyo ukamwagilie, wakati ziwa tunalo. Kwa nini usipandishe maji katika milima, halafu ukafungulia mabomba watu wakamwagilia?

Mheshimiwa Spika, mfano, kwangu kuna mradi wa Isole, alikuja Mkurugenzi wa Umwagiliaji, Mr. Ray tumezunguka naye Sengerema, ameona ile miradi. Tunayo miradi mitano ya irrigation. Kuna Isole/Kishinda, pia tuna mradi mwingine ambao uko Rwenge, Rwenge - Kagunga - Shimaka; tuna mradi mwingine ambao unaanzia Sima, huo uko katika sehemu inaitwa Ishokeya. Huo ni mradi mkubwa sana wa irrigation, aliuona Mr. Ray kule. Vile vile tuna mradi wa Ibanda - Igaka ambao tunashirikiana na mwenzangu kutoka Geita, Mheshimiwa Kanyasu. Huu mradi umetangazwa, tunashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, pia tuna mradi wa Katunguru ambao na wenyewe ulikuwa umekwama. Tunakushukuru Mheshimiwa Bashe, leo kuna Mchina yuko kule anamalizia kazi. Sasa kuna na mradi ambao ulikuwa unataka design na kujengwa, ni mradi ambao unatoka Kashindaga – Butonga - Nyamizeze – Nyamazugo. Kule sisi tuna mradi wa maji na kuna matenki kule. Ukijenga tenki kubwa mlimani, sisi tutamwagilia kwa maji ya ziwa. Sasa tunakuomba miradi hii kwa sababu Mkurugenzi wako alipita kule, tuone kama safari hii na sisi Sengerema tutabahatika kupata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, la pili ni suala la ushirika. Ushirika tumeona kwenye hizi gharama za kupanga bei za pamba. Bei za pamba, Mheshimiwa Bashe unapanga pamoja na watu wako wa Wizara ya kilimo, lakini mnapanga na wanunuzi wa pamba, Wakuu wa Mikoa wanakwenda pale. Kwa nini sisi Wabunge tunaotoka kwenye mikoa inayolima pamba tusiwemo katika upangaji wa bei? Mnaficha nini? Hivi mkitualika sisi tukaja pale hizo siku tatu au nne, tukakaa tukaangalia hicho mnachokifanya, ili tuwe mabalozi, turudi kwa wananchi, lakini mnawachukua watu wanakwenda kuwa mabalozi wa pamba, wameshastaafu, sisi tuko kazini; mnatuachaje sisi kuwa mabalozi wa pamba? Mimi nakushangaa, sijui unafeli wapi mdogo wangu katika jambo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni sula la ushirika. Ushirika mnawatengea pesa pale, naona shilingi 20kwenye kila kilo. Sijui kuna AMCOS, sijui kuna nani mnawatengea, sasa huu ushirika uliofilisika; ushirika kama Nyanza, wakati unaanzishwa mwaka 1972, wakati huo Mwanza kwa Mkoa mzima wa ilikuwa na wananchi 760,000. Leo wananchi tuko 3,600,000. Ushirika huu umeshindikana, umeshakufa, unaung’ang’ania wa nini Mheshimiwa Bashe? Mwisho tuje tugombane humu ndani, una tu-lock sisi kuendelea. Tuna Ginnery Buyagwi iko pale, inatakiwa ukarabati, wewe mwenyewe ulikuja ukaona.

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Bashiru Ally Kakurwa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa iwe na afya.

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba suala la ushirika ni sera ya CCM na iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Tabasam unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Namheshimu sana bosi wangu, lakini kama kuna kitu kiko ICU tukiacha kusema kwamba mgonjwa huyu ana hali mbaya, kwa sababu tu kiko ndani ya sera, sasa hii ni hatari. Kwa hali hiyo, tunavyozungumza, sisi ushirika tunautaka, lakini uwe ushirika wenye manufaa. Kwa mfano, kama ushirika wa KACU, walijiondoa SHIRECU, lakini leo KACU ndiyo kanunua mbolea, viuatilifu na kila kitu. Kaenda kukopa, ni ushirika ambao hauna deni.

Mheshimiwa Spika, ushirika wetu wa Nyanza, tuna godown Dar es Salaam, leo zinaweka marumaru badala ya kuweka pamba; zinaweka mabati na nondo; tuna godown ziko Mwanza, Mheshimiwa Bashe alikuja akaona, leo wanaweka cement na magodoro. Pia tuna ofisi zetu za Nyanza, hata mimi nina ofisi kule ndani, zilikuwa ni ofisi za ushirika, lakini leo tunapangishwa sisi kama ofisi. Kuna mabenki na kila kitu. Kwa hiyo, ule ushirika hauwezekani tena.

Mheshimiwa Spika, leo Mwanza hawalimi pamba. Nyamagana sasa hivi ni Jiji, hawana hata nafasi ya kwenda kutengeneza makaburi. Hawa wanatakiwa ushirika wa nini tena? Ilemela hawana hata sehemu ya kulima pamba, ushirika wa nini? Ushirika sasa unatutaka sisi watu wa Sengerema na Buchosa, unamtaka mtu wa Misungwi, Kwimba, Ngudu na Magu. Pia ushirika huu wa Nyanza unavyouona, pesa wanazo kule, tumeomba tuletewe CEO pale, tuweze kuja kugawana sisi. Huyo Mrajisi anachukua pesa karibu Shilingi sita kwa kila kilo ya pamba; ya nini? Huyo Mrajisi anafanya kazi gani, wakati ushirika umekufa? Leo Nyanza hajanunua pamba miaka 23. Sera ya CCM; miaka 23! Pamba inanunuliwa na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, washirika tumekaa sisi wenye ushirika wetu, tuna hali mbaya Mheshimiwa Bashe. Unashindwaje kuvunja hii? Nakamata kule kwenye fungu lako, ukurasa wa 15 kwenye ushirika, nitakukamatia kule mdogo wangu. Sina jinsi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Najua kabisa wewe ni mzalendo, lakini kama hutakuja kusema unakuja kuugawa ushirika wa Nyanza, watu wamebakia kuwa walaji tu pale, wanakula pesa za Nyanza. Wewe mwenyewe njoo uje useme hapa, Nyanza inafanya kazi gani?

SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu, kengele ya pili ilishagonga. Ahsante sana.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naomba sekunde moja nimalizie mchango huu.

SPIKA: Ahsante sana. Kuna wenzio wameomba kuchangia nao, sasa inabidi uunge mkono hoja.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)