Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Nancy Hassan Nyalusi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hii iliyoko mezani.

Mheshimiwa Spika, nina mambo matatu; jambo la kwanza ni pongezi na Shukurani. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa maono na msukumo Mkubwa ambao ameuweka kwenye wizara ya kilimo. Pia tunampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Mkoa wa Iringa, tunaishukuru Serikali sana kwa mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi katika Wilaya ya Mufindi, Kata ya Nyororo. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha atuambie ni lini ujenzi wa kiwanda hicho utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili, ni ruzuku ya mbolea. Tunaishukuru sana Serikali kwa ruzuku ya mbolea, wananchi wanafurahia sana kwa jambo hilo. Tunaishukuru tena Serikali kwa sababu mwaka huu wametenga tena pesa kwa ajili ya mbolea ya ruzuku. Lakini msimu uliopita kulikuwa kuna changamoto nyingi ambazo zilitokea. Naomba kutoa mapendekezo yafuatayo ili kuweza kutatua changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, tunaomba mbolea zifike kwa wakati kabla ya msimu haujaanza. Kwa sababu mwaka jana mbolea ya kupandia ilichelewa hadi mahindi yamekwisha ota mbolea ya kupandia ndio inafika ambayo ilileta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi na kero kubwa sana. Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, tunaomba ziwekwe center ambazo wakulima wataweza kupata m,bolea kwa wepesi. Kwa sababu kwa mfano kule kwetu Mkoa wa Iringa, mwananchi alikuwa anatoka Mauninga karibuni kilometa 100 anafuata mbolea Iringa Mjini, ni mateso makubwa sana. Mwananchi anatoka Maduma anakwenda mpaka Mafinga Mjini ndio apate mbolea, ni mateso makubwa sana. Tunaomba ziwekwe hizo center na pia Mheshimiwa Waziri, mfumo wa ugawaji wa mbolea uendane na uhalisia wa maisha ya watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine ni usajili wa wakulima. Mheshimiwa Waziri, tunakuomba uanze usajili wa wakulima mapema kwa sababu suala la usajili sio dharura. Unaweza kuanza kuwasajili sasa hivi ili kuondoa usumbufu ambao ulikuwa unajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la nne; ni Mamlaka ya Mbolea Tanzania, Mfumo wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania, tunakuomba Mheshimiwa Waziri, ukaufanyie mapitio. Kwa sababu una mapungufu mengi ambayo mawakala wanalalamikia. Kwa hiyo, tunaomba ukafanye mapitio kwenye mfumo huo ili kutoa haya mapungufu na kuwaondolea mzigo mawakala. Mheshimiwa Bashe, tunaimani kubwa na wewe na tunaimani kwamba utatatua changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya tatu; ni stakabadhi ghalani, Serikali ina mpango wa kuingiza zao la mahindi kwenye mfumo wa stakabdhi ghalani katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Lakini Mheshimiwa Waziri anapohitimisha tunaomba atwambie amejipangaje? Kwa sababu tumeona kwamba kwenye zao la choroko na dengu kulikuwa kuna usumbufu mkubwa na changamoto nyingi. Je, amejipangaje kwenye huo mpango wake wa kuingiza zao la mahindi kwenye stakabadhi ghalani? Kwa sababu wakulima wana hofu na wanahitaji kuondolewa hofu hiyo ili waweze kupata faraja katika jitihada zao za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)