Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha ushauri na maoni yangu kuhusu mbolea ya ruzuku kwa Mafinga na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwamba kwa kuwa sisi tunalima mwaka mzima, basi mbolea ipatikane mwaka mzima na kwa ujazo tofauti. Ukienda mpaka wa Namanga utaona bidhaa zinazovuka, kati ya bidhaa kubwa inayovuka ni pamoja na viazi ambavyo asilimia kubwa vinalimwa mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.

Mheshimiwa Spika, tunazungumza kuhusu kuongeza ajira, eneo hili linatoa ajira kuanzia wakulima, wauzaji wa pembejeo lakini pia sekta ya usafirishaji kuanzia kufikisha pembejeo shambani na kusafirisha viazi. Yawezekana ni gharama kubwa na yawezekana mwelekeo ni kutoa ruzuku kwa ajili ya mazao ya chakula, kama hivyo ndivyo, basi walau hata kama haitakuwa 50%, basi iwe ruzuku hata ya 25%, kwa mfano mbolea ya shilingi 150,000 basi ipatikane japo kwa shilingi 100,000.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujazo, wapo wakulima wanalima kilimo cha kumwagilia na cha mabondeni kwa maana ya vinyungu, hawa wanahitaji mbolea kwa matumizi ya awamu tofauti, kuna wakati anahitaji mbolea ya ujazo wa kilo tano, kilo kumi, kilo 20 na kadhalika. Hii itawapunguzia usumbufu ambapo kwa sasa wakulima wetu wanalazimika kuchanga fedha na kununua mfuko mmoja na baadae kuanza kugawana kwa kupima kwenye visadolini.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Wizara kwa wasilisho la bajeti na ninaomba kuchangia kama ifuatavyo; kwanza tuokoe zao la mkonge na viwanda vyake.

Mheshimiwa Spika, katika kitabu cha hotuba ya Waziri ukurasa wa 11-14 imetaja mchango wa kilimo katika pato la Taifa kuwa ni 26.1% na kwamba kilimo kinachangia 65% ya malighafi za viwanda. Zao la mkonge ni moja ya zao ambalo linaweza kuchangia asilimia za mchango wa kilimo katika pato la Taifa. Mawazo ya aina hii nimeyawasilisha pia katika bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Spika, katika ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imetaja kuzalisha ajira milioni nane, ni wazi kuwa ajira hizi kwa kiasi kikubwa zitatokana na mnyororo wa thamani kuanzia katika malighafi za kutoka mashambani/kilimo hadi viwandani (agro-processing industry). Ajira hizi pamoja na viwandani itaendelea hadi sokoni. Ni masikitiko makubwa sana kwamba wakati tumeamua kufanya zao la mkonge kuwa zao la kimkakati, hakuna jitihada za makusudi za kulinda viwanda vya kuchakata zao la mkonge kwa maana ya kulinda soko. Ndani ya Serikali hakuna ufuatiliaji wa maagizo na maelekezo ya Waziri Mkuu ya Septemba, 2021 na rejea yake Novemba, 2021 kwamba Wizara inayohusika na mazingira kwa maana ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira izuie importation ya kamba za plastic ambazo kwa kiasi kikubwa mbali ya kuvuruga soko la kamba za kitani, lakini pia zinaathiri mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo ni matarajio yangu kwamba ikiwa Wizara ya Kilimo mnayo dhamana ya kukuza kilimo na kuongeza mchango wa malighafi za viwandani, basi pia mnao wajibu wa kuwa kiongozi wa kulinda viwanda ambavyo vinatumia malighafi za kilimo. Hivyo kama Wizara ya Kilimo mnayo nafasi kubwa ya kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira kuhakikisha kuwa zuio hilo linasimamiwa ili kuwalinda wakulima na kulinda viwanda na ajira za Watanzania kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Pili ni kuhusu vijana waliohudhuria mafunzo ya kilimo nchini Israel, je, wamesahaulika, tumewatelekeza au hawana tija? Kwa miaka kadhaa kama Taifa tumekuwa tukiwapeleka baadhi ya vijana waliomaliza SUA kwenda kuhudhuria mafunzo ya miezi takribani kumi na moja, hata hivyo wakirudi hatuwatumii, hatujui wako wapi? Kwa nini vijana hawa tusingeanza nao kwenye BBT hata kuwafanya ndio viongozi wa wengine? Katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 75 amezungumzia mpango wa mashamba makubwa ya pamoja, nashauri kwa kuwa tayari tuna vijana waliopata maarifa ya hali ya juu ya kilimo huko Israel tuone kwa namna gani tutawatumia, sio sahihi na ni kupoteza rasilimali watu na fedha kuwaaacha hawa vijana wanaelea tu.

Mheshimiwa Spika, swali dogo, je, Wizara inawatambua, wako wangapi, wako wapi na wanafanya nini? Ndio maana baadhi ya watu wanaona BBT ni siasa, haya siwezi kuyasema Bungeni live bali nawaletea kwa maandishi, je, kama BBT sio siasa? Kwa nini hatuwatumii hawa vijana, wako idle wakati skills wanazo, kwa nini tutafute wapya ambao pengine kujiunga kwao na BBT ni kwa sababu wako desperate, hawana kazi, kwa sababu wamekosa ajira, hawana mbadala ndio maana wakakimbilia BBT.

Mheshimiwa Spika, je, BBT ni siasa au business as usual kama tulivyoshuhudia ya Kilimo Kwanza na kadhalika? Kama sio siasa basi ni matarajio yangu kwamba tuta-make maximum use of the available resources wakiwemo hawa vijana waliopata mafunzo Israel. Na ninatamani sana Waziri katika majumuisho aseme jambo kuhusu hawa vijana. Labda hii programu haikuwa na baraka za Wizara, labda kwa utaalam wenu mnaona haiwahusu, lakini iwe ni kilimo au yeyote aliyeratibu programu hii, bado mwisho wa siku ni Serikali katika ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushauri wangu kwa Wizara, Waziri atuambie hatma ya hawa vijana, vinginevyo kwangu mimi nitaona hata BBT it is business as usual, it is politics. Na kuthibitisha kwamba kama Serikali tunawatambua hawa vijana soma hii meseji; “Kwanza Waziri wa Kilimo Josephat Hasunga wa Songwe aliwahi kuja Israel na akaahidi mambo mengi tu endapo tutarudi Tanzania, pili, Naibu Waziri Anthony Mavunde mwaka jana alihudhuria mahafali. Tatu kuna siku alikuwa Dodoma Mavunde alisema BBT itakuchua wanafunzi waliotoka Israel sijui wamemsaliti akina nani huko juu! Nne, Naibu Waziri Katambi aliwakaribisha Bungeni kama wageni wake siku fulani Bunge lililopita."

Mheshimiwa Spika, kuhitimisha suala hili, ni wazi Wizara na Serikali kwa ujumla inawatambua vijana hao, basi tuone namna ya kufanya, kuwatumia ili wawe na mchango katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, mafuta ya kula na kuondolewa kwa ushuru kutoka 35% hadi 0% je imesaidia kukua kwa kilimo cha mbegu za uzalishaji mafuta ya kula au tumenufaisha ma- tycoon wa biashara ya mafuta ya kula?

Mheshimiwa Spika, suala hili pamoja na kuwa ni la Viwanda na Biashara pamoja na Hazina, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wenzetu wa Kilimo wanao wajibu wa kwanza kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mafuta ya kula na hata kuuza nje. Lakini kwa mshangao na masikitiko makubwa mwaka wa fedha tunaoumaliza huu wa 2022/2023, Serikali iliondoa ushuru wa the so called mafuta ghafi kutoka 35% hadi 0% kwa mwaka mmoja kwa waagizaji kutoka nje. Maamuzi haya baadhi yetu tuliyapinga na kushauri kwamba hata kama ni ahueni basi walau iende kwa hatua na kwa awamu, kwa kupunguza hata hadi 15%.

Mheshimiwa Spika, ilitolewa hoja kwamba ingesaidia kupunguza bei ya mafuta ya kula, tukiwa honest wala haikuwa na mashiko, sana sana tumewanufaisha wafanyabiashara wakubwa, kwa sababu kwanza hawaingizi crude kama walivyodai, wanaingiza refined na kufanya packaging, matokeo yake tumewaumiza wakulima wetu wa alizeti, je, sisi kama Wizara ya Kilimo tumekuza kilimo au tumekirudisha nyuma?

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa azma ya Taifa hili kujitosheleza kwa mafuta ya kula ina safari ndefu sana kwa sababu wafanya maamuzi wanaangalia maslahi binafsi na sio maslahi ya walio wengi ambao ni wakulima wetu. Leo hii morale ya kulima alizeti imeshuka mno kutokana na bei ya alizeti kuwa ndogo. Kuna kichaka watu wanajificha ooh tumeondoa ili kupunguza makali ya bei, makali ya bei yamekuja kupungua baada ya wananchi kuanza kuvuna alizeti zao, kwa hiyo kuondoa ushuru kutoka 35% hadi 0% hakujawa na faida sio kwa mlaji wa mwisho wala mkulima wa alizeti. Kama Wizara mnapaswa kuwa na wivu na kutetea kilimo na hasa kwa mazao ambayo yatalisaidia Taifa kuondokana na kuagiza baadhi ya bidhaa kutoka nje kama ilivyo kwa mafuta ya kula. Yafaa sote kwa pamoja tuwe na dhamira moja na tuone aibu kuendelea kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, na ndio maana mwaka jana nilishauri, washirikisheni JKT, mtaona matokeo in just two years.

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu zinazoendelea kule Kigoma za kilimo cha michikichi. Ninaamini tukiwawezesha JKT tutavuka, lazima tufike wakati tuwe na uthubutu, tuwe wakweli wa nafsi, sio sawa kama Taifa kuendelea kutumia zaidi ya USD milioni 300 kuagiza mafuta ya kule, tuone aibu kama Taifa. Tukiwekeza katika JKT sio tu kwamba tutaokoa fedha za kigeni, lakini pia tutauza mafuta katika nchi jirani za DRC, Malawi, Zambia na hata Burundi na Rwanda. Nchi hizi zinategemea mafuta ya kula kutoka Malaysia, tukizalisha tunalo soko la ndani lakini pia soko hata ndani ya EAC na baadhi ya nchi za SADC.

Mheshimiwa Spika, kule Chita, nashauri Serikali ikajifunze kilimo cha mpunga chini ya JKT, ni aibu sisi kutoa vibali eti kuagiza mchele tani 90,000; haya ni mambo tunapaswa kuyakataa kwa vitendo, hata programu ya BBT awamu ya pili, kama tuna dhamira njema na ya dhati, nashauri mngehusisha vijana waliopata mafunzo JKT na usimamizi ungefanywa kwa ushirikiano wa ofisi hizi tatu, Kilimo, Kazi na Ajira na JKT.

Mheshimiwa Spika, usalama wa mbegu na mbegu bora; katika ukurasa wa 119 wa hotuba ya Waziri ameeleza kuhusu suala la utafiti wa mbegu bora, ninashauri tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa mbegu bora na salama. Mfumo uliopo kwa hakika sio salama katika suala la usalama wa chakula na usalama wa Taifa. Nashauri pia tuhusishe vyombo vyetu hasa JKT katika kufanya tafiti za mbegu bora, mimi naamini kwamba innovation mara nyingine inatokea kwenye vyombo vya ulinzi na usalama hasa majeshi, simaanishi kwamba tuwaachie wao, hapana, tuwashirikishe, tushirikiane na ndio maana nawasihi ndugu zangu wa Kilimo mkatembelee Chita, kipo kitu mtajifunza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.