Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza kuhusu miradi ya umwagiliaji Jimbo la Singida Kaskazini, Bwawa la Mgori limejaa tope na halina miundombinu ya umwagiliaji. Naishukuru Wizara kwa kutuma timu ya wataalam kuhakikisha bwawa hili linafanyiwa kazi ili liweze kusaidia uzalishaji kwani ni eneo lenye ardhi nzuri kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mahindi, vitunguu karanga na alizeti. Bwawa hili litanufaisha hekta 1000 endapo litapatiwa miundombinu ya umwagiliaji.
Aidha, katika Jimbo la Singida Kaskazini tunayo Mabwawa ya Ntambuko, Kisisi, Masoghweda, Endesh na Mikuyu ambayo yanafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji endapo yatawekewa miundombinu yake. Pia ardhi yake ni nzuri kwa uzalishaji wa mazao anuai hasa mahindi, alizeti, vitunguu na mbogamboga. Naiomba Wizara iyatembelee na kuyafanyia upembuzi yakinifu na kuyajengea miundombinu yaweze kutumika kwa umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ina upungufu wa watumishi 93 wa Idara ya Kilimo, naomba kupatiwa watumishi ili kazi ziweze kufanyika ipasavyo; idara iwezeshwe usafiri wa gari ili iweze kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kilimo kwa urahisi. Gari lililopo ni kuukuu na ni bovu. Pia tunalo shamba la mbegu lenye hekta 600; naomba Wizara iweke mkakati wa kuzalisha mbegu za mazao hususan mahindi na alizeti ili kuepuka gharama kubwa tunazopata kusafirisha mbegu kutoka maeneo ya mbali.
Mheshimiwa Spika, zao la pamba lirejeshwe katika mkoa wa Singida kwani tunacho Kiwanda cha Pamba Mkoani Singida ambacho kinahudumia mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.