Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia hoja ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaisimamia Wizara hii na niwapongeze Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ni Wizara wezeshi na katika suala zima la utambuzi wa maeneo kwa ajili ya kilimo na shughuli zingine, Tume ya Mipango ya Ardhi ndio kazi yake. Ni jukumu lao kwanza la shughuli katika tume kuhakikisha kwamba wanaratibu na kuwezesha mpango wa matumizi ya ardhi yaweze kufanyika katika maeneo na kwa kipindi kifupi katika kutambua maeneo kwa ajili ya kilimo toka Mheshimiwa Rais alipowekeza na kujikita kwenye kilimo. Jumla ya hekta ambazo zimeshatambuliwa mpaka sasa ni 2,160,076. Zimetengwa kwa ajili ya kilimo kutoka katika vijiji 1,059, kati ya vijiji 2,765 ambavyo vimewekewa mpango wa matumizi. Mheshimiwa Josephine Genzabuke alizungumzia habari ya kuwawezesha wakulima na ndio hasa dhamira njema ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapowapimia wakulima maeneo yao maana yake kwanza tunaongeza thamani ya ile ardhi yao. Inapoongezwa thamani kwa kupewa ile hati, tunamwezesha pia kuondokana na migogoro, lakini tunampa uwezo wa kuitumia ile haki kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo. Mpaka sasa tunavyozungumza jumla ya hati 1,318 zimetumika, zile hati miliki za kimila zimetumika katika mabenki kutoka kwenye halmashauri 10 katika mabenki ambayo yametoa jumla ya bilioni 60, milioni 164 zimetolewa kama mkopo kutokana na hizi hati miliki za kimila.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa maana nyingine Mheshimiwa Genzabuke alivyoliongelea, Serikali inaliangalia hili na tunajua wakulima wako zaidi ya asilimia 65 kwa sensa ya 2022. Kwa maana hiyo ni kwamba unapowekeza kwenye kilimo lazima pia umwangalie mkulima na kumwangalia kwake ni kuhakikisha kwamba ile salama ya miliki yake inakuwepo na ndio maana tunakazania katika suala zima la kuweka mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo, ili kila kipande cha ardhi kipangiwe matumizi. Once ukishakipangia jukumu lingine linakuwa ni la kukitumia.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa kilimo nawapongeza sana kwa sababu katika haya maeneo ambayo tumeyaainisha wanalo jukumu la kupima ule udongo kuona unafaa kwa kilimo gani. Kuna Mbunge mmoja amechangia akawa anasema tuwe tunaangalia na udongo unafaa kwa namna gani ili katika mazao tuangalie kikanda. Nadhani hili Wizara wameshalichukua na wanalifanyia kazi. Sisi kama Wizara ya Ardhi jukumu letu ni kuhakikisha maeneo yale yanapangiwa mpango, yanatengwa kwa ajili ya kilimo ili wao waangalie udongo uko namna gani. unafaa kwa kilimo kipi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais katika hii program ambayo wanaendelea nayo ya BBT kwa vijana, lakini hili hajalianza leo, tuangalie pia hata kipindi kilichopita, Ofisi ya Waziri Mkuu imekwenda katika halmashauri 117 kati ya halmashauri 184, ikifundisha vijana na wamefundishwa vijana zaidi 12,000 kwa ajili ya kilimo cha kitalu nyumba. Kwa sababu tunatambua vijana wako mjini na vijijini na si wote watakaoweza kwenda vijijini kwa ajili ya kilimo ambacho kinakwenda kufanyika sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana wanawekeza pia, Serikali inawekeza kwenye kilimo cha kitalu nyumba kwa maana ya ile Green House. Sasa hawa vijana 12,000 na zaidi ambao wameshapatiwa mafunzo hayo ni jukumu letu katika halmashauri zetu kuhakikisha kwamba ujuzi ule wanaulea, walioko mjini wakaendeleza kilimo, wanaweza wakafanya kilimo cha horticulture, wakati wenzao wanaendelea huku katika vijiji na maeneo mengine, maana yake hawa huku tayari wanao na wanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba, Serikali inaangalia kwa uhakika namna ya kutumia vizuri ardhi yetu na kutambua na kwa kupima na kwa kuweka mpango madhubuti. Jukumu letu sasa kama halmashauri kama Wizara huko tuliko, tuone namna bora ya kuhakikisha mpango wa matumizi kwa wenye mamlaka za upangaji, tunaipa kipaumbele sekta ya kilimo ambayo ndio sekta inayochukua zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wamewekeza kule. Kwa hiyo hili tutalifanya kwa sababu tunajua ni jukumu letu kama Serikali kuwezesha Watanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)