Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi kwanza kabisa ningependa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mema anayoyafanya na kwa neema aliyoileta ndani ya Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki. Lakini pia nimpongeze kaka yangu Aweso, wana Morogoro Kusini Mashariki wanakupenda sana.

Na nikwambie, kwa sababu wanajua uwezo wako ukitaka kuongeza wanne karibu Morogoro Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza timu yangu ya Simba kwa kuendelea kufa kiume, na naamini tutafufuka kiume, na leo timu yao inacheza tuiombee mema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendele kuipongeza Wizara ya Maji, hapa niseme kidogo mimi wazazi wangu wote walikuwa wafanyakazi wa Wizara ya Maji, kwa hiyo mimi nimelelewa na Wizara ya Maji. Kwetu sisi kwenye Kata ya Tegetero ambako tunazalisha mradi wa Morong’anya. Na kwa mradi huu niendelee tena kumpongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, mradi wa bilioni 23, huu mradi unakwenda kulisha vijiji zaidi ya 24. Vilevile Mama Samia hajawa mchoyo akaleta pale Kata yangu ya Mkambarani, mradi wa bilioni 4, nani kama Mama Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niongee; wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Wizara ya Maji imefanya makubwa sana kwenye Tarafa yangu ya Mikese na Tarafa ya Mkuyuni. Sasa tunakwenda kwenye Tarafa ya Ngerengere ambapo ndipo pana mlango wa kupeleka maji zaidi ya asilimia 50 Dar es salaam, hii mimi inanitia aibu kusema sana kwa sababu zaidi ya asilimia 50 maji yanakwenda Dar es Salaam, wana Dar es Salaam wanakunywa maji baridi ambayo tunatunza sisi wana Morogoro Vijijini, Tarafa ya Ngerengere inapata maji kwa asilimia 31. Na hiyo asilimia 31 maji yote ni chumvi, na asilimia 69 watu hawapati maji. Sasa hapa ndugu yangu Aweso ndio utakosa mke Morogoro Vijijini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme ukweli tunamuona ndugu yangu Aweso anasema wali wa kushiba unaonekana kwenye sinia lakini niongee ukweli wana Ngerengere kwenye hiyo sinia bado hawajaiona mpaka leo. Nikuombe kaka yangu Aweso, najua unaweza. Leo hii tunaona umetangaza Mradi wa Kidunda ambao unatoka kwenye Tarafa ya Ngerengere, lakini huu mradi wa Kidunda sisi kwetu hatuna faida nao. Muda wa ukame tutaona mnapanda helkopta mpaka vijijini kutuswaga kule, sisi tunaowalindia maji mpate watu wa Dar es Salaam lakini sisi kama wana Tarafa ya Ngerengere hatujui maji baridim maji yote tunayokunywa ni ya chumvi. Basi angalia ule mradi ambao unakweNda Dar es Salaam tuma wataalamu wako na sisi basi tupate maji baridi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo hii ninavyoongea katika Kata ya Tununguo hawana mradi wowote tangu uhuru umeanza, kwa hiyo sisi tunakunywa maji tunayaita maji ya Nzasa, yale maji meupe. Kweli! zama hizi! zama za Rais jembe, Rais shupavu Mama Samia Suluhu Hassan, nikwambie kaka yangu tunajua, tunajua nguvu ya Mama Samia na tunajua nguvu ya Chama Cha Mapinduzi, hatuwezi kuona sisi tunakunywa maji ya Nzasa halafu tunawapelekea maji Dar es Salaam wanakunywa maji baridi, hilo ndugu yangu leo naweza nikaondoka na shilingi yako nikaenda nayo Ngerengere.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kumpa ndugu yangu anayechangia kwamba sera ya maji inasema. Pale ambapo maji yanaanzia kwenye chanzo cha maji wale watumiaji wanaozunguka eneo lile anatakiwa kupata maji kwa hiyo huo mradi wake watu wake wanapaswa kupata maji kama wale wa mradi unaopeleka maji Arusha pale Hai, nao wanatakiwa kupata maji. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taletale.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea taarifa ya ndugu yangu Saashisha lakini naendelea kusema kwamba nakumbuka Mheshimiwa Waziri alikuja kwenye kata yetu ya Tegetero wakati anafuata kutembelea mradi wetu wa Morong’anya pale ule mradi wa Morong’anya unapoanzia kwenye kata ya Tegetero, kata nzima ya Tegetero haina mradi wa maji. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri umeacha maagizo na sisi pale katika kata ya Tegetero tuwe wanufaiika. Basi hicho kikafanyike kwenye ule mradi wa Kidunda. Leo hii mimi naona maajabu na miujiza, ule mradi wa Kidunda yale maji hauendi kuyamwaga baharini unakwenda kuwauzia wananchi. Pale hatupati shilingi kumi kipande, tumeridhika Alhamdulillah sasa basi hata tukose na maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, mmetunyima shilingi kumi kipande basi tupeni maji. Tunaomba Tarafa ya Ngeregere nayo iwe sehemu ya unafaika ipate maji baridi Mheshimiwa Aweso. Hakuna kitu kinachoniuma, mimi wakati naingia kwenye nafasi hii ya Ubunge ku ukweli kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Alhamdulillah Rabbil Alamin. (Makofi)