Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji Pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa ambayo wanafanya hasa katika upelekaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni siku chache tu zimepita tangu Mheshimiwa Waziri aje kwenye Mkoa wetu wa Songwe na amekuja pale Mlowo ametupatia mradi mkubwa wa shilingi milioni 601. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wenzangu wa kata ya Mlowo kukushukuru sana. Lakini pia tunafahamu kwamba kwenye Mkoa wetu wa Songwe tunao mradi mkubwa sana wa maji wa kutoa maji kwenye Mto Momba kuyasambaza kwenye Miji ya Tunduma, Vwawa Pamoja na na mji wa Mlowo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwamba kwneye bajeti ya mwaka jana alutuahidi kwamba mradi huo ungeanza mwaka huu, lakini mpaka sasa hivi mradi huo haujaanza. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri mradi huo uweze kuanza. Sote tunafahamu kwamba azma kubwa ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejionesha kwa namna ambavyo anavyotafuta fedha na kuzipeleka kwenye miradi mikubwa ya maji. Miongoni mwa Wizara ambazo Mheshimiwa Rais amepleka fedha nyingi ni Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima azma hiyo njema ambayo anayo iendane sambamba na kuondoa vikwazo vyote ambavyo vinaweza vikachelewesha azma ambayo anayo Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu miongoni mwa matatizo makubwa ambayo tunayo kwneye Wizara ya Maji, na niseme kwamba ni jambo ambalo bado halijapewa umuhimu na Wizara, ni suala la upotevu mkubwa wa maji; hii ni changamoto. Hata ukiangalia, kwenye Ripoti ya EWURA ambayo imetolewa ya mwaka 2021 imeonesha namna gani ambavyo mamalaka mbalimbali za maji hapa nchini zina kiwango kikubwa sana cha upotevu wa maji. Hali hiyo inasababisha kwamba wananchi wanakosa maji lakini vilevile Serikali inapoteza mapato mengi kutokana na tatizo hilo la kutokudhibiti hali ya upotevu wa maji katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika hiyo ripoti ya EWURA, na sisi tunafahamu kwamba kiwango cha kimataifa cha upotevu wa maji ambacho kinakubalika duniani kote ni asilimia 20, lakini mamlaka nyingi za maji hapa Tanzania zimevuka hicho kiwango cha asilimi 20. Nikianza, mamlaka namba moja ambayo inaongoza kwa upotevu mkubwa wa maji ni Mamlaka ya Mbozi kwenye Mkoa wa Songwe, Mkoa ambao mimi natoka. Ile ripoti imezungumza kwamba kwenye Mji wa Vwawa Pamoja na Mji wa Mlowo ndiko kwenye changamoto kunbwa sana ya upotevu wa maji. Ukiangalia kwenye hii miji mikubwa ndiko ambako shida ya maji ni kubwa sana. Hata huo mradi ambao tunauomba wa kuoa maji Momba ni kuja ku–cover hili gap la changamoto ya maji katika huu Miji ya Tunduma, Vwawa Pamoja na Mji wa Mlowo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu mojawapo kubwa ni uchakavu wa mabomba; na ninaamini kwamba hiyo changamoto haipo tu kwenye mkoa wa Songwe ni nchi yote kuna uchakavu mkubwa sana wa miundombinu. Lakini ukiacha kwenye Halmashauri hiyo ya Mbozi kuna Mkoa wa Arusha, wao upotevu wa maji ni asilimia 51, Dar es salaam 39, Lindi 37, Mwanza 36, Moshi peke yao ndio wako kwenye 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa ni kwamba ni lazima sasa Serikali kwa maana ya Mheshimiwa Waziri uje na mkakati Madhubuti wa kumaliza tatizo la upotevu wa maji katika nchi yetu ya Tanzania. Mheshimiwa Waziri umesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge wote wameonesha namna gani ambavyo kwanza tunakuamini na tuajua kwamba wewe ni jembe kweli kweli. Kama Mheshimiwa Waziri umeweza kudhibiti mabomba ambayo yanapaa usiku na sasa hivi yanatoa maji mimi naamini Mheshimiwa Waziri huwezi kushindwa kukabiliana na tatizo la upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe ushauri wangu katika maeneo machache. Ushauri wangu wa kwanza, niombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hii ni bajeti mpya jambo la kwanza ambalo nataka nishauri Mheshimiwa Waziri kuwe na ajenda maalumu ya kudhibiti suala la upotevu wa maji. Niombe Wizara ibebe jambo hili kama ajenda ili fedha za Serikali zisipotee, lakini vile vile wananchi wapate maji kwa wakati, na ile azma ambayo Mheshimiwa Rais anayo ya kumtua ndoo mwanamke kichwani iweze kutekelezwa. Lakini jambo la pili, nataka niishauri Wizara ifanye utafiti wa kina nchi nzima ili kuweza kubaini maeneo yote ambayo yana uchakavu wa mabomba ya maji. Mimi naamini wakishafanya utafiti, kwa sababu tayari tunayo taarifa EWURA, itasaidia sana kuweza kujua ukubwa wa tatizo uko vipi ili Wizara iweze kujipanga kuweza kukabiliana na hiyo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la tatu, niishauri Wizara itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kukarabati miundombinu yote nchini Tanzania. Katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umetaja miradi mikubwa mbalimbali ambayo mmeifanya na ambayo mnakwenda kuifanya kwenye mwaka huu wa fedha. Miradi hiyo tukiendelea kutenga, tukijenga miradi mikubwa ya maji kama hatutengi bajeti kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya maji bado tatizo la maji litabaki pale pale. Kwa hiyo niombe tuanze kutenga bajeti ili tuweze kuzisaidia zile mamlaka ambazo zinashughulika na matatizo ya maji katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo jingine, nadhani ni wakati muafaka sasa tuhame kwenye mfumo wa kutumia bili za maji. Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukishauri sana kwa miaka mingi, kwamba tuanzishe luku za maji. Kwani changamoto ya kuwa na luku za maji ni nini? Kama kwenye umeme tumefanikiwa kwa nini kwenye maji tushindwe? leo hii kuna changamoto kubwa sana wananchi wanalalamika kwanza wanabambikiziwa bili za maji. Leo hii kuna taasisi zina madeni kubwa ya maji. Mwarobaini wa haya yote ni sisi kuwa na luku za maji kama ambavyo tuna luku za kwenye umeme tuwe na luku za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini hili likifanikiwa, tutaondoa tatizo kubwa la ukosefu wa maji na changamoto kubwa ya fedha za Serikali kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu, watumishi wake huko mikoani wana imani kubwa sana naye. Kwenye Mkoa wangu wa Songwe mara zote nikiongea na watumishi, kwa maana ya Mameneja, wale wa Mikoa, Mameneja wa Wilaya, mara zote wananiambia kwamba, Mheshimiwa Shonza tunaomba pamoja na yote, msiache kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu, msiache kumshauri kwa sababu, jamaa anafanya kazi kubwa sana, ndio kauli yao siku zote. Kwa hiyo, hii inaonesha watumishi wa Mheshimiwa Waziri kule chini wana imani kubwa sana naye. Nimwombe Waziri jambo moja, wanazo changamoto kubwa ikiwemo changamoto ya ukosefu wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unakuta mabomba yamepasuka sehemu, kuna changamoto sehemu, lakini wanashindwa kufika kwa sababu hakuna magari. Hivi juzi kuna mtumishi mmoja wa Wizara amefariki kwa sababu ya kukosa usafiri. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili katika bajeti yake ya mwaka huu anunue magari, kama ambavyo wamefanya kwenye elimu, kama ambavyo wenzetu wa TARURA wamefanya na kwenye afya, naamini hata kwenye Wizara ya Maji anaweza kuwapatia vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa sababu tunajua kwamba, Waziri ni mtu wa kazi, nimwombe tu, tumekuwa tukimwona mara kwa mara akishughulika na wakandarasi na mameneja ambao hawafanyi kazi yao ipasavyo; nimwombe Mheshimiwa Waziri aweke target kwamba, kigezo mojawapo cha mtu kuwa promoted kwenye kazi yake ni kudhibiti tatizo la upotevu wa maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)