Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ambae ametujalia afya njema na amekuwa akitujalia uhai. Naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hakika asilimia 96 ya fedha zilizotoka ni kubwa sana. Wabunge wa muda mrefu wataona ni muujiza kidogo kwamba siyo rahisi fedha nyingi kiasi hicho zitoke kwa pamoja kwa ajili ya miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninamshukuru Mheshimiwa Waziri. Ndugu yangu, Mheshimiwa Aweso, amekuwa akifanya kazi kubwa na Naibu Waziri wake, lakini pamoja na kazi kubwa leo itabidi niseme maneno machache kidogo. Nashukuru kwa mradi wa Farkwa, mradi mkubwa kabisa ambao naamini unaweza kutosheleza maji Dodoma. Changamoto ni moja tu katika mradi ule, andiko la mradi ule linaonesha maji yale yanakuja Dodoma maana yake sisi Chemba hatuna tunachopata katika mradi mkubwa ule. Sasa sijui hao walioandika wanawaza nini, yaani sisi tuna ng’ombe tunamlisha, tunakamua maziwa, tunapeleka watu wakanywe sisi tusipate, hii haiwezekani!
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishasema mara kadhaa, nimesema kwenye vikao vya ndani, lakini bado kila kikao mnaeleza maji haya ni kwa ajili ya Dodoma. Sasa sisi wananchi wa Chemba kwa nini tuwe na lile bwawa, la nini, linatusaidia nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri alisema ndugu yangu pale kwamba na yeye kwenye bwawa lake maelekezo ni hayo hayo, kwamba maji yanapatikana kwenye Jimbo lake lakini eti maji hayo yakatumike sehemu nyingine, hii haikubaliki. Ninataka niwahakikishie Mheshimiwa Waziri, mkiweka mabomba pale tutaenda na vijana wetu kwenda kuyakata, kwanza tuanze kutumia sisi halafu ndiyo watu wengine waende kutumia. Mheshimiwa Waziri, naomba ninukuliwe hivyo na hivyo ndivyo ninavyoamini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nina jambo la pili, umekuwa ukitupa miradi mingi sana ya maji na Chemba ni moja ya maeneo ambayo yanapata miradi mingi ya maji,
2021/2022 tulipata visima 11 lakini mpaka leo kwenye visima hivyo vilivyochimbwa ni vitatu. Tume-carry mwaka huu tulikuwa na visima vitano, hakuna kilichochimbwa mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini tuje hapa kwenye bajeti tujadiliane kwamba bwana tumekupa visima hivi, mimi niende vijijini nikaseme halafu fedha hizo, yaani visima hivyo havipo, hii haiwezi kuwa sawa. Mimi nafahamu namna ambavyo ninyi ni wachapakazi na mnafahamu nimetembea kila mahali kuhakikisha – na mimi naambiwa fedha zimetoka asilimia 96, ukiwauliza Wakandarasi kwangu wanasema hawajapata fedha ndiyo maana hawatekelezi miradi, hili jambo linaumiza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninafahamu kwamba mkiniambia kuna maji naenda kule kuwaambia ndugu zangu hapa kwenye Kijiji X maji yanakuja. Sasa nabaki naonekana mimi Mbunge mwongo wakati fedha tumepitisha hapa lakini kule hazifiki. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, ninafahamu namna ambavyo unafanya kazi vizuri, katika hili kidogo tunaweza kupishana kwa nia njema zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi miwili ya siku nyingi sana,Mradi wa Machije ambao una milioni 700 na mradi wa Chandama ambao una milioni 500. Mradi huu ulikuwa ni kabla RUWASA haijaanzishwa, mpaka leo mkandarasi kaweka bango hakuna kinachoendelea na kila siku tunau-carry over kwenye bajeti nyingine. Maana yake ni nini? uki-carry over unanipunguzia mimi ceiling ya kuendeleza miradi mingine. Wakati mwingine ukisema sana unaonekana kama unaleta vurugu. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri, mimi ni katika watu wanaokupenda sana na kukuamini, unafanya kazi kubwa, lakini wakandarasi wa namna hii wa nini? Na kwa nini iwe Chemba tu, kwa nini kwamba Chemba ndiyo miradi haiwezi kukamilika? Nataka nikuombe sana uingilie. Nikuombe baada ya kumaliza bajeti yako hii, najua tutakupitishia vizuri, twende kule ukamalizie na wewe hii miradi ambayo inakera zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la muhimu sana na hili ni la nchi nzima kwamba ni lazima tuweke sera ya uhakika. Amesema Mheshimiwa Taletale kwamba pale kwake upatikanaji wa maji ni asilimia 31, yapo maeneo upatikanaji wa maji ni asilimia 92, nchi hii moja haikubaliki. Wewe mwenyewe mara kadhaa umesema kupata maji ni haki ya mwananchi yeyote yule, haikubaliki! Kwangu pia ni asilimia 36, ukienda Jimbo la jirani ni asilimia 72.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima hao wanaopanga bajeti waangalie namna gani wanaweza walau ku-balance ili maeneo yote haya tuwe na uwiano unaofanana, walau unaokaribiana, hii haikubaliki. Kwamba una asilimia 36, mlipakodi huyohuyo kuna mlipakodi mwingine ambaye ana asilimia 92 na huyo mwenye asilimia 92 ndiye anayepewa miradi mikubwa mingi zaidi ya maji, haya mambo lazima tuyaweke sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima kuwe na mpangilio na uwiano wa namna gani tunaweza kugawana hizi rasilimali za nchi yetu haiko sawa kabisa, niliomba kulisema hilo ili wakati mwingine muangalie namna ambavyo tunaweza kwenda mbele kwa uelewano mzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye miradi ya UVIKO walinunua magari na Mheshimiwa Waziri tulikubaliana, tuliongea vizuri, kwamba kwa sababu Chemba kuna changamoto kubwa ya maji kuliko eneo lolote la Dodoma magari yale yakaanzie Chemba. Ninataka wakati unajumuisha ujibu maswali mawili maana kuna changamoto kidogo, utaniambia tangu yamekuja yamechimba visima vingapi. Maana lile gari tukimpa raia mwingine atachimba visima 100 kwa mwaka, lakini likiwa Serikalini linachimba visima 10 kwa mwaka mzima, haiwezi kuwa sawa na tija yake itakuwa ni ndogo sana, lazima tufike mahali tuangalie namna sahihi na bora ya kuyatumia hayo magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mara kadhaa nimekusikia ukisema kwamba yako maeneo ambayo ukichimba maji ni ngumu kuyapata na moja ya maeneo hayo ni la Chemba. Tuna mradi wa Chemchemi ya Ntomoko kule, kuna eneo la pale Igunga, kidogo kilometa kama tano, sita hivi. Tumechimba mara nne hatujapata maji lakini tunaweza kuyaleta pale kwa gharama ndogo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana, unajua namna ambavyo nakuheshimu, najua wewe ni mdogo wangu, lakini naomba katika hili tuweze kusaidiana. Hatuwezi kuendelea kila mwaka kuja hapa Bungeni mimi nisimame niseme upatikanaji wa maji ni asilimia 32 na mwakani uwe asilimia 32, hii haiwezi kukubalika kabisa na uwezekano wa kupanda unakuwa ni mdogo kwa sababu tunapitisha miradi ambayo haitekelezwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naomba nitumie nafasi hii kukushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)