Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Wizara Maji. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya katika kuhakikisha kwamba sehemu nyingi zinaanza kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Aweso kwa kazi kubwa anazofanya, anayaishi yale maneno yake ambayo amekuwa akiyazungumza kila siku. Pongezi hizo ziende pia kwa Naibu Waziri kwa kazi wanazofanya pamoja na kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu na wasaidizi wake. Kipekee nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Bwana Clement kwa kazi kubwa anazofanya kuhakikisha kwamba anawasimamia mameneja wa mikoa na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee pia nimpongeze sana dada yetu Engineer Miriam Meneja wa Mkoa wa Simiyu kwa kazi kubwa anazofanya. Kwa kweli anatupa heshima kubwa sana kuhakikisha kwamba sehemu kubwa tunaendelea kupata maji pamoja na Meneja wangu wa Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa alilofanya kuhakikisha kwamba wanaleta magari ya kuchimba visima katika mikoa yetu. Leo hapa naomba sasa nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba tumepokea gari katika Mkoa wa Simiyu tuneomba hizi gari sasa zikalete matokeo chanya kwa Watanzania. Tusinunue gari kuja kuzi-park, hakikisheni mnapanga bajeti kwa ajili ya kuendeleza gari hizi kwa ajili ya mitambo hii ambayo sasa tumeinunua na kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata fedha kwa ajili ya kuchimba visima. Tunataka wilaya zetu tuchimbe visima kwenye vijiji ambavyo nina shida ya maji. Kwa mfano pale Busega tunataka tuchimbe visima kwenye Kata za Shigala, Kata ya Igerukilo, Malili, Imalamate na Ngasamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunaomba sasa gari hii itengewe bajeti ili iweze kufanya kazi. Kwa sasa tumeletewa lakini bado haijatengewa bajeti ya kuiendesha gari hii; na ili liende katika mikoa yote. Tutengenezee hivi sasa bajeti ili gari hzi ziweze kufanya kazi. Kila mkoa tupeleke bajeti kufanya kazi. Mfano tupeleke bajeti za mabomba na mafuta ili hizi gari sasa zilete tija kwa Watanzania na kwa kuleta tija ambayo Mheshimiwa Rais anaitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie jambo moja ambalo kila siku tumekuwa tukipata ahadi hapa. Mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Mkoa wote wa Simiyu. Suluhisho kubwa Mheshimiwa Waziri hapa katika Mkoa wetu wa Simiyu ni mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao utaanzia Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu. Mradi huu ndilo suluhisho la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nimekaa hapa Bungeni mwaka huu ni wa tatu napitisha bajeti, kila mwaka mnaandika kilekile kwenye bajeti. Mwaka 2021/2022 mliandika kilekile, mradi huu utaanza mwaka huu na haukuanza. Lakini bado 2021/2022 mkaandika hivyo hivyo na haukuanza mradi huu. Sasa hivi nimesoma hapa mmeandika hivyo hivyo na mradi sujui kama utaanza. Ninaomba sasa tuchukulie maanani katika mradi huu uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikukumbushe, mimi nimeuliza maswali mawili hapa kwenye huu mradi; mwezi Aprili, 2021 niliuza swali nilijibiwa hivi naomba ninukuu majibu yalikuwa hivi kwenye huu mradi; “Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi utaanza mwezi Agosti, 2021 na miji mikuu ya wilaya itakayonufaika ni Busega, Bariadi, Itilima Maswa na Meatu na vijiji vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu umbaliwa kilomita 12 kila upande. Mradi huu umepangwa kutekelezwa kwa miaka minne.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni miaka miwili imeshamalizika na huu mradi haujaanza. Sasa nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hapa niliuliza mwezi Februari, 2022 swali hili hili kwenye mradi huu huu. Majibu yalikuwa hivi, ninanukuu; “Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Nikiri maelekezo ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni kutumia rasilimali toshelevu ikiwemo moto pamoja na maziwa kuhakikisha kuwa matatizo ya maji yanamalizika. Tumepata fedha naomba nirudie hapa tumepata fedha bilioni 400 kwa ajili ya kutumia Ziwa Victoria na kutatua tatizo la maji Mkoa wa Simiyu ikiwemo Busega, Bariadi na Itilima. Kwa hiyo mkakati wa Serikali sasa hivi tupo hatua ya kumpata mkandarasi na tupo hatua za mwisho. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mkandarasi atapatikana mapema na kwa wakati ili utekelezaji wa mradi huu uanze mara moja.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni mwaka na nusu nini maana yake? Lazima tuwe serious na kazi hii ambayo tunataka wananchi wetu tuone wanapata. Tunatamani wananchi wapate maji. Lakini bado, katika mwaka huu wa fedha inaandikwa tena hivi; ninanukuu; “Hadi mwezi Aprili 2023 kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kimetumika kulipa fidia kwa wananchi. Aidha taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi zinaendelea na utekelezaji unatarajiwa kuanza katika mwaka 2023/2024”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Habari ya mkandarasi itaisha lini? Kwa sababu kila mwaka ni mkandarasi kila mwaka ni mkandarasi Mheshimiwa Waziri mimi shilingi yako nakimbia nayo Busega, naomba kesho ukisimama utupe commitment ya Serikali kwenye huu mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria wa Mkoa wa Simiyu tunatamani wananchi wa Mkoa wa Simiyu tuondokane na tatizo la maji. Ni aibu leo kuzungumza Busega haina maji wakati kata ya mwisho kwa umbali ni kilometa 42 haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha kesho atupe commitment ya Serikali, haya maneno yaliyoandikwa hapa yaliandikwa 2021 yaliandikwa 2022 yameandikwa 2023 leo tunataka commitment ya Serikali ili wananchi wetu waweze kupata maji safi na salama kupitia Mradi wa Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nataka nichangie kwa Wizara ya Maji ni kuhusu wakandarasi. Sasa hivi wakandarasi wanalaamika hawajalipwa fedha. Sasa ni muda ambao tunatakiwa tutafakari tunapoingia kufanya kazi na wakandarasi tuhakikishe kwamba fedha zipo, wanapo-raise certificate tuwalipe kwa wakati ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni muda mrefu wakandarasi wetu wa miradi ya maji, miradi ya barabara hawajalipwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aangalie wakandarasi wake awalipe ili waweze kufanya kazi, kwa sababu kama hawatalipwa kwa wakati, tuta-raise riba, tuta- raise kucheleweshwa kwa kazi za wakandarasi. Ili kazi za wakandarasi zimalizike kwa wakati na ili wananchi wanufaike na miradi hii, ni lazima miradi hii imalizike kwa wakati. Ikiwemo kuwalipa wakandarasi kwa wakati ili waweze kufanya kazi ambazo tumewapa. Bila kuwalipa kwa wakati kwanza kunawarudisha nyuma, kunachelewesha miradi, kunaongeza gharama za miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na–declare interest kwamba niko Kamati ya PAC, kila miradi inaongezeka gharama zake kwa sababu ya kuchelewesha kuwalipa na tatizo hili sasa limeanza. Wakandarasi huko site wanalalamika, wengine wameshafikisha asilimia 75 za miradi, asilimia 80 lakini wamesimama kwa sababu hawajalipwa fedha zao. Ni wakati muafaka sasa tuweze kuwalipa ili wafanye kazi ambazo tumewapa na kuwatuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa, maana bado nina muda dakika mbili naziona hapa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)