Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimpwekeshe Mwenyezi Mungu na kumhimidi kwa neema kubwa ya Rais wetu tuliyenaye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na watendaji wake mahiri, wazalendo, wenye kupambana kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa jitihada kubwa na mahangaiko makubwa mnayoyafanya kuhakikisha
rasilimali maji inakuwa chanzo kikuu cha maendeleo ya Taifa letu. Lazima tuwe wakweli kwamba Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu Waziri wake wamekuwa wanahangaika sana kipindi kirefu kwa sababu, ni miaka mingi miundombinu ya maji haikuwa inafanyiwa matengenezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya maji ni chakavu Tanzania hii, na ndiyo sababu imesababisha katikakatika ya maji kila kukicha. Kwa hiyo, Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa kuanza kuboresha miundombinu ya zamani ya maji pamoja na miradi ile chechefu ambayo imeshafanyika, pia kutengeneza miundombinu mipya ya maji. Naipongeza sana sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan. Hakika imedhamiria kabisa kuleta huduma bora kwa wananchi wa Tanzania. Bila shaka, haihitaji tochi. Kazi kubwa ya Mama Samia Suluhu Hassan inafanyika, na watendaji wake wako mahiri kabisa kuhakikisha wanafanya kazi vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania amesema Waziri leo wakati anazungumza kwenye hotuba yake na Mheshimiwa Kapufi naye amezungumza, ni kwamba, sisi Tanzania ndiyo wa kwanza Afrika kuwa na maziwa makubwa Afrika nzima. Pia Tanzania ndiyo wa pili Afrika ukiacha DRC Kongo kwa water bodies. Vile vile, kiukweli so far so good, rasilimali maji hii tunavyoiangalia, ni kwa jicho la huduma tu zaidi, hatujaangalia potential kubwa ya maji tuliyonayo Tanzania katika upande pia wa kuongeza mapato ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Naomba niseme wazi, kaka yangu, Mheshimiwa Aweso, nakupenda sana, unajua; na umewasifia sana watendaji wako, ni vizuri kuwa na imani kubwa na watendaji wako, ni jambo jema, lakini mimi nasema hapa, Wahandisi wa rasilimali maji wa Bodi za Mabonde ya Maji, bado hawajafanya assignment yao sawasawa kukusaidia kufanya kazi yako vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Mpaka leo, juu ya potential kubwa tuliyonayo ya maji, hatuna Integrated Water Master Plan Tanzania, hatuna. Kamati imezungumza hapa kwamba tunahitaji National Water Master Plan. Master Plan tulizokuwanazo mpaka sasa ni za mikoa mikoa; ya Mkoa wa Tanga ni ya mwaka 1976; ya Mkoa wa Ruvuma, Kigoma na Iringa ni ya mwaka 1982. Ukisoma Water Master Plan zile za mikoa, utagundua kwamba inaonesha tu maeneo ambayo unaweza kupata maji, lakini hakuna details za undani zaidi, kwa maana maji yale yako kwa kiwango gani? Maji yale yana ubora gani? Naamini wahandisi wa rasilimali maji, kama watafanya tafiti ipasavyo, hivi vitu vinaweza kujulikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yake ni nini? Madhara ya kutokujulikana kiwango cha maji kilichopo. Leo umetutajia uhitaji wa maji kwamba ni Shilingi bilioni 60 meter cubic, lakini hizo nina uhakika umeangalia consumption per person, ukazidisha na idadi ya Watanzania. Kwa hiyo, watu wa bodi za maji wanapaswa kufanya tafiti kujua underground water scope ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na kasumba kubwa ya kuchimba visima. Tunachimba sana visima na Wabunge hapa tunaonekana tunahitaji sana kuchimba visima, lakini bodi za maji ndiyo zinapaswa kututengenezea mechanism ya kuhakikisha visima vile vitaendelea kuwa na maji. Hiyo inawezekanaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima wa-establish coordinates katika visima vilivyopo sasa na waweze kuonesha underground water channel, relationship yake na kisima kipya kinachojengwa. Kwa sababu mkondo wa maji una tabia wa kunyang’anyana maji. Visima vingi vikichimbwa sehemu moja, bila kujua capacity yake kule chini, ina maana kwamba kisima kimoja kitanyang’anya maji upande mwingine, at the end of the day ni kwamba visima vinakauka na hakuna sustainability. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimshauri sana kaka yangu kipenzi, watu wa bonde za maji wafanye tafiti ya kutosha, watuambie scope ya underground water. Kwa sababu huwezi kufanya management yoyote ya maji kama hujui capacity uliyonayo underground. Leo miji inatanuka, watu wanaongezeka, tunachimba visima kiholela, mwisho wa siku inaonekana miradi siyo sustainable, kwamba maji hayatoshi, maji yanakatika, ni kwa sababu bodi za maji; Wahandisi wa Rasilimali Maji hamjafanya tafiti za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mumsaidie ndugu yangu yule. Mheshimiwa Aweso ni mzalendo, anapambana, na ana maono mapana kwa ajili ya Wizara hii ya Maji. Msaidieni vya kutosha. Anaweza kufanya makubwa zaidi mkimpa mawazo. Ninyi ni wataalam, mko pale, fanyeni assignment yenu sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia, katika nchi ya Uholanzi, wenzetu sasa hivi, ile distribution ya water supply, anakaa ofisini, anai-monitor through GSI Technic (Geographical Information System Technic), inamwezesha ku-monitor distribution ya water supply. Hii ndiyo imesaidia ku-manage upotevu wa maji. Tuna maji mengi yanapotea lakini hatuna proper management ya upotevu wa maji. Sisi tuna wadau, tuna wahisani, tunashirikiana na nchi mbalimbali na wadau wako tayari, tunashirikiananao, watuwezeshe upande huu ili tuweze kudhibiti upotevu wa maji kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kufanya tafiti za kutosha, ina maana tutaweza hata kuvuna maji, tutaweza hata kuondoa chumvi kwenye maji, lakini watu wa mabonde ya maji bado hamjafanya assignment yenu sawasawa, na potential kubwa ya maji tuliyonayo Tanzania, bado hamjaiangalia kwenye jicho la kiuchumi. Miundombuni imekuwa chakavu muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga uwekezaji mkubwa ulifanyika kuanzia miaka 1990 na 1995. Wakati huo miundombinu yote imeshakuwa mibovu, maji yanakatika kila siku. Ina maana hakuna proper strategic maintenance program ya miradi ya maji. Kwa nini leo imeji-accumulate miradi mingi kwa wakati mmoja? Ni kwa sababu hiyo. Huko nyuma mmeshindwa kufanya ipasavyo. Sasa msimwangushe Mheshimiwa Aweso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso amekiri wazi kwamba, ule usemi wako unasemaje? Ukinizingua, tutazinguana. Yuko very serious na anachokifanya, msimzingue. Tunatamani Wahandisi mfanye kazi zenu vizuri, kwa ueledi na maarifa. Fanyeni tafiti za kutosha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eng. Mwanaisha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MWENYEKITI: Ahsante. Nilikuwa…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia mbili na tano. (Makofi)