Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutuletea maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Watendaji Wakuu wa Wizara na Watendaji wote wa RUWASA nchi nzima, lakini zaidi Meneja wetu wa RUWASA, Mkoa wa Kagera, Ndugu yangu Warioba, mtani wangu; na Meneja wetu wa Wilaya Muleba, Jerome. Ni watendaji wazuri sana, wanafanya kazi iliyotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea suala la upotevu wa maji. Mheshimiwa Waziri naomba hili uliangalie sana. Ukiangalia standard ya ulimwengu, upotevu wa maji haupaswi kuzidi asilimia 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko kwenye Kamati ya PIC, mamlaka nyingi ambazo tumezitembelea, unakuta wanaongelea upotevu wa maji zaidi ya asilimia kati ya 30 mpaka 40. Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji wakati anachangaia hapa, amesema mabomba mengi yanapasuka, na yanapopasuka hatuchukui hatua za haraka kwenda kuyaziba. Hapa ndipo tatizo lilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, huu upotevu wa maji, mara nyingi sana sisi ambao tumefanya kazi ya kuwalinda walaji, nimefanya kazi kwenye hiyo sekta. Unakuta unabebeshwa watumiaji kwa makosa ambayo yanafanywa na watu wengine, wanakuja kubebeshwa watumiaji. Naomba Waziri uliangalie hili, uwasisitize watendaji wako wawe wanachukua hatua za haraka kuziba mabomba ambayo yanapasuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri, jana tulikutana na management yake pale Wizarani. Kilichonipeleka pale Wizarani ilikuwa ni Mradi wa Muleba wa kutoa maji Ziwa Victoria. Huu mradi nimeuongelea mara nyingi sana. Tangu nije hapa, ni mwaka wa tatu naongelea mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea mwaka huu nitakuta kwenye bajeti, lakini nashukuru kwa commitment aliyotoa Mheshimiwa Waziri jana, na kwa commitment hiyo nategemea bajeti ya mwaka kesho, tulishauriana tukakubaliana kwamba sasa tutautekeleza kwa awamu. Nami nakubaliana na pendekezo la Mheshimiwa Waziri. Sasa isiishie hapa, au pale mezani ofisini kwake. Naomba mwaka kesho nilione kwa vitendo, na hii itampa heshima sana Mheshimiwa Waziri, na zaidi itampa heshima sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wilaya ya Muleba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu kuona wilaya ambayo iko pembezoni mwa ziwa tunahangaika na maji. Tuna miundombinu ya maji, tuna maji pembezoni mwa kata zetu, lakini hatuna maji. Mheshimiwa Waziri nakuomba hili ulichukue kwa uzito wake, na tukipata mradi huu wa Ziwa Victoria wa kuhudumia kata sita, itatusaidia, hasa maji yanayotumiwa Kata ya Muleba, sasa yataweza kusaidia Kata za Ikondo, Kata ya Kibanga na Kata ya Biirabo na Kata ya Nshamba, tutakuwa tumehudumia hizo kata nyingi kwa mradi huo mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara, tuna miradi mipya miwili. Tuna mradi wa Chebitembe Kisana kwenye hii bajeti, lakini tuna mradi mwingine wa Bushagara. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais kwa miradi hii na miradi mingine ambayo inaendelea. Naomba hiyo miradi mingine ambayo inaendelea isije ikasimama. Kazi kubwa imefanyika, na inaendelea kufanyika, tunaomba sasa kama wachangiaji wengine walivyosema, wakandarasi wale wapewe fedha ili miradi iendelee kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kata zetu ambazo ziko visiwani. Tuna kata tano Wilaya ya Muleba. Tuna Kata ya Ikuza, Kata ya Mazinga, Bumbire, Kerebe na Goziba. Hizi ni kata ambazo ziko katikati ya Ziwa Victoria. Tunakuomba utengenezwe utaratibu mzuri, kwani wenyeji wa kule ni wavuvi lakini hawana maji safi na salama, wanatumia maji ya ziwa ambayo siyo salama kwao. Tunakuomba ututengenezee utaratibu mzuri, angalau bajeti ya mwaka kesho hizi kata ambazo ziko katikati ya ziwa na wenyewe tuwakumbuke, ni Watanzania wenzetu na wanastahili kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa hili, Wilaya ya Muleba, hasa Muleba Magharibi, tulikuwa na matatizo makubwa sana. Mheshimiwa Waziri tuliongea jana ofisini kwako na umetupa commitment kwamba gari likitoka Karagwe liende Wilaya ya Muleba kuchimba visima kwenye hizi kata ambazo zina uhaba mkubwa sana wa maji hususan Kata za Kyebitembe nashukuru kuna Mradi wa Kyebitembe sana.

Mheshimiwa Mweyekiti, umetupa visima kwenye hizo baadhi ya kata. Kata ya Burungura, Kasharunga na Kata ya Karambi, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa commitment hiyo natumaini sasa mwaka kesho tutakapokuja hapa hatutakuja kuimba wimbo uleule, kibwagizo kilekile nakuomba tuendelee kufanya kazi tutakuunga mkono na bajeti yako mimi kwa commitment hii jana nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru na la mwisho kwamba nilikuwa na tatizo sana kwenye kijiji changu cha Msalala. Mheshimiwa Waziri kati ya visima ambavyo tumepata visima 10 Wilaya ya Muleba nakuomba na utoe maelekezo mahususi, kisima cha Chakaseni kuchimbwe Msalala, kule eneo la Msalala wana matatizo makubwa sana ya maji, wananunua ndoo moja ya maji mpaka shilingi 1,000 kwa sababu ya uhaba huo wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mmeishatoa commitment kwamba kisima kinakwenda kuchimbwa pale nikuombe Mheshimiwa Waziri utoe maelekezo wakati unatoa hotuba yako ya mwisho na natumaini na watendaji wako wa RUWASA Kagera wakachimbe kisima cha kwanza lile eneo la Msalala, umetupa kisima kimoja nadhani hakitoshi. Mheshimiwa Waziri kwa busara yako kwa sababu kuna watu wengi sana pale na ni mkusanyiko wa watu wengi hasa wavuvi na wanaokuja kununua dagaa ungetuongezea kimoja viwaka viwili watu wa Msalala watakushukuru sana na tutakutafutia samaki utakapo tembea Mkoa wa Kagera kuna guest house nzuri pale ukalale pale watakuandalia chakula kizuri sana kwa heshima utakayokuwa umewapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, niwatakie utendaji mwema wa kazi haya maelekezo mahususi ulimpatia Katibu Mkuu dada yangu Nadhifa kuhusu suala la kata sita kutoa maji Ziwa Victoria waandae kazi hiyo kwa haraka iweze kutekelezeka mwaka kesho niione kwenye bajeti. Ahsante sana. (Makofi)